Writen by
sadataley
6:05 PM
-
0
Comments
Na Nuzulack Dausen, MwananchiDar es Salaam. Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Peter Msigwa ameonyesha video inayobainisha namna baadhi ya kampuni za uwindaji nchini zinavyotumia vibaya leseni zao na kufanya ujangili.
Video hiyo, aliyoiita ya ushahidi alioutoa bungeni
kwa Spika Anne Makinda wakati akiwasilisha bajeti mbadala ya wizara
hiyo mwezi Mei, inaonyesha wawindaji wa kampuni ya Green Mile Safaris
Ltd wakifanya uwindaji kinyume na taratibu na sheria.
Video hiyo ya inayoitwa Tanzania Hunting Trip
Season 2012’, iliyotengenezwa mwaka 2012 na Green Mile Safaris kwa lengo
la matangazo, inaonyesha wawindaji wenye asili ya Kiarabu wakifanya
‘ufundi’ wa kuua wanyama wakiwa ndani ya gari pia wakitumia baadhi ya
bunduki kali kama Sub Mashine Gun (SMG) zenye viwambo vya kuzuia sauti.
Pia mmoja wa wawindaji katika moja ya sehemu za
video hiyo, anaonekana akimfundisha kuwinda wanyama wadogo na ndege
mvulana mwenye umri wa kati ya miaka 12-15.
Aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana
kuwa ameamua kutoa ushahidi huo kutokana na Serikali kutochukua hatua
zozote kuhusu kampuni za uwindaji zinazokiuka sheria.
Msigwa alisema wawindaji hao wanaonekana wazi
kukiuka sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 kwa kuwinda wanyama wadogo
na kutumia magari binafsi kuwakimbiza wanyama na kuwaua.
Waziri huyo kivuli ambaye pia ni mbunge wa Iringa
Mjini (Chadema), alisema kampuni hiyo ilifanya makosa 11 lakini Serikali
iliiacha iendelee kuwinda bila kuchukua hatua yoyote.
“Kutokana na ubutu wa Serikali hii katika
kusimamia rasilimali zetu, kuzuia uwindaji holela unaokuza ujangili na
kutishia hatima ya maliasili na utalii nchini, kampuni hii imekiuka
kifungu namba 42 cha Sheria ya Wanyamapori ya 2009, kinachoeleza kuwa
mtu yeyote atakayemjeruhi mnyama atatakiwa kutumia juhudi zote kadiri ya
uwezo wake kumuua mnyama ndani ya muda mfupi iwezekanavyo,” alisema
Msigwa.
Msigwa aliitaka Serikali kuzifanyia uchunguzi wa kina kampuni zote za uwindaji nchini ikiwa ni pamoja na Green Mile.
“Waziri wa Maliasili na Utalii awawajibishe watendaji wa wizara ambao wameshindwa kutimiza na kutekeleza wajibu na majukumu yao.
Akijibu tuhuma hizo jana, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu alikiri kuwapo kwa video hiyo na kuwa ameshaipa
kazi Idara ya Wanyamapori kufanya uchunguzi juu ya mambo yaliyomo na
iwapo watabaini uhalisia, watatoa majibu stahiki.
“Ni kweli video hiyo ndiyo iliyowasilishwa rasmi
bungeni na mimi nilichukua hatua za haraka ikiwamo kuitask (kuipa kazi)
Idara ya Wanyamapori kuangalia authenticity (uhalisia) wa video hiyo.
“Pia nimewaagiza wataalamu kubaini ni sheria zipi zimevunjwa
iwapo ile video ni ya kweli na ni hatua zipi zichukuliwe ili kuhakikisha
tabia hiyo haijirudii,” alisema Nyalandu.
Alisema anatarajia majibu ya uchunguzi huu
yatatolewa ndani ya wiki mbili kuanzia leo na baada ya wataalamu hao
kuwasilisha matokeo hayo kwake, atatoa tamko rasmi kuhusu hatua ambazo
Serikali itazichukua.
Pia alisema Serikali inawasaka watuhumiwa waweze kujibu tuhuma hizo.
No comments
Post a Comment