Writen by
sadataley
7:01 PM
-
0
Comments
Na Exuper Kachenje, Mwananchi
Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ametoa dira ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kutaja sifa za rais anayefaa kuiongoza Tanzania.
Warioba alisema kwamba taifa la Tanzania
linastahili kuongozwa na vijana wenye nguvu ya mwili na akili. “Mimi
nafikiri tuangalie kati ya vijana tulionao, nani anatufaa kuiongoza
nchi, tusirudi kuangalia wazee,” alisema Jaji Warioba.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya
mwandishi wa habari hizi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika wiki hii
ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja huku ukiwa
umesalia takribani mwaka mmoja na miezi minne, kabla ya taifa kuingia
kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
utakaoshirikisha vyama zaidi ya 23 vyenye usajili wa kudumu nchini.
Uchaguzi huo mkuu ambao ni wa tano wa vyama vingi
nchini, unatarajiwa kulipatia taifa rais mpya, baada ya Rais Jakaya
Kikwete kumaliza muda wake wa utawala wa awamu ya nne.
Mbali na wagombea wa vyama vya upinzani, ndani ya
CCM pekee kunatajwa kuwa na makundi zaidi ya manne yanayotarajia kuwania
urais mwaka ujao.
Makundi hayo ni pamoja na linalotajwa kumuunga
mkono Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, kundi lingine linatajwa kuwa
nyuma ya Samuel Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki pamoja na linalomuunga mkono Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera
na Uratibu, Stephen Wassira anatajwa kuwania nafasi hiyo ya juu ya
uongozi nchini.
Hata hivyo, viongozi hao wamekuwapo madarakani
katika nyadhifa na nyakati tofauti huku pia wakiwa na umri uliovuka
ujana, unaopendekezwa na Jaji Warioba.
Ndani ya CCM vijana wanaotajwa kutaka kuwania
urais mwakani ni pamoja na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini,
William Ngeleja na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January
Makamba.
Makamba tayari ametangaza nia yake ya kuwania
urais akisema huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola, licha
ya chama hicho kuzuia kutangaza nia na kupiga kampeni kabla ya muda.
Makamba, mmoja wa makada wa CCM walioonywa na
chama hicho baada ya kutuhumiwa kuanza kampeni mapema, alijipigia debe
kuwa iwapo atapitishwa na chama hicho, ataelekeza nguvu kwenye
vipaumbele vinne ambavyo ni ajira, huduma za jamii, uchumi imara na
utawala bora. Akizungumzia uzoefu Makamba alisema hakuna ushahidi wowote
kwamba miaka mingi kwenye siasa ndiyo inatengeneza kiongozi mzuri.
“Uongozi mzuri unatengenezwa na haiba, wajihi,
dhamira, uwezo, maadili, uhodari, hekima na maarifa. Sifa hizi
hazipatikani kutokana na uzoefu wa miaka mingi kwenye siasa hata baadhi
ya vijana wanazo,” alisema Makamba.
Alitolea mifano mingi duniani ambapo vijana ambao hawakuwa na uzoefu kabisa katika nafasi za siasa wameshinda na kubadilisha nchi kama Tony Blair wakati anakuwa Waziri Mkuu wa Uingereza aliongoza nchi hiyo kubwa wakati alikuwa hajawahi kuwa hata Naibu Waziri.
Alitolea mifano mingi duniani ambapo vijana ambao hawakuwa na uzoefu kabisa katika nafasi za siasa wameshinda na kubadilisha nchi kama Tony Blair wakati anakuwa Waziri Mkuu wa Uingereza aliongoza nchi hiyo kubwa wakati alikuwa hajawahi kuwa hata Naibu Waziri.
“Barack Obama (Rais wa Marekani) alikuwa Seneta
miaka mitatu tu, Julius Nyerere alikuwa Mwalimu akaingia siasa akaja
kupewa uongozi wa nchi akiwa na miaka 39 tu.”
Hata hivyo, Februari mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM
iliwapa onyo kali makada wake sita akiwamo January Makamba ikiwatuhumu
kupiga kampeni za urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao kabla ya muda.
Katika maelezo yake Jaji Warioba alisema kwamba tangu uhuru, walioshika madaraka ya kuliongoza taifa walikuwa ni vijana.
Wazee kugombea urais
Akijibu swali kama atakuwa tayari wananchi
wakimtaka kuwania urais baada ya kazi kubwa ya kukamilisha Rasimu ya
Katiba nchini, Jaji Warioba alisema:
“Hili nilikwishalijibu, tusahau mawazo kwamba sisi
(wazee) tutarudi madarakani. Nadhani mara ya mwisho tulipozungumza
niliwaambia inafika wakati kiongozi unang’atuka. Unawaachia vijana ambao
wana nguvu ya kimwili na akili ndiyo watumikie taifa hili, waongoze
nchi.
“Na mimi nashangaa kwa nini, kwa kweli nashangaa
kabisa kutajwatajwa huku, wazee kama mimi na Salim (Dk Salim Ahmed
Salim). Nini kimetokea katika nchi hii hata sisi tufikiriwe?” alihoji
Jaji Warioba.
Alisema kuwa tangu uhuru hadi sasa Tanzania imetayarisha vijana wengi wanaofaa kuliongoza taifa na kuongeza:
“Hatuna ombwe la uongozi, tunao vijana wengi sana, tena kwa bahati nzuri nchi kwa kiwango kikubwa ilikuwa ikiongozwa na vijana.”
Huku akitaja mifano ya viongozi hao vijana
walioongoza taifa, Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alisema:
“Tulipoanza Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa
nchi hii, alikuwa kijana. Alikuwa hajafika hata miaka 40, hata wenzake
walikuwa vijana. Vijana ambao hawakuwa na uzoefu wa kuendesha Serikali,
waliichukua nchi.”
Mwanasheria huyo mkongwe aliyelitumikia taifa katika nyadhifa
mbalimbali alieleza kuwa hata waliofuata katika kulitumikia taifa
walikuwa vijana.
“…Waliofuata, walioshika nafasi za kuitumikia nchi
hii tuliwaona, walikuwa vijana. Edward Sokoine (aliyekuwa Waziri Mkuu),
aliingia akiwa bado kijana, akastaafu bado kijana, bahati mbaya
akafariki akiwa pia bado kijana. Dk Salim aliingia na miaka 42, mimi
nilikuwa na 45, Sumaye aliingia bado akiwa kijana,” alisema Jaji mstaafu
Warioba huku akihoji tena: “Hivi kimetokea nini sasa tunaanza kuangalia
wazee…, nini kimetokea nchi hii tuanze kufikiria wazee?”
Jaji Warioba alipoulizwa kati ya vijana walio kwenye uongozi, yupi atafaa kuongoza taifa alisema:
“Sitaki, sitaki majina, … ni sifa. Sifa zipo, hebu
mchukue alizotaja Mwalimu Nyerere mwaka 1995. Tunataka kiongozi mwenye
maadili, mwenye ‘commitment’ (kuwajibika),ambaye atasimamia, ataapa
kuisimamia Katiba.”
Makundi ya urais
Warioba pia aliulizwa iwapo makundi yanayotajwa
kusaka urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 kuwa huenda yanahusika
na kusuasua kwa Mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema kwamba, yeye na wenzake waliokuwa wajumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walikutana jijini Dar es Salaam kwa siku
tatu na kutafakari mchakato huo unavyokwenda ukihusisha maeneo na
makundi mbalimbali.
“Tulikwenda kutafakari, hatutaki kwenda kwenye
matukio, wala kuzungumzia makundi, nasema wote wakae pamoja waone
masilahi ya taifa, kwa sababu wasipokaa pamoja kuna hatari ya mchakato
huu wa Katiba Mpya kukwama. Na kukwama siyo kwa masilahi ya
taifa,”alisema.
Ikiwa Rasimu ya Katiba Mpya itapitishwa na
mapendekezo yake ya kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu, kutalazimika
kuwapo kwa Rais wa Tanganyika, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, hivyo nguvu na mfumo wa kisiasa kubadilika.
No comments
Post a Comment