Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, September 19, 2014

Serikali yakwaa kisiki kuizuia TLS mahakamani


 
Na James Magai, Mwananchi
Dar es Salaam. Serikali jana ilijikuta ikikwaa kisiki mahakamani baada ya kushindwa kuzuia usikilizwaji wa maombi ya Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ya kutaka ipatiwe kibali cha kufungua kesi kupinga Bunge la Katiba.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitupilia mbali pingamizi hilo la awali lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya maombi hayo.

TLS ilifungua maombi hayo kwa lengo la kutaka kibali cha mahakama ili iweze kufungua kesi kupinga mwenendo wa Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa maombi hayo, TLS inaiomba mahakama itamke kuwa mwenendo wa bunge hilo ni batili.
Pia, inaiomba itoe tafsiri ya mamlaka ya bunge hilo kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba 8 ya mwaka 2011 na namba 2 ya mwaka 2012 Sura ya 83.

Maombi mengine katika kesi hiyo yatakuwa ni mahakama kumwamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wawasilishe bungeni muswaada wa marekebisho ya sheria hiyo na amri ya zuio lavikao vya Bunge la Katiba.
Kufuatia maombi hayo, AG aliwasilisha pingamizi akiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo.

Katika pingamizi hilo, AG kupitia jopo la mawakili wa Serikali walioongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alidai kuwa maombi ya TLS mbele ya mahakama hiyo hayana mashiko kisheria kwa kuwa yamewasilishwa wakati hakuna hukumu, uamuzi, amri wala mwenendo unaopaswa kuhojiwa.

Hoja nyingine ilidai kuwa maombi hayo yanayotafutwa na waombaji hayana maana na ni ya kuudhi na kwamba, hayawezi kuthibitika kisheria kwa kuwa hakuna uamuzi wa kibali cha kufungua maombi hayo.
Hata hivyo, Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za AG na majibu ya watoa maombi, ilitupilia mbali hoja zote za AG na kuamua kuendelea kusikiliza maombi hayo leo.

Uamuzi huo uliandikwa na kusomwa na Jaji Dk Fauz Twaib, kwa niaba ya jopo la majaji watatu wanaosikiliza maombi hayo ambao ni Augustine Mwarija (Mwenyekiti wa jopo) na Aloysius Mujulizi.

Katika uamuzi huo, Mahakama ilisema hoja za AG hazikidhi kuwa za pingamizi la kisheria kiasi cha kuifanya hati ya kiapo cha mtoa maombi kuwa na dosari za kisheria.

Hata hivyo, alikubaliana na hoja za Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata katika aya moja tu ya kiapo hicho kuwa ina dosari kwa kuwa inazungumzia hoja ambazo hazikupaswa kuwamo, na kukubaliana na hoja ya TLS.
Kuhusu hoja nyingine za pingamizi hilo, Mahakama ilisema katika hatua iliyofikiwa si wakati muafaka wa kuyasikiliza kwakuwa maombi hayo yanahitaji uthibitisho wa ushahidi.

Wakati huohuo; Mahakama hiyo jana ilishindwa kukamilisha usikilizwaji wa kesi ya kupinga Bunge la Katiba iliyofunguliwa na mwandishi wa habari, Saed Kubenea ambayo sasa itasikilizwa leo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment