Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA limeongeza tiketi kwa Tanzania kwaajili ya fainali za kombe la Dunia zitakazochezwa Russia mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na TFF, shabiki yeyote anayetaka kwenda kushuhudia fainali hizo za Kombe la Dunia awasiliane na idara ya mashindano ya TFF kwa utaratibu wa namna ya kupata tiketi hizo.
Taarifa imesema Ngwe hii ya pili ya tiketi za Kombe la Dunia imefunguliwa Februari 15, 2018 na itafungwa Machi 12, 2018. Ikumbukwe awali FIFA walitoa tiketi 290 kwa Tanzania ili kushuhudia fainali hizo za Kombe la Dunia kabla ya zoezi hilo kufungwa mwezi Januari na sasa imefunguliwa ngwe nyingine ya tiketi hizo.
Wakati huo huo, TFF imetangaza kwamba hatua ya mzunguko wa Nne (4) wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam inatarajia kuanza kesho Jumatano Februari 21, 2018.
Taarifa imebainisha kwamba kwenye Uwanja wa Sabasaba Njombe kutakuwa na mchezo mmoja utakaowakutanisha mwenyeji Njombe Mji atakayecheza dhidi ya Mbao FC kutoka Mwanza saa 10 jioni.
Mechi nyingine za Kombe la Shirikisho la Azam zitaendelea Jumamosi Februari 24,wakati Singida United watakapowakaribisha Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Namfua saa 10 jioni na KMC watawaalika Azam FC saa 1 usiku Azam Complex.
Jumapili Februari 25, 2018 Buseresere watakuwa uwanja wa Nyamagana Mwanza saa 8 mchana kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro,Majimaji FC ya Ruvuma watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Majimaji kuwakaribisha Young Africans ya Dar es Salaam saa 10 jioni wakati Ndanda FC watakuwa ugenini kucheza na JKT Tanzania saa 1 usiku Azam Complex Chamazi.
Jumatatu Februari 26, 2018 kutachezwa mechi mbili Kiluvya United dhidi ya Tanzania Prisons saa 8 mchana Uwanja wa Mabatini na Stand United watawaalika Dodoma FC saa 10 jioni uwanja wa Kambarage.
No comments
Post a Comment