Msanii wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto ameteuliwa kuwa balozi wa hifadhi ya wanyama ya Ngorongoro kwaajili ya kuwahamasisha watanzania kutembelea kivutio hicho na kujionea ufahari wake.
Mshairi huyo ameteuliwa na Wizara ya Utalii baada ya kuonyesha jitihada mbalimbali anazozifanya katika hatua ya kuitangaza nchi ya Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Akiongea na mwandishi wetu Jumamosi hii akiwa katika viwanja vya Sabasaba ndani ya banda la Ngorongoro, Kaimu Mhifadhi wa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Samson Mtunga amesema wameona Mrisho Mpoto ni mtu sahihi ambaye ataweza kuitangaza nchini katika mambo ya kitalii.
“Tumemteua Mrisho Mpoto kuwa balozi wetu wa utalii, tumeona ni mtu ambaye anaweza kufanya kazi hiyo vizuri kwa sababu tayari kuna baadhi ya juhudi zake binafsi tumekuwa tukiziona katika shughuli zake mbalimbali. Kwahiyo kama mnavyojua wizara ina bidhaa nyingi Mpoto anaanza na Ngorongoro lakini baadaye anaweza kuongezewa majukumu kwa sababu tuna vitu vingi sana tunahitaji vitangazwe,” alisema Samson Mtunga.
Kwa upande wa Mpoto amesema ataitumia nafasi hiyo kuwahamasicha Watanzania juu ya ufahari wa hifadhi hiyo pamoja na kuvitangaza vitu pekee vinavyopatikana.
“Kazi iliyopo mbele yangu kwa sasa ni kuhakikisha Watanzania wanatembelea vivutio vyetu, tukiizungumzia Ngorongoro ni hifadhi ambayo ndani yake pia kuna binadamu wanaishi, kuna wanyama wengi. Kwahiyo huu ndio wakati ya kuthamini vya nyumbani na kuvitumia ipasavyo. Kwa mfano umechukua likizo ya mwezi mmoja tembelea kule ukiwa na familia yako ukaone mambo mazuri ambayo huwenda hayapatikani duniani kote,” alisema Mpoto.Mpoto amewataka Watanzania ambao wanatembelea maonyesho ya Sabasaba wasiache kutembelea banda hilo ili kujifunza mambo mbalimbali kuhusu hifadhi ya Ngorongoro.
“Kwa sasa hivi nipo kwenye banda la Ngorongoro kwahiyo ukifika hapa tunaweza kuongea mengi kuhusu hifadhi hii ili na wewe ukirudi nyumbani ukawaeleze wengine kwamba Ngorongoro sio sehemu ya mchezo mchezo,”
Alisema Watanzania wakitembelea hifadhi hiyo kwa wingi kwanza watafurahia upekee wa hifadhi hiyo pia wataweza kuchangia kuongeza pato la taifa hela ambazo zinaenda kutatua kero mbalimbali za watanzania iliwemo maji, barabara na huduma ya afya.
No comments
Post a Comment