Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, December 27, 2013

Kuundwa Tume Huru ya Uchaguzi kunasubiri kuwapo machafuko?

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Warioba.PICHA|MAKTABA 
Kama kuna jambo ambalo limewafanya wananchi wengi kukuna vichwa kwa muda mrefu pasipo kupata majibu, ni kutoundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia chaguzi mbalimbali na mchakato wa kupata Katiba Mpya katika ngazi zote zilizosalia, baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kumaliza kazi yake rasmi wiki ijayo.
Kwa maana hiyo, mchakato wa Katiba Mpya unaingia katika awamu ya pili kwa Tume hiyo ya Warioba kukabidhi kijiti cha mbio za mchakato huo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ambayo majukumu yake sasa ni pamoja na kusimamia mambo muhimu mwakani ambayo ni pamoja na: Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura; Kura ya Maoni kuhusu Rasimu ya Tatu ya Katiba Mpya; Utoaji wa Elimu ya Uraia kuhusu upigaji wa kura hiyo na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nec pia ndiyo itasimamia na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Majukumu hayo hakika ni mazito mno kutekelezwa na Nec, ambayo imekuwa na udhaifu mkubwa kiasi cha kupoteza mwelekeo na imani kwa wananchi. Tangu kuanzishwa kwake na Sheria ya Bunge mwaka 1977, Tume hiyo imedhihirisha kwamba siyo huru hata kidogo kutokana na kuonekana machoni mwa wananchi kwamba imo mfukoni mwa Serikali na chama tawala, kwani yamejitokeza matukio mengi ya aibu katika uhai wake wa miaka 36, ikiwa ni pamoja na kuegemea upande wa watawala.
Ndiyo maana siyo wananchi wengi walioshangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Damian Lubuva alipokiri miezi michache iliyopita wakati akitoa maoni ya Tume yake mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa, Tume yake siyo huru. Alishauri kwamba katika mazingira ya sasa ya kuwapo mchakato wa kupata Katiba Mpya, iundwe Tume Huru ya Uchaguzi ili chombo hicho kipate mwafaka wa kitaifa ili kiweze kusimamia mchakato mzima kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, chini ya Katiba Mpya.
Kauli ya Jaji Lubuva imethibitisha pasipo kuacha chembe ya shaka kwamba hoja za muda mrefu za vyama vya upinzani na asasi zisizo za kiserikali kwamba Tume hiyo siyo huru zina mashiko. Tafsiri sahihi ya hoja hizo ni kuwa, siyo tu kwamba Tume hiyo siyo huru, bali pia chombo hicho hakina uwezo wa kusimamia majukumu yake kwa ufanisi kutokana na matatizo ya kisera na kimfumo. Kukosekana kwa utashi wa kisiasa pia kumechangia mno katika kudumaza Tume hiyo, ambayo kwa mujibu wa Katiba iliyopo wajumbe wake wanateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye ni kada namba moja wa chama tawala.
Kitendawili kinachoshindikana kuteguliwa hadi sasa ni sababu za mamlaka husika kutoona umuhimu wa kuwapo mfumo wa kupata Tume Huru ya Uchaguzi ili uende sambamba na kupatikana kwa Katiba Mpya. Lazima tukubali ukweli kwamba Tume iliyopo sasa haikubaliki katika mazingira tuliyomo na ya baadaye. Kama Tume hiyo imekataa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa miaka mingi sasa, kwa mfano, tutegemee nini zaidi ya vurugu, machafuko na umwagaji damu huko tuendako?
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment