Writen by
sadataley
4:51 PM
-
0
Comments
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
umefafanua hoja ya kuanzisha ushirikiano katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2015 ni kujenga serikali imara yenye kuheshimu matakwa ya wananchi.
UKAWA inaundwa na vyama vinavyounga
mkono rasimu ya katiba ya serikali tatu iliyowasilishwa bungeni na
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba
ambavyo ni CUF, CHADEMA, NCCR- Mageuzi, UDP, DP na vyama vingine ambavyo
wajumbe wake walisusia Bunge la Katiba.
Mwishoni mwa wiki iliyopita wakiwa
katika mikutano ya hadhara visiwani Zanzibar, baadhi ya viongozi wa
UKAWA walikaririwa na vyombo vya habari kwamba wanakusudia kusimamisha
mgombea mmoja katika uchaguzi mkuu mwakani kuanzia udiwani, uwakilishi,
ubunge na urais.
Akifafanua sababu za UKAWA kuingiza
ajenda nyingine ya kutaka kushirikiana katika uchaguzi mkuu wa mwakani,
Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema
wamefanya hivyo ili mamlaka ambazo ni serikali na Bunge ziweze kuheshimu
matakwa ya wananchi.
Profesa Lipumba alisema ili kuhakikisha
mamlaka hizo zinatekeleza wajibu wake, zitasukumwa na UKAWA ambayo
ilibaini makosa yake hapo awali na sasa imekuja kwa lengo moja la
kuwatetea wananchi na kuwatimizia yale wayatakayo katika katiba na
siasa.
“UKAWA haijaja kwa maswala mengine,
imekuja ili ipatikane serikali imara yenye Bunge lenye kuheshimu matakwa
ya wananchi… ndiyo maana tunataka kuhakikisha suala la katiba na
uchaguzi vinakwenda sambamba,” alisema Profesa Lipumba.
Wakati huo huo, CUF imebariki suala la
kuanzishwa kwa UKAWA na kueleza kuwa hoja zilizotolewa kwa ajili ya
kuanzishwa umoja huo zina maslahi kwa wannachi na taifa kwa jumla.
Msimamo huo umetolewa na wajumbe wa
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho linaloendelea na vikao
vyake jijini Dar es Salaam kwa siku tatu hadi kesho likiwa na ajenda
mbili.
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na
Haki za Binadamu wa CUF, Abdul Kambaya, alisema ajenda zinazojadiliwa
katika mkutano huo ni kuhusu kuanzishwa kwa UKAWA na madhumuni yake
pamoja na namna watakavyofanya uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Kambaya alisema wakiwa katika ajenda ya
kwanza iliyohusu UKAWA ambayo ilitolewa kama taarifa na viongozi wake,
ilipokelewa kwa furaha na kuwataka waendelee na msimamo huo wenye
maslahi kwa wananchi na taifa.
“Pamoja na kuwataka waendelee na msimamo
huo, tumewaonya wajumbe wote wa UKAWA na wajumbe wengine 201 wanaounga
mkono rasimu ya Jaji Warioba kutokubali kuyumbishwa na wajumbe wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ambao wana msimamo wao.
“Nafikiri sasa viongozi wetu wa juu
wamejifunza kutokana na makosa… sasa hawataki kurudia makosa na katika
kufanya hivyo, naiona CCM iking’oka madarakani, wagombea udiwani,
uwakilishi na ubunge katika nafasi ya UKAWA wakishinda kwa ushindi
mkubwa,” alisema Kambaya.
Habari kwa hisani ya chademablog.blogspot.com/
No comments
Post a Comment