Writen by
sadataley
11:22 AM
-
0
Comments
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Wakili wa walalamikaji katika rufaa ya kupinga ushindi wa ubunge katika jimbo la Singida Mashariki, Godfrey Wasonga jana alipata wakati mgumu baada ya mawakili wa upande wa walalamikiwa kudai maombi ya kuiondoa kesi hiyo yana lengo baya na pia hayakufuata taratibu za kisheria.
Rufaa hiyo ilikatwa mara baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma kutupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na wakazi wawili wa kijiji cha Makiungu mkoani Singida, Shabani Selema na Paskali Hallu, Aprili 27, mwaka jana.
Walalamikiwa katika rufaa hiyo ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kesi hiyo namba 49 ya mwaka jana, iliendeshwa jana katika majengo ya Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, chini ya jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa likiongozwa Jaji Engela Kileo.
Majaji wengine waliokuwa katika jopo hilo ni Natalia Kimaro na Salum Masati .
Katika kesi hiyo iliyokuwa na mvuto kwa watumishi wa mahakama na wanachama wa Chadema, Wasonga aliwasilisha ombi la kutoendelea na kesi hiyo kwa sababu walalamikaji wametaka kutoendelea na kesi hiyo.
Alisema maombi hayo hayakufuata kifungu namba 102 cha kanuni za mahakama ya Rufaa cha mwaka 2009, ambacho kinamtaka kuleta maombi hayo kabla ya Msajili kupanga siku ya kusikilizwa kwa shauri.
Pia aliomba mahakama iwapo italazimika kufuta kesi hiyo basi iamue pia ni nani atalipa gharama za kesi hiyo,lakini ikizingatia kuwa Selema alipeleka mahakamani kiapo cha kukana kumweleza Wasonga kukata rufaa.
“Sisi tuliosumbuliwa, tutalipwa nani gharama zetu, ninaiomba mahakama kutokubali ombi la ku- with draw (kuondoa) kesi kwasababu limeletwa kwa nia mbaya lakini kama itaipendeza mahakama kuondoa kesi hii basi tunaomba gharama zote azibebe Wakili msomi Wasonga,”alisema na kuongeza.
Haitakuwa haki kuwalipisha gharama za rufaa wakati hakupokea maelekezo kutoka kwao ya kufungua kesi. Ila kwa gharama za mahakama ya chini walipe walalamikaji.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Wakili wa Serikali Mkuu, Vicent Tangoh, ambaye alisema kuwa hata kifungu cha kanuni kilichotumika ya 102 ya Mahakama ya Rufaa, haikuwa sahihi.
Alisema kifungu hicho kinamtaka muombaji kupeleka maombi ya kuondoa kesi kwa msajili wa mahakama na si mahakamani kama alivyofanya Wasonga.“Mahakama haijapewa mamlaka ya kuondoa kesi katika kifungu cha kanuni hii, hivyo maombi yake (Wasonga) hayajakamilika,” alisema Tangoth aliyekuwa akisaidiwa na mawakili wa serikali, Onesmo Mpinzile na Killey Mwitasi.
Alipopewa nafasi ya kujibu hoja hizo Wasonga alisisitiza kuwa hakuweza kuitaarifu mahakama mapema kwa sababu mteja wake (Hallu) alimletea taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na rufaa hiyo Septemba 6 mwaka huu, wakati ambapo tayari msajili wa mahakama alikuwa ameshapanga tarehe ya kesi hiyo.
Hata hivyo, alivyotakiwa kueleza ni kwanini ametumia kanuni hiyo ambayo mawakili wenzake wanasema kuwa si sahihi, Wasonga alisema hakuna kanuni nyingine inayompa nafasi ya kuomba kuondolewa kwa kesi inapofikia katika hatua hiyo na wakati kukiwa na mapingamizi yaliyowasilishwa mahakamani.
Hali hiyo, ilimfanya jaji Kileo kumhoji mara kadhaa kama jambo analolisema kama ana uhakika nalo, “ una uhakika kuwa hakuna kanuni nyingine.”
Jaji Kileo alisema, “hatutaki hapa ustadi wala malumbano ya kisheria, tunachotaka hapa ni haki itendeke kwa pande zote mbili.”
Wakili Wasonga alisema gharama za rufaa hiyo zitalipwa na Hullu (mlalamikaji namba mbili) kwasababu yeye ndiye aliyechelewa kuwasilisha ombi ka kutoendelea na kesi hiyo.
Hata hivyo, kwa zaidi ya mara moja Jaji Kileo alionyesha kukerwa na tabia ya Wasongwa kucheka wakati kesi hiyo ikiendelea. Lakini Wasonga alimjibu, “ndio sura yangu ilivyo mheshimiwa Jaji.”
Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Jaji Kileo aliahiriha kesi hiyo kwa muda wa saa moja na baadaye kurejea na uamuzi wa kuiondoa huku akiamuru gharama za rufaa kulipwa na Hullu.
Jaji Kileo aliamuru gharama za mahakama kuu kulipwa na walalamikaji wote wawili.
“Si sera ya mahakama kulazimisha kuendelea nakesi na kukataa maombi haya (ya kuondolewa kwa kesi ), itakuwa ni kinadharia,”alisema Jaji Kileo.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment