SHIRIKISHO la Soka duniani (Fifa), limebariki mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF), uendelee kama ulivyopangwa, imefahamika.
Taarifa kutoka katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF na ujumbe huo wa Fifa kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam kilielezwa msingi mkubwa ni kuheshimu katiba ya shirikisho hilo.
Chanzo chetu kilieleza kuwa sekretarieti ya TFF imetakiwa kuendelea na maandalizi ya uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mkoani Dodoma.
"Uchaguzi uko pale pale na maandalizi yake yanaendelea kama kawaida, wajumbe wataelezwa hili na mambo mengine muhimu yaliyojadiliwa kwa kirefu," kilisema chanzo chetu.
Taarifa nyingine kutoka katika kikao hicho ilieleza kuwa wafanyakazi wa TFF ambao wameajiriwa kwa mikataba hatima yao imekalia kuti kavu kutokana na sababu mbalimbali za utendaji ambazo zimebainika.
Pia, kikao hicho kimeamua kuwa mkoa wa Songwe hautashiriki katika mkutano mkuu huo kutokana na kutotimiza taratibu za kuwa mwanachama wa TFF tangu mkoa huo ulianzishwa rasmi.
"Kuna watu wamekalia kuti kavu pale TFF, nani atatoka na nani ataingia inaweza kujulikana kabla au baada ya uchaguzi," alisema mjumbe mwingine wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo.
Wakati huo huo wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo wa TFF wamekuwa wakiendelea kufanya kampeni za hapa na pale kuomba kura ili wachaguliwe na hatimaye kuliongoza shirikisho hilo kwa muda wa miaka minne ijayo.
TFF inafanya uchaguzi mkuu baada ya viongozi waliokuwapo madarakani sasa ambao walichaguliwa mwaka 2013 kumaliza muda wao kwa mujibu wa katiba.
No comments
Post a Comment