WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi za nje hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika mipaka yote na kuonya tabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za Afrika Kusini, Malawi na Zambia.
Waziri Mkuu ametoa karipio hilo alipozungumza na watumishi wa kituo cha forodha cha Kasumulu kilicho katika mpaka wa Tanzania na Malawi wilayani Kyela na kusema ili kuhakikisha jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi wa watu wanaopita kwenye maeneo hayo pamoja na mizigo ukaimarishwa.
Amewataka Maofisa wa Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani kuhakikisha wanadhibiti uingiaji holela wa raia wa kigeni kwa lengo la kuimarisha ulinzi nchini ambapo imebainika katika baadhi ya maeneo kumeanza kuonekana silaha ambazo hapo awali hazikuwepo na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika matukio ya kihalifu.
Waziri Mkuu pia amewataka viongozi hao kuhakikisha biashara zote za magendo zinazofanyika mipakani, zikiwemo za kubadilisha fedha zinadhibitiwa kwa kuwa zinaikosesha Serikali mapato na kwamba ni vema yakawepo maduka ya kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili kudhibiti biashara hiyo ambayo kwa sasa inafanywa kimagendo huku Serikali ikikosa kodi.
Awali, Bw. Taniel Magwaza ambaye ni Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi katika kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo na kufafanua kuwa katika doria zilizofanywa mwaka 2016/2017 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
No comments
Post a Comment