Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, September 14, 2013

Serikali kutafuta mwarobaini kudhibiti dawa za kulevya

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi 
Na Kelvin Matandiko, mwananchi
Dar es Salaam: Serikali kupitia Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, imeanza kutafuta mwarobaini wa kumaliza sakata la usafirishaji wa dawa za kulevya baada ya kuwaomba wadau mbalimbali nchini kushiriki uchangiaji wa maoni ya kuboresha sheria mpya.
Mbali na hilo pia imeomba mapendekezo ya kuunda chombo maalumu na kuanzisha mahakama maalumu ya kuendesha kesi za dawa za kulevya ili kukomesha biashara hiyo nchini.
Hatua hiyo imekuja baada ya siku kadhaa serikali kutangaza kuanzisha chombo hicho, kutunga sheria mpya na kuanzisha kwa mahakama inayojitegemea ili kushughulikia kesi za watuhumiwa kutokana na ongezeko la usafirishaji na utumiaji wa dawa hizo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema tume na sheria zilizopo hazina nguvu ya kupambana na sakata hilo kwa sasa.
“Adhabu zilizopo kwenye sheria ya sasa haziwaogopeshi wafanyabiashara ndio sababu ya kuongezeka kwa matukio hayo, kwa hivyo tunatoa mapendekezo ya sheria hii mpya kwa wadau ili waweze kutoa maoni yao jinsi ya kudhibiti mitandao ya biashara hiyo,” alisema.
Akiwakabidhi waandishi wa habari mapendekezo ya sheria hiyo, Lukuvi alisema Oktoba 30, mwaka huu itakuwa ni mwisho wa kupokea mapendekezo hayo kutoka kwa wadau.
Aidha, Lukuvi alisema mbali na kuwepo kwa Kikosi Maalumu cha Jeshi la Polisi(Task Force), serikali inapendekeza kufanyika kwa maboresho hayo ili kwenda sambamba na mazingira ya sasa.
.“Hata hiyo task force iliyopo kwa sasa haitambuliwi kisheria katika utekelezaji wa jukumu hilo, adhabu zilizopo zimepitwa na wakati ukilinganisha na ilivyokuwa kwa miaka ya 1995 tangu kuanzishwa kwake, kwa hivyo tunataka kuongeza nguvu,” alisema Lukuvi.
Agosti 31, mwaka huu mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa huku Addis Ababa, Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Kukamatwa kwao kumezidi kuongeza idadi ya Watanzania maarufu waliotiwa mbaroni nje ya nchi katika siku za karibuni wakituhimiwa kwa makosa hayo.
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili, wasanii Agnes Gerald Masogange na Melisa Edward kukamatwa kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6bilioni.
Aidha, tukio lingine limetokea baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50milioni (Sh125 bilioni).
Kaniki na Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.

« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment