Writen by 
                            sadataley
12:41 PM
                            - 
                            
0
                            Comments
                          
            
Rais Jakaya Kikwete (Kushoto) akiwa na Mbunge wa Monduli (CCM)Edward Lowassa  
            
Na Raymond Kaminyoge, MwananchiDar es Salaam. Vigogo sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambao walipewa onyo kali na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 12 wamezidi kukitesa chama hicho, na katika kuwadhibiti, kimetoa maagizo kwa Kamati ya Usalama na Maadili kufuatilia nyendo zao.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao cha kawaida
 cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, kuwa 
kamati hiyo ifanye mapitio ya mwenendo wa utekelezaji wa adhabu kwa 
vigogo hao waliotiwa hatiani kwa kufanya kampeni za urais kabla ya 
wakati.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa 
zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa 
Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
 na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na 
Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na 
Madini, William Ngeleja.
Vigogo hao ambao wamekuwa wakitajwa na wakati 
mwingine wenyewe kuzungumzia nia ya kushika nafasi hiyo, walipewa onyo 
kali ikiwamo kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 tangu Februari 
mwaka huu ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokiuka
 maadili ya chama hicho.
Vigogo hao walipatikana na makosa ya kuvunja ibara
 ya 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inayozuia kutoa 
michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya 
kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya 
eneo husika.
Jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi 
na Uenezi, Nape Nnauye alisema mwezi ujao kamati hiyo itafanya mapitio 
ya utekelezaji wa adhabu hiyo ili kubaini iwapo wanaitekeleza au la.
“Kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo 
masharti ya adhabu zao, itapendekezwa kwa Kamati Kuu ili waongezewe 
adhabu nyingine kufuatana na taratibu za chama,” alisema Nnauye.
Kwa mujibu wa Nnauye, Kamati Kuu imepokea taarifa 
za kuwapo kwa harakati za baadhi ya wanachama walioonyesha nia ya kuomba
 ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya kutafakari kwa kina Kamati Kuu 
inawakumbusha kuwa ili wanachama hao wasipoteze sifa za kugombea, ni 
muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia 
masuala hayo,” alisema Nnauye.
Tangu wapewe adhabu hiyo, makada hao wamekuwa 
wakijitokeza hadharani kwa nadra, lakini Makamba na Wassira walikaririwa
 na vyombo vya habari wakitangaza nia ya kugombea urais.
Hata hivyo, CCM ilisema kuwa Makamba hakukiuka 
taratibu kwa kutangaza nia hiyo, ingawa Rais Jakaya Kikwete alisema 
mtoto huyo wa katibu mkuu wa zamani wa chama hicho anataka mambo makubwa
 na hakumtaarifu nia hiyo.
Yajadili Ukawa 
Kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya, Nnauye 
alisema Kamati Kuu imefurahishwa na mazungumzo yanayosimamiwa na Msajili
 wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kati ya CCM na vyama 
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujaribu kuwashawishi 
wapinzani kurejea bungeni.
“Kamati imepongeza juhudi zinazofanywa na msajili 
na kwamba ni imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda ili wajumbe
 waliosusia Bunge Maalumu la Katiba waweze kurejea kuendelea na mijadala
 ya mchakato wa Katiba Mpya,” alisema Nnauye.
Wajumbe wa Bunge wanaounda Ukawa walisusia Bunge 
Aprili mwaka huu ni kutoka vyama vya upinzani vya Chadema, NCCR-Mageuzi,
 CUF na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 ili kushinikiza kujadiliwa kwa
 rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza muundo wa 
serikali tatu badala ya ile ya serikali mbili inayodaiwa kupigiwa debe 
na CCM.
Wajumbe hao wanasisitiza hawawezi kurudi bungeni 
hadi watakapohakikishiwa kwamba kitakachokwenda kujadiliwa bungeni ni 
Rasimu ya Katiba na si vinginevyo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mutungi ameanzisha 
mazungumzo na vyama hivyo ili kuwashawishi wajumbe kubadilisha uamuzi 
wao na hatimaye kurejea bungeni Agosti 5, mwaka huu.
 
 
 
 
 
 
 
No comments
Post a Comment