Writen by
sadataley
1:24 PM
-
0
Comments
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Dodoma. Mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), ya kuitaka Serikali kutowateua wabunge
kuwa wajumbe wa bodi za mashirika ya umma, hayajatekelezwa kwa miaka
mitatu mfululizo.
Ripoti ya CAG ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa
mwaka 2013/2014 iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma imesema mapendekezo
hayo yaliwasilishwa kwa mara ya kwanza 2008/2009.
Katika ripoti hiyo, CAG Ludovic Utouh amesema
katika mkutano wa uwajibikaji uliofanyika Januari 23 na 24, 2009
iliamuliwa kuwa wabunge ambao ndiyo wasimamizi wa sheria kikatiba,
wasiteuliwe kuwa wajumbe wa bodi za mashirika ya umma.
“Mwenendo huu ni wa kipekee na upo Tanzania tu na
hautumiki mahali popote katika jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama
wake na hata nchi yoyote duniani,” alisema CAG Utouh katika ripoti hiyo
na kuongeza: “Nimerudia pendekezo hili kwa miaka mitano mfululizo bila
kutekelezwa na mamlaka husika.”
Kisheria, Rais huteua mwenyekiti wa bodi husika na waziri mwenye dhamana huteua wajumbe.
Aidha, CAG alisema kanuni za utawala bora zinataka
watendaji wakuu wa mashirika ya umma wateuliwe na bodi za wakurugenzi
wa mashirika hayo badala ya kazi hiyo kufanywa na Rais.
“Ili kumpunguzia mzigo Mheshimiwa Rais, ninashauri
angeachiwa jukumu la kuteua wenyeviti wa bodi za wakurugenzi wakati
uteuzi wa maofisa watendaji wakuu liwe ni jukumu la bodi,” alisema.
CAG alisema mfumo huo utaziwezesha bodi za
wakurugenzi kuziwajibisha menejimenti za mashirika ya umma pale viongozi
hao watakaposhindwa kuwajibika ipasavyo.
No comments
Post a Comment