Writen by
sadataley
12:19 PM
-
0
Comments
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Mradi huo ulioanzishwa mwaka 2000 kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupambana na umaskini, umetoa mikopo ya kiasi hicho cha fedha kwa vyama vya kuweka na kukopa mijini na vijijini.
Dar es Salaam. Mradi wa Kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali (Self), umetoa mikopo yenye thamani ya Sh52.6 bilioni kwa vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) tangu ulipoanzishwa mwaka 2000 hadi sasa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupambana na umaskini.
Mratibu wa Mafunzo wa Self, Christopher Ilomo alisema juzi wakati wa kufunga mafunzo ya maofisa ushirika mikoa na warajisi wasaidizi wa ushirika kuwa Saccos 361 nchini zilinufaika na mikopo hiyo.
Ilomo alisema kati ya hizo Saccos 225 ziko vijijini wakati 136 ziko mijini na kwamba mikopo hiyo imewafikia watu 93,334 huku wanawake walionufaika wakiwa 53,605.
Alisema tatizo kubwa la vyama hivyo ni kwamba vimekuwa vikikopeshwa fedha nyingi na taasisi mbalimbali za kifedha lakini vimekuwa vikishindwa kurejesha.
Alitaka maofisa hao kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama hivyo na kwamba wafanye ukaguzi na kutoa taarifa kwa mujibu wa kanuni.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Beatha Swai alisema wakati umefika kwa maofisa ushirika kubadilika na kufanya kazi kwa weledi ili kuvinusuru vyama hivyo.
“ Ule mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unatuhusu sisi sote, ni lazima tuufanyie kazi hata kama sekta nyingine hazijaapa kuutekeleza,” alisema.
Swai alisema wako baadhi ya maofisa ushirika ambao hawavitembelei vyama vya kuweka na kukopa kwa visingizio vingi na kwamba bila kufanya ukaguzi na kutoa ushauri vyama hivyo vitakufa.
Wakitoa risala, washiriki hao walisema kwa kuwa Serikali imeanzisha Tume ya Ushirika, maofisa ushirika wote wawajibike kwa mwajiri mmoja ili kuongeza uwajibikaji ili kuimarisha ushirika nchini.
Akisoma risala yao kwa niaba ya wanachama wenzake, Kessy Abdallah alisema Serikali iongeze ajira kwa maofisa ushirika ili waweze kusimamia vyama hivyo kwa ufanisi zaidi.
No comments
Post a Comment