Latest News

GNM Cargo

GNM Cargo
GNM CARGO & LOGISTICS

menu

Thursday, December 12, 2013

Ni vilio vitupu A. Kusini

Mjane wa Rais wa Kwanza Mazalendo wa Afrika Kusini, Graca Machel akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa mumewe katika Ikulu ya Pretoria nchini humo jana. Picha na AFP 
Na Neville Meena,Mwananchi
Pretoria: Familia ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela jana iliongoza utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa kiongozi huyo, katika tukio ambalo limebadili mwelekeo wa maombolezo tangu alipofariki dunia, Desemba 5, mwaka huu.
Mjane wa Mandela, Graca Machel aliwaongoza wanafamilia katika Ikulu ya Pretoria waliposema ‘buarini’ kwa kiongozi huyo katika tukio ambalo mbali na kufungua pazia ya utoaji wa heshima za mwisho, liliibua simanzi miongoni mwa waliohudhuria.
Mandla ambaye ni mjukuu mkubwa wa Mandela, yeye alikuwa katika Majengo ya Umoja ilipo Ikulu tangu asubuhi na alikabidhiwa mwili kama kiongozi wa familia kutoka kwa Majenerali wa Jeshi la Afrika Kusini (SADF).
Mandla akionekana mwenye mawazo mengi na huzuni kubwa, kutwa nzima alikuwa ameketi pembezoni mwa jeneza lililokuwa na mwili wa babu yake, hadi ulipoondolewa Ikulu na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi saa 11:30 jioni. Wakati familia ya Mandela ikiingia kuaga, jeneza lilikuwa wazi likiacha kioo pekee kilichokuwa kikiwatenganisha na mwili wa mpendwa wao.
Graca alikuwa hatua chache nyuma ya Rais Jacob Zuma na alipofika katika jeneza lenye mwili wa mumewe alisimama kwa sekunde chache akimtazama, kisha akaendelea. Nyuma ya Graca, alikuwa ni Mtalaka wa Mzee Mandela, Winnie Madikizela na mabinti zake wawili, pamoja na wanafamilia wengine, ambao baada ya kutoa heshima zao za mwisho, walionekana wakitumia lesso zao kufuta machozi. Familia hiyo ilifuatiwa na Rais Mstaafu, Thabo Mbeki na Frederick de Klerk ambao waliambatana na wake zao, lakini mke wa de Klerk, Elita alishindwa kujizuia na kuangua kilio.
Kulikuwa na simanzi kubwa miongoni mwa waombolezaji waliofika kutoa heshima zao za mwisho, wakati ambao Rais Zuma pia aliwaongoza viongozi wa nchi mbalimbali kumuaga Madiba.
Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa waliotoa heshima za mwisho akiungana na marais wenzake, wengi wakiwa kutoka Afrika ambao waliondoka jana mchana baada ya kupata fursa hiyo.
Miongoni mwao walikuwa marais wastaafu; Kenneth Kaunda wa Zambia na Joachim Chissano wa Msumbiji.
Marais wengine waliokuwapo na nchi zao kwenye mabano ni Robert Mugabe (Zimbabwe), Joyce Banda (Malawi), Uhuru Kenyatta (Kenya), Ellen Johnson – Sarlief (Liberia), Goodlucky Jonathan (Nigeria) na Michael Satta (Zambia).
Jeneza lenye mwili wa Mandela liliwekwa juu ya kizimba maalumu ambacho kilikuwa kimezungushiwa utepe wenye rangi nyekundu, huku ukiwa umefunikwa na kibanda cha rangi nyeupe kilichojengwa kwa ustadi mkubwa.
Walikuwapo askari wanne wa Kikosi cha Jeshi la Wanamaji wa Afrika Kusini wakizunguka jeneza hilo; wawili mwanzoni na wawili mwishoni, wakiwa wamevalia mavazi meupe, kushika kitara mkononi kila mmoja.
Huzuni PretoriaMji wa Pretoria ambao ni Makao Makuu ya Serikali ya Afrika Kusini, jana ulikuwa katika hali ya majonzi na simanzi ya hali ya juu pale jeneza lililobeba mwili wa Mandela lilipoonekana kwa mara ya kwanza hadharani tangu alipofariki dunia, siku sita zilizopita.
Likiwa limefunikwa bendera ya taifa ya Afrika Kusini, jeneza hilo liliingia katika mitaa na barabara za Pretoria, kuanzia saa 1:00 asubuhi baada ya kuondolewa katika Hospitali ya Jeshi kwa ajili ya kupelekwa katika Majengo ya Umoja (Union Buildings) ilipo Ikulu ya Pretoria.
Itakumbukwa kuwa mara baada ya kifo chake, Desemba 5, mwaka huu saa 2:50 usiku, mwili wa Mandela uliondolewa saa 9:00 usiku wa manane katika makazi yake Mtaa wa Laa Na:12, Houghton, Johannesburg na kusafirishwa usiku huohuo hadi Pretoria.
Tangu wakati huo, jeneza lake halikuwahi kuwekwa hadharani na hata katika ibada iliyofanyika juzi katika Uwanja wa FNB (Soccer City), Johannesburg na kuhudhuriwa na mamia ya wageni mashuhuri, mwili huo haukuwapo.
Kuonekana kwa jeneza la Mandela hadharani kulibadili hali ya maombolezo kutoka katika nyimbo, kushangilia na kucheza vilivyokuwa vikifanyika tangu kutokea kwa kifo chake na badala yake kuwa hali ya huzuni na majonzi.
Ulinzi mkali
Kulikuwa na ulinzi mkali tangu alfajiri ulioambatana na barabara kadhaa kufungwa na helikopta za SADF na polisi zilihanikiza anga la Pretoria, huku zikitumia muda mrefu kuzunguka Ikulu ambako shughuli za kuaga zilikuwa zikiendelea.
Mamia ya polisi na wanajeshi walikuwa katika maeneo yanayozunguka Ikulu pamoja na maeneo mengine ya Pretoria hasa katika barabara za kuelekea katika Majengo ya Umoja. Magari ya polisi ya aina mbalimbali, malori ya SADF na magari mengine ya kijeshi pia yalionekana katika eneo hilo ambalo si kila mmoja aliyeruhusiwa kuingia.
Maelfu wajitokeza kuaga
Maelfu ya wakazi wa Pretoria wengi nyuso zao zikionekana kuwa za huzuni walijipanga katika barabara za mji huo na baadhi yao walikuwa wakipunga mikono na wengine bendera wakati jeneza lenye mwili wa Mandela lilipokuwa likipita. Baadhi yao walisikika wakiimba, “Rais wangu….rais wangu……”
Tangu kulipopambazuka pia wananchi walikuwa wameanza kujikusanya nje ya majengo ya kuagia na kadri muda ulivyokwenda, idadi yao ilikuwa ikiongezeka na misururu kuwa mirefu. Walilazimika kusubiri hadi saa 5:30 ili kuanza kutoa heshima za mwisho kwa kuzingatia ratiba ilivyokuwa imepangwa.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment