Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, July 15, 2014

Ridhiwani aitamani nafasi ya Kinana CCM


Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete 
Na Mwandishi Wetu, MwananchiDar es Salaam. Matamanio ya wanasiasa wengi kwa sasa yako kwenye urais, lakini hali ni tofauti kwa mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ambaye ameweka bayana kuwa nafasi ya juu kisiasa anayotamani ni kuwa katibu mkuu wa CCM.
Mtoto huyo wa Rais Jakaya Kikwete aliamua kuweka bayana ndoto yake ya sasa katika mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika mjini Dodoma.
Ridhiwani, ambaye ni mwanasheria, alisema anapenda nafasi ya chama na ndiyo maana hata katika ‘posti’ zake katika ukurasa wa facebook amekuwa akiandika kikada zaidi.
“Kwangu mimi ngoja niseme ukweli, napenda sana nafasi ya chama kwa maana napenda sana chama na kuna siku nilikuwa nafanya mahojiano na Star Tv na niliwahi kuwaambia kwamba mapenzi yangu ni kuwa katibu mkuu wa chama,” alisema Ridhiwani alipoulizwa kama anafikiria kuwania urais.
“Yaani naamini nafasi ya katibu mkuu wa chama ni nafasi kubwa sana. Hizi siasa za urais ni matokeo tu,” aliongeza Ridhiwani ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Ridhiwani, ambaye aliingia bungeni mwezi Aprili baada ya kushinda kwenye uchaguzi mdogo, alisema iwapo wenzake wataona yeye anafaa hilo ni suala la mbele, lakini tamaa yake ni kushika nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa chama hicho tawala.
“Ukiwa katibu mkuu wa chama ndiyo nchi ya kwako hii, kwa sababu leo hii (katibu mkuu wa CCM, (Abdulrahman) Kinana anaweza kuwaambia wabunge wa CCM tokeni bungeni na wakatoka,” alisema mwenyekiti huyo wa zamani wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya Bagamoyo.
“Anaweza akatuambia tulale chini na tukalala. Yeye ndiyo tajiri wetu, lakini kubwa la msingi zaidi ni kwamba mimi napenda zaidi nafasi za chama. Hizi nafasi za serikalini ni nafasi za baadaye. Kama ikitokea kusaidia nchi tutasaidia, lakini hisia zangu zipo sana kwenye chama,” alisema.
Makundi ya kampeni
Alipoulizwa iwapo kuna kundi au mtu aliyemwomba amsaidie au awe katika kambi yake kusaka nafasi ya urais, Ridhiwani alijibu, “Nataka nikwambie ukweli kabisa. Hakuna mtu anayeweza kufanya hivyo, tena akiwapo basi atakuwa na moyo sana. Kwa sababu wanajua mimi matamanio yangu ni kumwona Rais yKikwete anamaliza uongozi wake vizuri.”
Alisema anaamini iwapo Rais Kikwete atamaliza vizuri na kuwaachia nchi yao vizuri, yeye (Ridhiwani) ataendelea kupata heshima katika nchi hii.
“Sasa leo hii nikijiingiza kwenye makundi ya siasa nitamvuruga mzee na nikifanya hivyo akashindwa kufanya kazi, tena tutarudi mwanzoni na akiondoka kesho watasema tumewavurugia nchi na akisemwa yeye nimesemwa mimi.”
Wanaowania urais kujitoa CCM
Ridhiwani pia alizungumzia tishio la watu kujiondoa ndani ya chama hicho iwapo hawatapitishwa kugombea urais, akisema hali hiyo ipo, lakini CCM imejiandaa na hakutakuwa na mpasuko kama inavyodhaniwa.
“Leo hii mtu anaposema mimi nisipochaguliwa najitoa, nitakigawa chama, nataka nikwambie CCM inajua hata mtu huyo akiondoka leo hii wanachama kumi nendeni, chama kitaendelea kama kawaida. Chama kimejiandaa kwa hali zote. Hakutakuwa na mpasuko ila kuna watu wataondoka kwa hasira zao ambao hao tunawatarajia,” alisema.
Hata hivyo, Ridhiwani alipoulizwa kama anayajua majina ya watu hao alijibu: “Hapana. Lakini kama kuna watu wanasema wasipochaguliwa watu wangu au mtu ninayemtaka sisi tutajiondoa CCM, maana yake asipochaguliwa mtu huyo ataondoka kweli. Kwa hiyo tunasema acha aondoke lakini chama kinajua kwamba likitokea hili kuna fulani atakasirika.”
Alisema ndiyo maana hata mwaka 1995 Rais Kikwete alipokuwa hajachaguliwa wako watu ambao walisema kwamba wataondoka, lakini kwa kuelewa kinachofanyika ni kitu gani, Kikwete aliamua kuwa hataondoka na watu wakasema nao hawaondoki.
Ampinga Pius Msekwa
Akitoa maoni yake kuhusu mchakato wa katiba na kauli ya Pius Msekwa kwamba hakuna haja ya katiba, Ridhiwani alisema: “Kwenye chama chochote kilicho hai kuna watu ambao hawataki kubadilika. Hata CCM tunalo tatizo hilo.
“Sasa Msekwa anatakiwa ajue kuwa hapa tulipo leo hii nchi yetu inapita miaka 50. Katika mfumo tulionao kuna vitu vya msingi huwezi kuvishughulikia kutokana na Katiba ya sasa. Hivyo ni lazima tukubaliane kupata Katiba Mpya ambayo inaweza kutupa mwanga mpya,” alisema na kuongeza: “Lazima ajue kuwa huhitaji ufike kwenye matatizo ili uanze kujitathmini.”
Kuhusu mvutano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar juu ya Muungano, alisema, “Mambo haya yanatakiwa kupatiwa majibu na majibu yake ni lazima watu wasema katika Katiba yao.”
Alisema kama suluhu ya hilo ni kuunda serikali tatu basi twende kwa serikali tatu au kama suluhu ni kuziunganisha nchi hizo ili tuwe na serikali moja basi twende kwa serikali moja basi iwe hivyo.
“Au kama mfumo tulionao unatosha lakini unatakiwa kufanyiwa marekebisho fulani basi twende kwa mfumo huu ambao unapendekezwa.
“Lakini kusema kwamba hatuhitaji Katiba Mpya, hilo jambo mimi sikubaliani nalo. Sikubaliani na Msekwa katika hilo. Lazima ajue mahitaji ya leo yanahitaji hilo.”
Kumiliki mali
Ridhiwani amekuwa akihusishwa na umiliki wa kampuni kubwa, majumba na mali nyingine ambazo watu wanahoji alizipataje katika umri wake wa miaka 35 akiwa amehitimu masomo si zaidi ya miaka mitano iliyopita.
Miongoni mwa mali ambazo inadaiwa ana hisa ni Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), kampuni ya mafuta, hoteli na malori.
“Nimekuwa nikihusishwa na mali hizo kwa sababu ni za marafiki zangu,” anasema Ridhiwani.
“Kuna marafiki zangu ambao nimewakuta wakiwa wana mali zao, lakini katika maisha kwa sababu wanaendelea kuhangaika, wanaendelea kupata mali pia. Hao nao wanadai kwamba Ridhiwani anashirikiana nao,” alisema.
“Mimi nataka kukwambia hayo yote unayoyasikia sijui ya Uda, sijui ya Lake Oil na nini, hao wote ni watu ninaofahamiana nao katika safari za maisha. Sina ushirika wowote nao wa kusema labda wana uhusiano wowote wa kibiashara na mimi. Ndani ya hizo kampuni zao mimi sina lolote.”
Alitoa mfano wa mwendeshaji wa Uda, Robert Kisena, akieleza kuwa alijuana naye mwaka 2003 na kwamba alimkuta Mwanza akiwa na kampuni yake ya Simon Group ambayo ilikuwa inasaga mbegu za pamba na kutoa mashudu.
“Nilimkuta akiwa na kiwanda cha pamba Malampaka. Nilimkuta anajenga kiwanda cha tumbaku Kaliua kule kwa Mzee (mbunge wa Urambo Magharibi, Juma) Kapuya. Kwa hiyo leo hii yeye anapojitanua kibiashara na kuwa mmiliki wa sehemu ya Uda, hilo jambo halihusiani na mimi. Ni yeye Kisena na harakati zake.
“Kwa sababu yeye anakopa, ananunua vitu, anauza vitu, kusafirisha na kuuza vitu. Sasa watu wanategemea akikutana na Ridhiwani ndiyo arudi chini, ni kitu ambacho hakiwezekani.”
Pia, alimzungumzia rafiki yake Saidi Mtanda, ambaye ni mbunge wa Mchinga akisema wakati akiwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wilaya ya Bagamoyo, alikuwa mhamasishaji wake.
“Amekuwa rafiki yangu tangu enzi hizo, amekuwa mbunge, mbona hajapewa hata unaibu waziri. Mbona watu hawazumgumzii hilo kwamba Ridhiwani amemnyima rafiki yake uwaziri. Wanachoangalia ni wale waliofanikiwa tu. Lazima wajue katika safari ya maisha kufanikiwa ni sehemu ya maisha na kutopata pia ni sehemu ya maisha.”
Mahojiano kamili ‘Swali na Jibu’ na Ridhiwani yatakuwa Ndani ya Habari kuanzia kesho
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment