Writen by
sadataley
6:44 AM
-
0
Comments
Rais Jakaya Kikwete akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2014, Rachel Kassandra kwenye sherehe za Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge huo na Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere zilizofanyika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora jana. Picha na Freddy Maro wa Ikulu
Na Robert Kakwesi na Peter Elias, Mwananchi
Tabora/Dar. Wakati mbio za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 zikianza kushika kasi nchini, Rais Jakaya Kikwete amewataka vijana kumchagua mtu anayefanana na kijana kurithi nafasi yake.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja huku kukiwa na makada kadhaa ndani ya chama chake ambao wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo huku baadhi wakifungiwa kwa kuanza kampeni mapema na wengine wakiendelea na mikakati ya chinichini kabla ya kujitangaza.
Rais Kikwete alisema hayo jana mjini Tabora alipokuwa akihutubia wananchi waliohudhuria kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere zilizokwenda sambamba na kilele cha Wiki ya Vijana na hitimisho la Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Alisema vijana ndiyo chachu ya maendeleo ya Taifa lolote hivyo washiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura kumchagua rais anayefanana na kijana kama alivyokuwa yeye wakati akigombea urais 2005, wakati huo akiwa na umri wa miaka 55.
“Siyo kijana wa chini ya miaka 35, Katiba yetu hairuhusu, lakini mtu ambaye anaonekana kijana kama nilivyokuwa mimi wakati nagombea nafasi hiyo mwaka 2005,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliohudhuria uwanjani hapo.
Mgombea mwenye sifa zilizotajwa na Rais Kikwete anaweza kutoka nje au katika kundi la wanaCCM wanaotajwa au kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu.
Miongoni mwa wanaotajwa wamo makada sita waliopewa onyo kali na chama hicho kwa kuanza kampeni mapema wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa (61) na Frederick Sumaye (64) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (61).
Wamo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira (69), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (40) na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja (47).
Mbali na hao waliopewa onyo, wanaCCM wengine wanaotajwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (66), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (72), Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla (39), Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (39) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya (65).
Pia wamo Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi (43), Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (66) na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal (69).
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni kama ile iliyowahi kutolewa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa mwaka 2005, kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ambapo aliweka bayana kwamba wakati huo ulikuwa ni wa vijana kuongoza nchi kwa kuwa tafiti ndivyo zilivyokuwa zikionyesha.
Baada ya Rais Mkapa kutoa kauli hiyo, wakati huo Kikwete ndiye aliyepitishwa na CCM kugombea urais kwa kuwashinda wenzake 11 waliojitokeza ndani ya chama hicho kuwania uteuzi huo.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/JK-agusia-ujana-urais-2015/-/1597296/2486934/-/ry9u0wz/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/JK-agusia-ujana-urais-2015/-/1597296/2486934/-/ry9u0wz/-/index.html
No comments
Post a Comment