Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, August 28, 2017

Kardinali Pengo aikabidhi serikali mradi wa kisima

  Na Pascal Mwanache, Dodoma

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Dar es salaam limekabidhi mradi wa kisima kwa serikali, katika kituo cha mafunzo kwa watoto (mahabusu ya watoto) cha Upanga jijini Dar es salaam, huku serikali ikiazimia kujifunza kupitia jitihada za Kanisa katika kujenga jamii ya watanzania yenye maadili, upendo na kujali wengine.
Akikabidhi mradi huo kwa niaba ya watoto wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa Kanisa linajikita katika utoaji wa huduma za kijamii kuonyesha kuwa linaunga mkono jitihada za serikali katika kuandaa taifa adilifu linaloongozwa na upendo bila kujali tofauti za uchumi, siasa au dini, kwa manufaa ya watanzania wote.
“Watoto ndiyo tumaini la kila taifa. Kadiri tunavyokuwa na watoto wenye maadili, wale wanaojua kipi kifanywe ili kujenga taifa, tunaweza kuwa na matumaini kwa taifa la kesho. Kuonyesha kwamba Kanisa hatuko mbali na serikali yetu katika kujenga yale yanayokua ya manufaa kwa taifa letu ndiyo maana tunafanya haya yote. Sisi tuna sehemu yetu, kimacho au kimwili inaweza kuonekana ni sehemu ndogo kulinganisha na kinachofanywa na serikali. Lakini kidogo kile tunachoweza kuchangia, daima tunakichukulia kama ishara ya nje ya hali iliyokuwa kubwa zaidi kutoka moyoni” amesema.
Aidha ameongeza kuwa lugha pekee inayozungumzwa na Kanisa ni upendo, ndiyo maana wanapotoa huduma mbalimbali za kijamii hawaulizi dini ya mtu, bali wanasaidia  wote kwa pamoja, ili kuwafunza umuhimu wa kuwa wamoja.
Akipokea mradi huo uliogharimu Milioni 11, 780, 000/=, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali itaendelea kuthamini na kujifunza kupitia jitihada zinazofanywa na Kanisa Katoliki katika kujenga jamii ya watanzania yenye maadili, upendo, na kujali watu wengine.
“Napenda kutoa shukrani zangu kwa niaba ya serikali kwako wewe Baba Mwadhama kwa kufikiria kutuwezesha kupata huduma hii muhimu kwa watoto. Tumesikia kuwa unakuwa unawaelekeza watoto, walezi wao na wazazi kufanya matendo mema. Mimi ni mtu wa imani tofauti ila nataka kukiri kwamba Kanisa Katoliki linatusaidia sana katika kujenga jamii ya watanzania yenye maadili yenye upendo, yenye kujali watu wengine” ameeleza.
Pia ameliomba Kanisa liendelee kushirikiana na serikali katika kuwasisitiza watanzania hasa wazazi na walezi, watimize wajibu wa malezi kwa watoto wao. Amesema kuwa malezi bora kwa watoto yatasaidia kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa watoto, kwani wanaofanya vitendo hivyo ni watu wa karibu na watoto, ambao wanapaswa kuwa walinzi.
“Tutaendelea kutambua mchango mkubwa wa Kanisa katika kutatua changamoto na kero zinazowakabili watanzania. Kila mwezi tulikuwa tunatumia takribani shilingi laki nne kwa ajili ya kulipia bili za maji. Maana yake kukamilika kwa mradi huu tutaweza kuokoa shilingi laki nne kila mwezi, na kwa mwaka ni takribani ni shilingi milioni 4 na laki 8, tunawashukuru sana” ameeleza.
Aidha Waziri Mwalimu amewathibitishia watoto walio katika kituo hicho uhakika wa matibabu yao kwa mwaka mzima, kwa kuwapatia bima ya afya inaitwa toto afya card.

Ushauri wa Padri Nyasulu waitea taswira mpya kwa Taifa
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Padri Timothy Nyasulu ameomba kuangalia uwezekano wa kuacha kutumia jina ‘mahabusu’, kwa kuwa maana hiyo ina mwelekeo wa unyanyapaa, ushauri ulioungwa mkono na Kardinali Pengo na Waziri Ummy Mwalimu, ambaye ametoa agizo kwa Taasisi ya Kiswahili nchini kutafuta neno linalofaa.
“Nakubaliana na Padri Timothy kwamba kuita mahabusu inaweza ikawa kama tunazidi kuwanyanyapaa watoto. Kwa jina la kiingereza tunaita retention home. Kwa kiingereza haileti ukakasi, kwamba ni sehemu ambayo tunawazuia watoto ambao wapo katika mkinzano na sheria, kwa hiyo tutawaomba wenzetu wa taasisi ya Kiswahili Tanzania watutafutie jina zuri la Kiswahili”

Chimbuko la kukabidhi mradi huo
Mnamo Desemba 3, 2016 Askofu Msaidi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa akiambatana na watoto wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu wa Parokia ya Kurasini, walitembelea kituo cha mafunzo cha watoto Upanga na kukabidhi zawadi mbalimbali zilizotokana na michango ya watoto hao.
Hapo ndipo Afisa Mfawidhi wa Mahabusu hiyo ndugu Ramadhan Yahaya alipotaja kero inayohitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka kuwa ni kero ya maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
“Tangu nimekuja kituo hiki miaka mitatu iliyopita, kituo kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji. Tunadaiwa bili kubwa zaidi ya shilingi milioni 5, hadi kupelekea kukatiwa huduma ya maji” alieleza ndugu Yahaya.

Baada ya kusikiliza kero hizo, Askofu Nzigilwa mara moja aliagiza kufanyika kwa tathmini na upembuzi yakinifu ili kuona uwezekano wa kuchimba kisima kwa ajili ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji. Na Agosti 21, 2017 zoezi la kukabidhi mradi wa kisima hicho kwa serikali likakamilika, ikiwa ni mwendelezo wa utoaji huduma kwa jamii, unaofanywa na Kanisa Katoliki nchini kwa zaidi ya miaka 150 sasa.

TEC BLOG
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment