Writen by
sadataley
4:59 PM
-
0
Comments
Na Habel Chidawali na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema
Wizara ya Maliasili na Utalii inaongozwa kwa ubabaishaji na ‘mvutano wa
kimasilahi’ baina ya waziri na katibu mkuu, hivyo kukwamisha shughuli
za kuendeleza utalii.
Msemaji wa kambi hiyo (Maliasili na Utalii),
Mchungaji Peter Msigwa alitoa kauli hiyo juzi wakati akisoma maoni
kuhusu hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara hiyo kwa
mwaka 2014/15.
Alisema kambi ya upinzani inasikitishwa na mvutano
baina ya Waziri Lazaro Nyalandu na Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarishi
ambao unaonyesha udhaifu wa Serikali.
“Hii inathibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa
kuwa, waziri na katibu mkuu wa wizara moja wanafanya kazi bila
kushirikiana na kila mmoja anaonekana kumvizia mwenzake hadharani badala
ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge,” alisema Msigwa.
Alisema kitendo cha Waziri Nyalandu kuwasimamisha
kazi wakurugenzi wawili, lakini wakarudishwa na katibu mkuu huku akisema
taratibu za kuwafukuza hazikufuatwa na hii ni dalili kuwa hata yeye
(Nyalandu) siyo msafi kwa kuwa anashindwa hata kujua mipaka yake ya
kazi.
Mbali na mvutano huo, Msigwa alisema maazimio ya
Bunge kuhusu matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili yanaendelea
kupuuzwa na watumishi wenye tuhuma wakihamishwa vitengo.
“Ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote
hamfichi mnafiki na debe tupu haliachi kutika (siyo maneno yangu, bali
ya wahenga). Siyo mara ya kwanza kambi ya upinzani kuhoji juu ya usafi
wa Lazaro Nyalandu,” alisema.
Alisema Waziri Nyalandu alipozungumza katika kikao
cha wadau wa ulinzi wa maliasili Juni mwaka jana mkoani Iringa,
aliahidi kuwa majina ya majangili yakiwamo ya vigogo yangetangazwa
hadharani, lakini hadi sasa hakuna majina yoyote yaliyotangazwa
hadharani.
Uteuzi wa Sarakikya
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema) alizungumzia kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Paul
Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori, jambo alilosema
ni kinyume na haki za binadamu.
Msemaji huyo alibainisha kuwa, wakati wote
Watanzania wanajiuliza maswali ambayo hayajapata majibu kuhusu vigezo
vilivyotumika kumteua Sarakikya.
“Katika Operesheni Tokomeza, mtu huyu alikuwa
kiongozi wa utekelezaji wa moja kwa moja na kinachodaiwa ni uvunjifu wa
haki za binadamu, inashangaza kuona mtu huyu tena ndiye ana nafasi ya
kukaimu ukurugenzi, lini kawa msafi?” alihoji Msigwa.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Wizara-ya-Maliasili-inaongozwa-kwa-ubabaishaji/-/1597296/2314974
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Wizara-ya-Maliasili-inaongozwa-kwa-ubabaishaji/-/1597296/2314974
No comments
Post a Comment