Writen by
sadataley
2:23 PM
-
0
Comments
KASEJA MCHEZAJI BORA WA JANUARI LIGI KUU YA VODACOM
Golikipa wa timu ya Kagera
Sugar, Juma Kaseja Juma amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya
Vodacom wa mwezi Januari kwa msimu wa 2016/2017.
Kaseja aliwashinda wachezaji Mbaraka Abeid pia wa Kagera Sugar na Jamal S. Mtengeta wa Toto African.
Katika mechi tatu ambazo timu ya
Kagera ilicheza kwa mwezi huo, Kaseja ambaye alicheza kwa dakika zote
270 alikuwa kiongozi na mhimili wa timu na aliisaidia timu yake kupata
ushindi katika michezo yote ambapo ilikusanya jumla ya pointi 9
zilizoifanya timu hiyo kupanda nafasi mbili katika msimamo wa ligi kwa
mwezi huo wa Januari (kutoka nafasi ya 5 hadi ya 3).
Katika michezo hiyo mitatu,
Kagera Sugar ilifunga mabao sita na Kaseja alifungwa bao moja tu na
alionesha nidhamu ya hali ya juu ikiwemo kutopata onyo lolote (kadi).
Kwa kushinda tuzo hiyo, Kaseja
atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini
wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.
NAPE KUZINDUA MFUKO WA KUSAIDIA SERENGETI BOYS
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye (Mb) kesho Februari 23, 2017
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Mfuko wa Maendeleo ya
Mpira wa miguu kwa vijana na wanawake.
Uzinduzi huo utakaofanyika saa
5.00 asubuhi, utahudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Mkurugenzi wa Michezo, Yussuph Singo.
Utafanyika kwenye Ukumbi wa
Hoteli ya Courtyard, Upanga jijini Dar es Salaam.
Mfuko huo uko chini ya Mwenyekiti
Bw. Tido Mhando ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Azam Media wakati
Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo ni Bw. Dereck Murusuri.
Wajumbe wake ni Bi. Beatrice
Singano, Bw. Ephraim Mafuru, Bw. Tarimba Abbas, Bw. Joseph Kahama, Bw.
Salum Rupia na Bw. Meshack Bandawe.
Majukumu ya Kamati ya Mfuko huo
ni kukusanya rasilimali kwa ajili ya kuendeshea program za TFF za
maendeleo ya mpira wa vijana wa wanawake.
Kwa mujibu wa Katiba ya TFF,
mfuko huu ni huru, una sekretariet yake, akaunti yake benki na ofisi
zake zinazotarajiwa kuwa Mikocheni, Dar es Salaam.
MALINZI AZIPONGEZA SINGIDA UNITED, NJOMBE MJI
Mara baada ya wiki iliyopita
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuipongeza timu ya Lipuli ya
Iringa, leo Jumanne Februari 21, mwaka huu kwa mara nyingine, Rais wa
TFF Jamal Malinzi amezipongeza kwa mpigo, timu za Singida United ya
Singida na Njombe Mji ya Njombe kwa kupanda daraja.
Juma lililopita, Rais Malinzi
aliuandikia barua uongozi wa Lipuli ya Iringa kwa mafanikio ya kupanda
daraja msimu huu kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/18 kama alivyofanya sasa kwa Singida
United ya Singida na Njombe Mji ya Njombe.
Katika salamu hizo kwa Lipuli
ambayo imepanda daraja baada ya kusota miaka 17 iliposhuka daraja, Rais
Malinzi alimwandikia barua Katibu Mkuu wa timu hiyo akisema: “Nitumie
fursa hii kukupongeza wewe, uongozi wa klabu yako, benchi la ufundi na
wadau wote wa timu ya Lipuli kufuatia kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.
Kama ilivyotokea kwa Lipuli, Rais
Malinzi pia kwa moyo mkunjufu amewaandikia barua, viongozi wa Singida
United ya Singida na Njombe Mji ya Njombe, akisema: “Pia nanyi
nawapongeza kwa kupanda daraja. Bila shaka ni kazi kubwa imefanyika
ikihusisha kujitolea kwa ari na mali kuhakikisha mnafika hapa mlipo.”
Pamoja na salamu hizo za
kuwapongeza, Rais Malinzi hakuacha kuziusia timu hizo akisema: “Rai
yangu kwenu ni kuongeza juhudi na kuendesha klabu kwa weledi mkubwa
zaidi ili muweze kuwa washindani wa kweli katika ligi (Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara).”
MKUTANO WA BARAZA KUU LA BODI YA LIGI FEBRUARI 26, 2017
Mkutano wa Tatu wa Baraza Kuu la
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) chini ya Mwenyekiti wake Bw. Hamad
Yahya Juma utafanyika Jumapili, Februari 26 mwaka huu jijini Dar es
Salaam.
Wajumbe wa Mkutano huo wa mwaka
2016 ambao utaanza saa 4 asubuhi ni wenyeviti wa klabu zote za Ligi Kuu
ya Vodacom, na klabu zote za Ligi Daraja la Kwanza.
Ajenda za Mkutano huo ambazo
zimeainishwa katika Ibara ya 21 ya Kanuni za Uendeshaji Bodi ya Ligi
Kuu ni Kuhakiki Akidi, Kufungua Mkutano, Kuthibitisha Ajenda,
Kuthibitisha Muhtasari wa Mkutano Uliopita, Yatokanayo na Mkutano
Uliopita, Hotuba ya Mwenyekiti, Taarifa ya Utendaji ya Kamati ya
Uongozi, Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa, Kupitisha Bajeti,
Mengineyo na Kufunga Mkutano.
No comments
Post a Comment