Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, October 15, 2013

Busara itawale mkutano wa JK, wapinzani leo

Mwenyekiti wa kambi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akisalimiana na Rais Jakaya Kikwete huku Mbunge wa Vunjo Augustino Lyatonga Mrema akishuhudia.Picha na Maktaba 
Rais Jakaya Kikwete leo asubuhi anatazamiwa kukutana Ikulu, jijini Dar es Salaam na wenyeviti wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013. Muswada huo umeonekana kwa wengi kuwa na kasoro nyingi, hasa kwa kuzingatia kwamba ulipitishwa katika mazingira ya kutatanisha na Mkutano wa 12 wa Bunge.

Hatuoni sababu ya kutonesha kidonda kwa kueleza kwa kirefu matukio ya aibu yaliyosababisha kuwapo kwa hali ya mfarakano bungeni. Jambo pekee tunaloweza kusema hapa ni kuwa, Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM baada ya wabunge wa upinzani kususia mjadala wa Muswada huo na kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge wakipinga hatua ya Naibu Spika, Job Ndugai kuzima hoja zao.

Kilichoendelea ndani ya Bunge kililitia Bunge doa kubwa, tena la kihistoria. Badala ya wabunge wa CCM waliobaki ukumbini kuujadili Muswada huo kwa umakini mkubwa na kutanguliza masilahi ya taifa kabla ya kuupitisha, walijielekeza zaidi na kutumia muda mwingi katika kutoa kejeli, tambo na matusi ya nguoni dhidi ya wabunge wa upinzani, huku Naibu Spika huyo akiacha hali hiyo ya aibu iendelee.

Viongozi wa vyama hivyo vikuu vya upinzani walipeleka hoja zao kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara wakianzia Dar es Salaam na Zanzibar, lengo likiwa kuwaelimisha wananchi nchi nzima kuhusu upungufu na kasoro zilizomo katika Muswada huo na kuwashawishi waikatae Rasimu ya Katiba Mpya wakati wa kupiga kura ya maoni.

Hata hivyo, kwa kuongozwa na uungwana, busara, ujasiri na uzalendo, Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwezi uliopita aliwashauri viongozi hao wa upinzani wasitishe maandamano na mikutano ya hadhara na badala yake wakae naye meza moja kujadiliana kuhusu kasoro na upungufu uliomo katika muswada huo. Viongozi hao wa upinzani waliitikia wito huo wa Rais Kikwete kwa kauli moja na kusitisha maandamano na mikutano ya hadhara. Matokeo yake ni mazungumzo kati ya pande hizo mbili yanayofanyika Ikulu leo, chini ya Rais Kikwete.

Sisi tunazipongeza pande zote mbili kwa kuweka mbele masilahi ya taifa letu. Tunadhani Rais Kikwete anastahili pongezi za pekee kutokana na kukataa shinikizo la wahafidhina ndani ya Serikali na chama chake ambao tayari walikuwa wametangaza kwamba milango ya Ikulu imefungwa, hivyo hakuna majadiliano kuhusu muswada huo. Ni jambo la kheri kwamba mkuu wa nchi, ingawa Katiba iliyopo sasa inampa uwezo wa kutumia mabavu na ubabe, anatambua kwamba kupatikana kwa Katiba Mpya katika mazingira ya sasa kunahitaji mwafaka wa kitaifa ili kulinda amani na mshikamano na kuepuka kuzuka vurugu na vita nchini.

Ni matumaini yetu kwamba mazungumzo ya leo yataleta mwafaka utakaotupatia Katiba Mpya itakayokidhi matakwa ya Watanzania wote. Ni matumaini yetu pia kwamba pande zote mbili katika mazungumzo hayo zitapata ufunuo wa kung’amua upungufu na kasoro zilizomo katika Rasimu hiyo ili zirekebishwe kwa manufaa yetu sote. Tunawashauri viongozi wa upinzani wajiandae vizuri ili hoja zao zimsaidie Rais Kikwete kuridhia marekebisho katika Muswada huo ambayo yatatuwezesha kupata Katiba Mpya itakayotupeleka kule tunakotaka kwenda.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment