Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, July 21, 2014

Msigwa ataka serikali ichunguze kampuni kubwa halali za uwindaji


Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mch. Peter Msigwa. Picha ya Maktaba 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameitaka Serikali kufanya uchunguzi hata kwa kampuni kubwa za uwindaji zenye leseni halali kwani yapo yanayokiuka sheria.
Msigwa pia amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wa Kampuni ya Green Miles Safari Ltd, GMS kwa madai kuwa wamekiuka masharti ya uwindaji.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mchungaji Msigwa alisema ana wasiwasi hata kampuni kubwa zenye vibali halali yanakiuka sheria za uwindaji.
Msigwa ndiye aliyeibua video ya Kampuni ya Uwindaji ya GMS na kulazimisha Waziri Nyalandu kuifutia kibali cha uwindaji,
Alisema haiwezekani kuwa kampuni za uwindaji za Tanzania au za kutoka nje ziko safi kwa asilimia 100 na haziendi kinyume cha leseni zao, na baada ya uchunguzi, zitakazobainika zifutiwe leseni na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Mimi niko tayari kusimamia na kuhakikisha wahusika wanafikishwa mahakamani, hii ni rasilimali ya Watanzania na tunatoa vibali kwa kazi maalumu,” alisema.
Akizungumza suala la Kampuni ya GMS, Msigwa alimtaka Waziri Nyalandu kutoishia kutangaza kuwafutia kibali cha uwindaji kampuni hiyo.
“Ninashangaa hadi leo hawajachukuliwa hatua, niliorodhesha makosa yao 11, lakini Waziri kaishia kuwafutia leseni, hiyo haitoshi, lazima wachukuliwe hatua,” alisema Msigwa.
Hata hivyo, uongozi wa GMS, umepinga hatua hiyo ya Nyalandu kuwafutia leseni, hivyo wameahidi kulifikisha suala hilo mahakamani.
Msigwa ambaye ni waziri kivuli wa maliasili na utalii, alisema GMS hawawezi kukwepa mkono wa sheria kwa kile walichokifanya na ataendelea kupambana kuhakikisha wanalinda maliasili za nchi kwa kushirikiana na Mtanzania mwenye uchungu bila kujali itikadi ya vyama.
Hata hivyo, pamoja na kusisitiza mkono wa sheria kwa GMS na kutaka kuungwa mkono, Msigwa alionyesha wasiwasi wa kuungwa mkono katika kampeni yake kwa kusema kuwa ni mtandao mkubwa ambao hauhofii hata kuondoa roho ya mtu anayewafuatilia.
Msigwa kwa upande mwingine, alikanusha tuhuma kwamba yeye pamoja na Waziri, Nyalandu na Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli wanatumika na wametengeneza ‘utatu mtakatifu’ kwa maslahi yao binafsi.
“Unajua watu wanasema hivyo, mimi siko kwa ajili ya kumbeba Nyalandu wala Lembeli na wanalifahamu hilo, mimi naangalia ulinzi wa maliasili.
“Hata nikipewa safari za nje, si ‘favour’ ni haki yangu kwa nafasi yangu na nikija bungeni kama wataharibu, nawalipua ...niliwahi kuwalipua viongozi mbalimbali wa juu kwa nyara za maliasili, sasa nitakuwaje kwenye utatu, wenye utatu wanalipuana?” Alihoji.
Msigwa aliwataka Watanzania kuwa na uchungu na maliasili za taifa kwa maslahi ya taifa badala ya kuachia wachache wakihujumu.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment