Writen by
sadataley
4:17 PM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe, MwananchiDar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti, Serikali imeshindwa kutekeleza bajeti ya mwaka 2013/14 kutokana na kukosa fedha na hivyo kusababisha miradi mbalimbali katika halmashauri nchini kukwama.
Katika bajeti ya mwaka 2013/14 Serikali ilitenga
Sh4.2 trilioni kwa ajili ya halmashauri zote nchini, lakini fedha za
maendeleo zilizofika katika halmashauri hizo ni asilimia 43 tu na za
matumizi ya kawaida asilimia 76, hivyo halmashauri kushindwa kutekeleza
miradi iliyojipangia kwa kipindi hicho cha mwaka wa fedha.
Juzi wakati akisoma Mwelekeo wa Bajeti ya mwaka
2014/15, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya alisema sababu ya
kutotekelezwa kwa miradi mbalimbali ni kutokana na Serikali kushindwa
kukusanya kodi ipasavyo katika mwaka wa fedha wa 2013/14.
Alisema pia kulikuwa na mapato pungufu ya kodi ya
kampuni kuliko ilivyotarajiwa kutoka kwenye baadhi ya kampuni za madini
kutokana na kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kampuni za simu za
mkononi kutokusanya tozo ya kadi za simu ambayo ilitarajiwa kuiingizia
serikali mapato ya Sh178 bilioni.
Kwa mujibu wa Mkuya hadi kufikia Machi mwaka huu,
mapato ya halmashauri yalifikia Sh213 bilioni sawa na asilimia 74 ya
makadirio ya kipindi husika.
Alieleza kuwa katika kipindi hicho mapato
yasiyotokana na kodi yalifikia Sh324 bilioni sawa na asilimia 58, wakati
lengo lilikuwa ni kukusanya Sh555 bilioni.
Katika bajeti ya mwaka 2014/15 inayoanza Julai Mosi mwaka huu, Serikali imetenga Sh4.9 trilioni kwa ajili ya halmashauri.
Katika mwaka wa fedha wa 2013/14, serikali
ilipanga kutumia Sh18.2 trilioni kutoka vyanzo vya mapato vya ndani na
nje na Sh12.6 trilioni yalikuwa matumizi ya kawaida na Sh5.6 trilioni ni
matumizi ya maendeleo.
Katika mwaka wa fedha wa 2014/15 Serikali imeeleza
kuwa itatumia Sh19.6 trilioni kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi.
Kati ya mapato hayo, mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ni Sh11 trilioni
na vyanzo kutoka halmashauri ni Sh462.2 bilioni.
Akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Hamisi
Kigwangalla alikiri uwapo wa tatizo hilo na kufafanua kuwa katika bajeti
ya mwaka wa fedha 2013/14, fedha zilizopelekwa katika halmashauri zote
nchini ni asilimia 43 tu ya fedha walizotengewa.
“Kama kamati tumeamua kuzibana halmashauri ili
zikusanye mapato yake ya ndani na kutenga asilimia 60 ya mapato hayo kwa
ajili ya kusaidia miradi ambayo haijafanyika kutokana na kukosa fedha
kutoka Serikali Kuu.”
Alisema kamati yake imebaini kuwa katika mwaka wa fedha wa
2013/14 miradi mingi imekwama na kusema kuwa iliyoweza kufanyika ni ile
ambayo ipo katika sekta zilizowekewa kipaumbele na Serikali.
Alisema mbali na fedha za maendeleo, fedha nyingi
zinazopelekwa katika halmashauri hizo huishia katika kulipa mishahara na
matumizi mengineyo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC), Rajab Mbarouk Mohamed amesema asilimia 60 ya bajeti
hazifiki katika maeneo husika, hivyo kukwamisha shughuli nyingi za
maendeleo.
Alifafanua kuwa kutofika kwa asilimia 60 ya bajeti
katika maeneo husika kunachangiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
kutokusanya mapato ipasavyo pamoja na kuchelewa kwa fedha za nchi
wahisani.
“Serikali ni kama imepooza, kwa kuwa fedha
zinazotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo hazifiki
sehemu husika. Hili limekuwa tatizo na linatakiwa kupatiwa ufumbuzi,”
alisema Mbarouk.
Alisema kitendo cha Serikali kutokuwa na vyanzo
vya mapato vya kutosha na vya uhakika nayo ni moja ya sababu ya kukwama
kwa shughuli mbalimbali.
Mbali na kueleza hayo, Mbarouk alifafanua kuwa
kati ya fedha hizo asilimia 20 hupotea kutokana na uwezo mdogo wa elimu
walionayo madiwani ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa fedha hizo.
“Fedha hizi zinapotea kwa sababu madiwani ambao ndiyo wasimamizi wakuu wameshindwa kudhibiti wizi,” alisema.
Alipoulizwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima
kuhusu bajeti finyu iliyopelekwa katika halmashauri nchini alisema
maswali yote yanayohusu bajeti yatajibiwa Jumanne ijayo na Waziri Mkuya,
bungeni Dodoma.
Kwa upande wake mjumbe wa Kamati ya LAAC, Ezikiel
Maige alisema kitendo cha Serikali kushindwa kupeleka fedha katika
halmashauri kinakwamisha utekelezaji wa miradi iliyoahidi kwa wananchi.
“Asilimia 80 ya miradi ambayo Serikali imeahidi
inatekelezwa kupitia halmashauri na kama fedha ikikosekana maana yake ni
kwamba serikali imeshindwa kutekeleza ilichokiahidi,” alisema.
Alisema licha ya kuwapo kwa vikwazo mbalimbali
katika utafutaji wa fedha ni vigumu kwa wananchi kuelewa vikwazo hivyo,
“Katika hili Serikali inaweza kutoa maelezo lakini yasieleweke kwa
wananchi,” alisema Maige.
No comments
Post a Comment