Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekana kuwa na mwaliko wa kuhudhuria kongamano la kujadili dhana ya demokrasia na vyama vya upinzani litakalofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Ilala, linatarajia kuwashirikisha watu mbalimbali maarufu wakiwamo wanasiasa na viongozi wakuu wa vyama vya siasa.
Mratibu wa kongamano hilo, Makongoro Mahanga alisema jana kuwa wamemwalika Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ambao chama chao kimekana kupokea mwaliko huo.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alisema hakuwa na taarifa za kongamano hilo na kwamba yupo mkoani Dodoma kwa sasa.
‘Nani anaongoza hilo kongamano? Mbona mimi sina taarifa. Linahusu nini ?” alihoji Mangula.
Hata Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Rodrick Mpogolo alipoulizwa alisema hana taarifa kama viongozi wa chama hicho wamealikwa kwa sababu naye yuko safarini.
“Siwezi kufahamu kama tumealikwa kwa sababu niko safarini,” alisema. Hata hivyo, simu ya Polepole iliita bila kupokewa na Kinana hakupatikana kabisa alipotafutwa.
Awali, Mahanga alisema watu wengine maarufu walioalikwa kwenye kongamano hilo ni Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad, mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
No comments
Post a Comment