Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, July 31, 2017

Tanzania kuanza huduma ya kupandikiza Figo Mwezi Septemba

Kitengo cha huduma za upandikizwaji na usafirishwaji wa figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kinatarajiwa kuanza kutoa huduma Septemba mwaka huu, baada ya ujenzi wa miundombinu yake kukamilika kwa asilimia 97.

Huduma hiyo inatarajiwa kuanza kutolewa baada ya mwaka jana MNH kupatiwa mkopo wa Sh3.7 bilioni kutoka NHIF kwa ajili ya kutengeneza vyumba vya upasuaji na kununua vifaa kwa ajili ya upasuaji wa figo lakini pia kufanya ukarabati wa hospitali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi , Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Aminiel Aligaesha amesema huduma hiyo inakuja nchini ikiwa ni moja kati ya mikakati ya Serikali kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi.

Amesema kitengo hicho ambacho kilitakiwa kuanza kutoa huduma Juni mwaka huu, hivi sasa kimekalimika kwa asilimia 97.

Amesema kwa sasa MNH ipo katika matayarisho ya mwisho kwa kuweka maandalizi ya miundombinu stahiki kwa ajili ya matibabu ya huduma ya figo kwani inajumuisha mambo mengi.

“Tunahitaji kuwa na vyumba maalum kwa upasuaji wa figo pekee, ICU na vyumba vingine ambavyo vinahitajika kwa ajili ya huduma hiyo,” amesema Aligaesha.

Alisema miundombinu hiyo imekamilika kwa asilimia kubwa na kilichobaki ni kufungwa baadhi ya vitu ili huduma ya upandikizaji ianze.

Aligaesha alifafanua kuwa upande wa ICU wamekamilisha ujenzi wake kwa asilimia 95 na kilichobaki ni kufunga baadhi ya mashine na vifaa muhimu.

Alisema tayari upande wa mafunzo kwa madaktari watakaotoa huduma hiyo yamekamilika kwa asilimia 100, kinachosubiriwa ni miundombinu na vitendanishi.

“Kwa asilimia 80 manunuzi ya vitendanishi, dawa, mashine ndogo zinazohitajika vimekamilika na mchakato uliopo ni namna ya kuviwasilisha,” alisema na kuongeza:

“Vitu hivi ambavyo tunatarajia vitatumika katika huduma hii ya upandikizaji figo ni vya kuweka oda na inachukua muda mrefu kidogo kufikishwa, tunafikiri mambo yakienda vizuri mwanzoni mwa Septemba tutaanza kutoa huduma ya upandikizaji figo.”

Kitaokoa mabilioni ya fedha

Kitengo hicho kinatarajiwa kuokoa zaidi ya Sh12.4 bilioni ambazo Serikali imezitumia kwa kipindi cha miaka mitatu kusafirisha wagonjwa wa figo 160 nje ya nchi kwa matibabu.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa MNH, Dk Jacqueline Shoo, alisema utaratibu wa kusafirisha wagonjwa nje ya nchi umekuwa ukifanyika kwa kuratibiwa na Wizara ya Afya, huku ukiigharimu Serikali Dola 15,000 (Sh33 milioni) mpaka 35,000 (Sh77 milioni).

Mkurugenzi wa MNH, Lawrence Museru alisema huduma ya upandikizaji figo ni mwendelezo wa jitihada za hospitali kuhakikisha huduma hizo sasa zinaanza kupatikana nchini baada ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Upasuaji wa Mifupa (MOI) kufanikiwa kwa asilimia 100.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja amesema kuwa magonjwa ya figo yameonekana kuwakumba zaidi watu wazima kwani kwa miaka mitatu mfululizo, hakuna mtoto aliyekwenda nje ya nchi kwa matibabu ya figo.

Amesema kuanzia Julai 2013 mpaka Juni 2016, Watanzania 160 walikwenda India kupandikizwa figo, wakiambatana na ndugu zao 160 waliokwenda kuwatolea figo hizo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment