Writen by
sadataley
10:21 AM
-
0
Comments
Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Stephen Wasira amekiri kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo la maadili katika uongozi. Kuna haja ya kuweka sheria kali kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo.
Amesema kilio chake katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba ni kupata itakayowabana watu wanaovunja maadili kwa masilahi yao binafsi.Wasira alitoa kauli hiyo alipozungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu mjini Dodoma.
Wasira ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Namba sita ya Bunge la Katiba, alibainisha kuwa ndani ya rasimu iliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kuna mambo mengi ambayo yalipaswa kufanyiwa marekebisho.
“Kuna tatizo kubwa ndani ya nchi yetu linalohusiana na miko ya viongozi pamoja na maadili ambayo kwa njia nyingine yanaonekana kuporomoka sana, lakini suala la rushwa pia ni tatizo kubwa,” alisema.
Alisema kwa hali ilivyo, hakuna namna nyingine ya kuweka mambo vizuri kama siyo kuyaingiza katika Katiba inayoendelea kutungwa ili yatungiwe sheria kali zitakazowabana watu wanaovunja maadili kwa masilahi yao binafsi.
Wasira alitaja baadhi ya maeneo ambayo maadili yameporomoka kuwa ni kwa viongozi wa umma ambao wakati wote wakiingia madarakani wanafikiria wataiba kiasi gani cha fedha badala ya kuwaza uwajibikaji na uzalishaji.
“Katika maeneo mengi rushwa imetawala na hata hili suala la ununuzi, hebu angalia glasi ndogo kama hii (anaonyesha) ukienda sokoni inauzwa Sh 1,000, lakini kwa bei ya zabuni wataiuza Sh 5,000, huu ni wizi mkubwa,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi, alisema mambo kama hayo yanamkosesha usingizi kwa muda mrefu, lakini sasa ni nafasi yake na Watanzania wengine kutumia mchakato wa Katiba ili kuyaingiza ili mwisho wa siku yatungiwe sheria.
Kuhusu matumaini yake ya kupata Katiba Mpya kupitia mchakato unaoendelea sasa anasema, “Sina wasiwasi kwa kuwa Katiba nzuri itapatikana kupitia mkutano na Watanzania wataikubali.”
Katika hatua nyingine, Wasira amekanusha madai kuwa ni mtu wa kupinga rasimu kutokana na ugomvi wa kisiasa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Badala yake alibainisha kuwa mambo mengi ya Tume hiyo ni mazuri na yamepita kama yalivyo. Lakini ugomvi wetu na Warioba ulishakwisha, alisema.
“Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati Namba sita, tumepitisha mambo mengi yaliyokuwa ndani ya rasimu hiyo na hatukufanya mabadiliko ya aina yoyote kutokana na uzuri wake na baadhi ndiyo tumeboresha na kuyapa meno zaidi,” alisema.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hakubaliani na muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa kwenye Rasimu hiyo kwa kile alichoeleza kuwa baadhi ya mambo ambayo kamati yake na Bunge vimeyapinga hayako sawa. Ila nakubaliana moja kwa moja na mapendekezo ya Rais wa Zanzibar awe Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kuhusu suala la wapinzani kudai Bunge hilo linatumia fedha nyingi katika kutengeneza kitu ambacho hakitakuwapo, alisema hizo ni ndoto, kwani wanachokisema hakina msingi. “Wewe fikiria Bunge la kwanza ambalo lilikuwa la siku 67, wale jamaa walikaa siku 60 lakini fedha walilipwa zote na hawakurudisha. Leo wanaposema sisi tunatumia fedha nyingi nani awe wa kwanza kulaumiwa kama si wao. “Tukisema tusitishe Bunge sasa ndiyo itakuwa matumizi mabaya zaidi ya fedha, kwani Rais ajaye atatakiwa aje aanze upya. Badala ya kuishia katika Katiba inayopendekezwa ili aanzie kwenye kura ya maoni, wao wanataka fedha hizi ziende bure, nadhani hawana hoja hapo.
No comments
Post a Comment