Writen by
sadataley
3:30 PM
-
0
Comments
Serikali imetenga zaidi ya Sh700 milioni kwa ajili ya kukabiliana na
ugonjwa wa Homa ya Dengue ambayo imeendelea kushika kasi huku wengine
wakipoteza maisha.
Na Suzan Mwillo, Mwananchi
Dar es Salaam. Serikali imetenga zaidi ya Sh700 milioni kwa
ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Homa ya Dengue ambayo imeendelea
kushika kasi huku wengine wakipoteza maisha.
Tangu kuanza kwa ugonjwa huo Januari mwaka huu
hadi kufikia juzi jumla ya wananchi 494 wa mkoani hapa walipimwa na
kugundulika kuwa na vimelea vya homa hiyo, kati yao akiwamo Daktari
Bingwa wa magonjwa ya akili nchini, Gilbert Buberwa wamepoteza maisha
kutokana na ugonjwa huo.
Akizungumzia kuhusu fungu hilo, Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema mkoa ni hapa halmashauri
imetenga jumla ya Sh218 milioni zinazotumika kwa sasa katika kupambana
na ugonjwa huo.
“Fedha hizo zinatumika kwa sasa katika kutoa
huduma mbalimbali za dharura kwa wananchi wa mkoa huu kutokana na homa
hiyo wakati tukiendelea kutafuta vyanzo vingine ili kuongeza kasi ya
mapambano haya,” alisema Sadiki.
Mkuu huyo alifafanua kuwa katika fedha hizo kila
manispaa itatumia kiasi chake na Manispaa ya Temeke itatumia kiasi cha
Sh24 milioni, Ilala Sh32 milioni na Kinondoni Sh150 milioni.
“Tayari manispaa hizo zimeanza kufanyia kazi fedha
hizo kwa kuendesha shughuli mbalimbali za kutoa elimu kwa wakazi wa
maeneo husika, ikiwamo elimu ya usafi ambayo ndiyo msingi wa kuepukana
na ugonjwa huu,” alisema Sadiki na kuongeza pia watanunua vifaa vya
kupimia wagonjwa (Test kits) vitakavyokuwa vinatumika katika hospitali
za manispaa hizo.
Hata hivyo Sadiki alisema hatua hizo ni za mwanzo na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kupambana na ugonjwa wa dengue.
Akizungumzia Sh500 milioni zilizoahidiwa bungeni
mapema wiki hii na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe
Stephen Kebwe, Sadiki alisema fedha hizo bado zinashughulikiwa na mfuko
wa Hazina na pindi zitakapotoka basi zitaongeza nguvu katika mchakato wa
kupambana na homa hiyo nchini.
Sadiki alisema mbali na hatua hiyo zoezi la kuweka
viua vijidudu kwenye maji yaliyotuama ili kuwaangamiza viluilui wa mbu
linaendelea, hadi sasa jumla ya kata 58 zinaendelea kuweka viuadudu na
kuharibu mazalia ya mbu.
Mkuu huyo alisema kuwa zoezi la kunyunyiza dawa
litafanywa nao kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na
Nchi Kavu (Sumatra) kwenye magari 600 yanayofanya safari zake kati ya
Dar es salaam na mikoani.
“Bado tunaanda utaratibu huo ambao utaanza haraka
iwezekanavyo kwa sababu kumekuwa na uvumi kuwa watu wanaotoka Dar es
salaam ndiyo wanaosambaza ugonjwa huu na endapo tutabaini kuwa kuna gari
linaloenda mikoni bila ya kunyunyizia dawa basi tutafungia gari hilo
kufanya safari,” alisema Sadiki.
No comments
Post a Comment