Writen by
sadataley
1:31 PM
-
0
Comments
Na Elias Msuya na Aidan Mhando, MwananchiDar/Mwanza. Siku moja baada ya Steven Wassira kutangaza nia ya kutetea ubunge wa Jimbo la Bunda mwakani, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya amesema anashangaa kuona mwanasiasa huyo mkongwe anaweweseka kwa kutojua ni nafasi ipi anaitaka.
Bulaya, ambaye alisema muda wa yeye kutangaza nia
ya kugombea nafasi hiyo bado haujafika, alishangaa kuhusu hatua ya
waziri huyo wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) kutangaza
kugombea ubunge kuwa ni kukiuka kanuni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa katika kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu
ya CCM wilayani Bunda juzi, Wassira (69) alitangaza nia hiyo huku
akijigamba kuwa yeye ni mwarobaini wa matatizo ya wananchi wa jimbo hilo
na hivyo atagombea tena ubunge mwakani.
Akizungumza na gazeti hili jana, Bulaya, ambaye
amekuwa akijishirikisha kwenye shughuli mbalimbali za kijamii kwenye
jimbo hilo ikiwa ni pamoja na kuendesha mashindano ya mpira wa miguu,
alisema ingawa wazee na akina mama wa Bunda wanamwomba awanie nafasi
hiyo kwenye uchaguzi mkuu, muda wake kutangaza nia hiyo bado.
Bulaya alisema: “Mimi namshangaa Wassira kwa
kutangaza kutaka ubunge wakati anatumikia adhabu aliyopewa na chama.
Mimi siwezi kusema chochote sasa hivi kama nitagombea ubunge mwaka 2015
au la,” alisema Bulaya na kuongeza: “Kwa taratibu na kanuni za chama
muda wa kutangaza nia bado, ndiyo maana Wassira na makada wengine
walishapewa onyo walipobainika kuanza kampeni za urais,” alisema Bulaya.
Aliongeza: “Wenye haki ya kuchagua viongozi ni
wananchi. Kama wananitaka wao ndiyo watanichukulia hadi fomu. Kizuri
chajiuza, kibaya chajitembeza,” alijigamba Bulaya na kufafanua kuwa
upepo mzuri katika siasa ni wananchi, kama wanakuunga mkono huna haja ya
kuwa na wasiwasi.”
“Mwaka 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete anataka
kugombea urais, aliacha ubunge, lakini yeye mara atake urais, mara
ubunge. Mtu anayejiamini hawezi kugombea nafasi mbili. Kizuri chajiuza,
kibaya chajitembeza,” alisema Bulaya.
No comments
Post a Comment