Writen by
sadataley
4:19 PM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe na Nuzulack Dausen, Mwananchi
Dar es Salaam. Serikali itawasilisha bungeni rasimu ya maboresho
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo itafuta misamaha ya kodi
hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema jana kwamba mpango huo
unafanyiwa uchambuzi na Serikali na kwamba utawasilishwa katika Bunge la
Bajeti wiki mbili zijazo.
Kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa CUF ambaye pia
ni mtaalamu wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa akipigia kelele
juu ya wingi wa misamaha ya kodi akisema imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa
cha mapato ya Serikali.
Profesa Lipumba alisema hivi karibuni kuwa ili
kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi, Serikali inatakiwa kufuta kabisa
misamaha holela ya kodi inayofikia Sh1.8 trilioni ambayo ni sawa na
asilimia tano ya pato la taifa.
Siku tano zilizopita, Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya, wakati akiwasilisha mpango wa Bajeti ya mwaka 2014/15 kwa
wabunge, alisema Serikali imepanga kukamilisha utungwaji mpya wa Sheria
ya VAT.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na kuongeza
wigo wa kodi kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kuanzisha vyanzo vipya
pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo rasmi wa
kodi.
Katika bajeti ya mwaka 2013/14, Serikali iliondoa msamaha wa VAT kwa viwanda vya nguo vinavyotumia pamba ya ndani.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya taasisi ya CRC
Sogema ambayo inaishauri Wizara ya Fedha, misamaha chini ya Kodi ya VAT
ilifikia Sh802 bilioni kwa mwaka 2012, wakati jumla ya misamaha yote
ilikuwa Sh1.8 trilioni.
Ripoti hiyo ya mwaka 2013 inasema: “Matokeo ya
utafiti huu muhimu yanapendekeza kuwa kuna ufanisi zaidi kwa nchi
zinazoendelea kujikita zaidi katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji
kuliko kutoa misamaha ya kodi kwa mashirika.”
Jana, Lukuvi alisema: “Serikali ina mpango huo na
hivi sasa rasimu ya VAT bado inaandaliwa na jambo hilo lipo mikononi mwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema hakupatikana jana kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika
maandalizi ya rasimu hiyo.
Hatua hiyo imepokewa kwa mitizamo tofauti na baadhi ya wachumi,
wengine wakisema itaongeza mapato ya Serikali tofauti na ilivyokuwa
awali na wengine wakisema itawaumiza zaidi wananchi.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Humphrey Moshi alisema ni hatua nzuri ambayo itaongeza mapato kwa
Serikali kwa sababu taasisi nyingi zilikuwa zikitumia vibaya misamaha
hiyo.
“Fedha zitakazopatikana zitumike vizuri kwa
kugharimia miundombinu, kutoa huduma bora za elimu na afya na si posho
na vikao visivyo na tija,” alisema.
Alisema hata kama Serikali itaondoa misamaha hiyo,
bado ina wajibu wa kufanya uchambuzi wa kina na kuujulisha umma kuwa ni
taasisi gani zilitumia vibaya misamaha hiyo.
Hata hivyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine (Sua), Dk Damian Gabagambi alisema hatua hiyo
ikifanikiwa itaathiri jamii kwa kuwa baadhi ya taasisi zilizokuwa
zinasamehewa kodi zilikuwa zikisaidia kwa kiasi kikubwa.
Alisema Serikali na baadhi ya watu wanaopinga
misamaha ya kodi wamekuwa wakiangalia upande wa gharama au hasara
inayotokana na misamaha hiyo bila kuangalia faida zake.
“Nipo tofauti kabisa na wanaounga mkono hatua
hiyo; kwa sababu taasisi nyingi kama mashirika ya dini yamekuwa yakitoa
huduma nzuri kwa wananchi. Wasikurupuke kuondoa misamaha kwa
kuwafurahisha watu,” alionya Dk Gabagambi.
Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ilishindwa kufanya uchunguzi wa kina kugundua ni kina nani waliokuwa
wakitumia vibaya misamaha hiyo kutokana na usimamizi mbovu.
“Unapokuwa umetoa misamaha ni lazima uweke mifumo
mizuri ya ufuatiliaji kubaini watu watakayoitumia vibaya, lakini TRA
hawatumii mfumo huo,” alisema.
Alisema iwapo Serikali itafuta misamaha hiyo kuna
uwezekano mkubwa wa kuwepo madhara makubwa katika uwekezaji, ajira na
huduma kwa jamii kwa kuwa baadhi ya mashirika yanayosamehewa kodi
yalikuwa yanaajiri watu wengi na kutoa huduma nzuri.
Serikali imekuwa ikitafuta vyanzo mbalimbali vya
mapato na moja ya hatua ilizochukua ni kuhamasisha matumizi ya Mashine
za Risiti za Kielektroniki (EFD) ili kuziba mianya ya wakwepa kodi.
Hata hivyo, mashine hizo zimekuwa zikipingwa na baadhi ya wafanyabiashara kwa madai kuwa ni ghali.
Mkakati mwingine ni kuanzisha kodi ya kila mwezi ya matumizi ya kadi za simu ambao haukufanikiwa kutokana na kupingwa na wadau mbalimbali.
Mkakati mwingine ni kuanzisha kodi ya kila mwezi ya matumizi ya kadi za simu ambao haukufanikiwa kutokana na kupingwa na wadau mbalimbali.
No comments
Post a Comment