Writen by
sadataley
1:33 PM
-
0
Comments
Na Alawi Masare, Mwananchi
Dar es Salaam. Utafiti mpya umebaini kuwa
Tanzania inapoteza zaidi ya Sh3 trilioni kila mwaka kutokana na ukwepaji
kodi unaofanywa na kampuni za uchimbaji madini na katika uingizaji
bidhaa na kuuza nje.
Shirika la kiuchumi lenye makazi yake Marekani
(GFI), lilitoa ripoti yake mwishoni mwa wiki iliyopita likieleza kuwa
Tanzania inaongoza kwa kupoteza fedha nyingi zaidi kutokana na
udanganyifu huo miongoni mwa nchi tano zilizofanyiwa utafiti za Kenya,
Uganda, Ghana na Msumbiji.
Kiasi cha fedha kinachopotea kila mwaka, kingeweza kujenga zahanati 374 za kisasa kwa Sh8.1 bilioni kila moja.
Vilevile, utafiti huo umeonyesha kuwa kiasi hicho
kinachopotea kingeweza kulisaidia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
kuzalisha nishati ya kiasi cha megawati 1,800, tatizo ambalo limekuwa
sugu kwa miongo mingi.
Pia, kiasi hicho kingeliwezesha Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL) kununua ndege 30 aina ya A320 ambayo hugharimu dola 60
milioni kila moja. Hivi karibuni Shirika la Ndege la Afrika Kusini
lilinunua ndege hiyo.
Udanganyifu katika mauzo ulionekana zaidi katika uingizaji mafuta yenye msamaha wa kodi kwa kampuni za madini.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa huenda kampuni za
madini hupandisha gharama za uingizaji wa nishati hiyo ili kuhamisha
fedha nje ya nchi kwa njia haramu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango ambacho Tanzania hupoteza kila mwaka ni sawa na asilimia 16 ya bajeti ya sasa.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa kiasi kinachopotea
ni mara tatu ya kile ambacho Serikali ilitangaza kukopa kupitia
mashirika ya mikopo yenye masharti nafuu katika bajeti yake ya sasa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania inafuatiwa na
Kenya ambayo inapoteza Sh131 bilioni za Kenya (Sh2.489 trilioni), Ghana
Dola za Marekani 1.44 bilioni (Sh2.304 trilioni) na Uganda Sh2.2
trilioni za Uganda (Sh1.4 trilioni) na Msumbiji iliyopoteza Dola za
Marekani 585 milioni (Sh936 bilioni).
No comments
Post a Comment