Writen by
sadataley
8:03 AM
-
0
Comments
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.PICHA|MAKTABA
Na Mwandishi wetu
Dodoma. Sasa ni dhahiri kuwa Serikali iko taabani kifedha na hali hiyo imeanza kuwatia hofu wabunge hasa baada ya kubainika kwamba katika bajeti ya mwaka 2013/2014 pekee, kuna upungufu wa Sh1.8 trilioni.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wizara kupatiwa fedha kati ya asilimia 25 na 30 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge mwaka jana na hali hiyo inatarajiwa pia kuzikumba baadhi ya wizara kwa bajeti ya 2014/2015, hivyo kushindwa kutekeleza vyema mipango yake.
Mfano mzuri ni Wizara ya Maji ambayo Waziri wake, Profesa Jumanne Maghembe alipoulizwa alikiri kuwapo kwa upungufu mkubwa wa fedha na kwamba kwa mwaka 2013/2014 ilipatiwa asilimia 30 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge.
Profesa Maghembe ambaye bajeti ya wizara yake imesogezwa mbele hadi Mei 31, mwaka huu ili kutafuta fedha zaidi, alisema anazo taarifa za wabunge wengi kuikamia wizara yake kutokana na miradi mingi ya 2013/2014 kutokutekelezwa lakini akasema tatizo si yeye, bali uhaba wa fedha uliojitokeza.
Hata hivyo, alisema pamoja na ufinyu huo, miradi iliyotekelezwa kati ya Julai, 2013 hadi Machi mwaka huu imeongeza watumia maji hadi kufikia 2,640,000.
“Huko nyuma kila mwaka tulikuwa tunaongeza watumia maji 200,000 lakini kwa Julai mwaka jana tu, hadi Machi mwaka huu licha ya kupata fedha kidogo tumeongeza watumia maji mara 10,” alisema.
Siku chache kabla ya Bunge la Bajeti, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alilieleza gazeti hili kuwa nakisi katika bajeti ya 2013/2014 ilisababishwa na matumizi ya Serikali kuwa makubwa kuliko mapato.
Mkuya ambaye jana hakupatikana kuzungumzia hali hiyo, wakati huo alisema pia utegemezi wa wahisani ni tatizo kwa kuwa baadhi yao hawakutoa fedha walizoahidi kutokana na hofu hasa kwa upande wa usalama wa fedha zao.
Wabunge mbalimbali waliohojiwa kwa nyakati tofauti walisema tatizo ni baadhi ya wabunge kugeuka kuwa sehemu ya Serikali badala ya kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia na kuishauri.
Waziri kivuli wa Fedha, James Mbatia alisema tatizo linaloitafuna nchi ni kutokuwapo nidhamu ya matumizi na kwamba fedha nyingi zinakwenda kwenye matumizi ya anasa kuliko maisha ya wananchi.
Mbatia alisema taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha kuwa imekuwa ikikusanya mapato kati ya asilimia 90 na 100 na wakati mwingine kuvuka lengo lakini bado hazitoshi.
“Mfano mdogo tu ni sherehe za Muungano, mbwembwe zote zile nchi iko taabani kifedha… Watoto hawana madawati barabara za Dar es Salaam ni mashimo matupu… matumizi ya ajabu ya anasa ya Serikali,” alisema.
No comments
Post a Comment