Kikosi cha Simba.KOCHA na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ‘King Kibadeni’, amefunguka kuwa kama Simba itaendelea na moto ilionao, basi ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, tofauti na wapinzani wao Yanga ambao wanaonekana kuchoka.
Simba inaongoza ligi kwa pointi 42, ikiwa ni tofauti ya pointi tano dhidi ya Yanga wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 37 wakati Azam wakiwa nafasi ya tatu na pointi 35 hali inayosababisha ushindani kuwa mkubwa.
Kibadeni ameyasema hayo kufuatia kasi ya Simba msimu huu ambapo imefanikiwa kushinda mechi 12 katika michezo 18 iliyocheza, wakitoka sare mechi sita huku wakiwa hawajapoteza mchezo wowote tofauti na Yanga ambao wamefanikiwa kushinda mechi kumi katika michezo 18 na wametoka sare michezo saba huku wakipoteza mmoja.
Kikosi cha YangaAkizungumza na Championi Jumatatu, Kibadeni alisema kuwa Simba ya sasa ina nafasi kubwa ya kuweza kutwaa ubingwa iwapo wataendelea kukomaa na kasi waliyonayo hivi sasa katika Ligi Kuu Bara tofauti na wapinzani wao.
“Ligi ya msimu huu imekuwa ngumu na ushindani mkubwa kwa timu zote lakini kwa hizi timu za juu yaani Simba na Yanga kila moja inaonekana inapambana vilivyo, ila binafsi naona Simba wapo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuweza kutwaa ubingwa tofauti na Yanga.
“Lakini haitakuwa rahisi kama hawataweza kuendelea na kasi ambayo wanayo hivi sasa, kwa sababu ukiangalia wameweza kushinda michezo mingi kwa mabao ya kutosha na ukiwaangalia Yanga wa safari hii ni wazi hawapo vizuri kama tulivyozoea,” alisema Kibadeni.
No comments
Post a Comment