Writen by
sadataley
1:38 PM
-
0
Comments
Tuliwahi kusema kupitia katika safu hii kwamba vituko vingi vinavyotokea hapa nchini ni vigumu kutokea katika nchi nyingine. Tulikuwa na maana kwamba nchi yetu ina matukio mengi ya ajabu na ya aina yake. Sote tunatambua kuwa iwapo matukio hayo yangetokea katika nchi nyingine, yangeonekana kama maajabu na kusababisha mitafaruku kiasi cha viongozi kuwajibika kwa kujiuzulu nyadhifa zao.
Habari kwamba uwasilishwaji bungeni wa Bajeti ya
Wizara ya Maji na ya Nishati na Madini umesogezwa mbele kutokana na
kasoro mbalimbali, zinathibitisha jinsi nchi yetu ilivyo ya ajabu. Muda
wa mwaka mmoja wa kutengeneza bajeti ni mrefu. Hakuna ubishi kwamba muda
huo siyo tu unatosha, bali pia ni mwingi mno kulinganisha na uzito wa
kazi hiyo ulivyo. Serikali imesema bajeti hizo zimesogezwa mbele kwa
sababu “hawajaweka bajeti zao vizuri”. Hayo ni maajabu ambayo hutokea
Tanzania pekee.
Lakini kama Serikali inaweza kushindwa kutambua
umuhimu wa bajeti kwa uchumi na maendeleo ya taifa, badala yake
inatanguliza siasa na kusababisha uwasilishaji wa bajeti isiyokidhi
vigezo, kwa maana ya bajeti iliyofanyiwa kazi kwa weledi na umakini,
wananchi wanayo kila sababu ya kuhoji utendaji huo wa Serikali. Kwa
upande mwingine, hali hiyo ilitarajiwa kwa kuwa mawaziri wote wa
Serikali, ambao walitegemewa kusimamia sera zinazoongoza masuala ya
utayarishaji wa bajeti za wizara zao walihamia Dodoma kwa siku 70 eti
kushiriki katika Bunge Maalumu la Katiba. Hatuoni kama ilikuwa busara
kwa mawaziri wote kuwa sehemu ya Bunge hilo na kupoteza muda katika
kupiga siasa wakati masuala muhimu kama bajeti yakiwa yamewekwa kando.
Bajeti za wizara hizo sasa zitasomwa mwezi ujao.
Wakati Wizara ya Maji ilikuwa iwasilishe bajeti yake jana, Bajeti ya
Wizara ya Nishati na Madini ilipangwa kuwasilishwa Ijumaa ijayo. Sasa
tunaambiwa kwamba Serikali imemwandikia Spika barua ikimwomba asogeze
mbele uwasilishwaji wa bajeti hizo za Mwaka wa Fedha wa 2014/15. Sisi
hatuoni uwezekano wa Spika kulikataa ombi hilo la Serikali. Hata hivyo,
tunadhani lingekuwa jambo jema iwapo mamlaka husika zingewawajibisha
viongozi wa wizara hizo kutokana na kutayarisha bajeti zisizotekelezeka.
Kutokana na kushindwa kusimamia wizara zake katika
utayarishaji wa bajeti, Serikali imejiweka katika wakati mgumu. Baadhi
ya mawaziri na watendaji wao wakuu wamekuwa wakidhalilika katika
kuwasilisha bajeti zao kutokana na Kamati ya Bunge kuzikataa bajeti
hizo. Wakati mwingine, Serikali imekuwa ikitoa visingizio kama
ilivyofanya juzi kwa kusema kwamba wizara hizo hazitawasilisha bajeti
bungeni kwa kuwa bado Serikali inafanya mazungumzo na Wizara ya Fedha,
huku Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akikanusha kuwapo kwa jambo hilo.
Zipo fununu kwamba Serikali inaogopa kuwasilishwa
kwa bajeti hizo baada ya kubaini kwamba wabunge wengi wamekamia
kuzikwamisha kutokana na miradi mingi iliyopangwa mwaka jana
kutokamilika.
Tunadhani wabunge wana haki ya kuzikataa bajeti za
wizara hizo kama hazitaendana na uhalisia kwa kuwa ndizo zilizopewa
kipaumbele katika mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Wabunge kamwe wasikubali kuburutwa. Tunataka wakomalie bajeti ya wizara
yoyote iliyotayarishwa kisanii, kiujanjaujanja na isiyokuwa na uhalisia.
Habari kwa hisani ya http://www.mwananchi.co.tz
Habari kwa hisani ya http://www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment