Writen by
sadataley
5:02 PM
-
0
Comments
Na Mwananchi
Nchi nzima imekumbwa na taharuki kutokana na watu zaidi ya 400
kuugua homa ya dengue na tayari watu watatu wamepoteza maisha, akiwamo
daktari bingwa wa magonjwa ya akili aliyekuwa akifanya kazi Hospitali ya
Temeke, jijini Dar es Salaam. Hofu hiyo kwa kiasi kikubwa imetokana na
habari kwamba ugonjwa huo hauna tiba wala chanjo na husababishwa na aina
ya mbu ajulikanaye kama aedes, ambaye husambaza maradhi hayo nyakati za
mchana.
Kinachotia hofu zaidi ni mwenendo usioridhisha wa
Serikali ambayo imekuwa kama mtazamaji katika kupambana na ugonjwa huo.
Badala ya kuongoza na kuonyesha njia, kwa maana ya kubuni mikakati ya
kupunguza kasi ya ugonjwa huo na kutoa taarifa za uhakika na kwa wakati
kwa wananchi, Serikali imejenga taswira ya kutokuwa na uwezo katika
mapambano hayo. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilisema juzi kwamba
itapeleka taarifa za kuwapo kwa ugonjwa huo nchini katika Shirika la
Afya Duniani (WHO) kama mwongozo wa kanuni za afya za kimataifa
unavyoelekeza.
Kitu muhimu hapa ni aina ya taarifa zitakazotumwa
kwa shirika hilo, kwani kulitaarifu tu kuhusu uwapo wa janga hilo hapa
nchini siyo muhimu kwa kuwa tayari suala hilo linajulikana.
Kinachotakiwa ni taarifa zenye takwimu sahihi, ikiwa ni pamoja na idadi
kamili ya watu walioambukizwa na maeneo wanakotoka. Tunasema hivyo
kutokana na takwimu zilizotolewa na Serikali kutiliwa shaka na kukosa
uhalisia kulingana na ukubwa wa tatizo. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba
idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa huo ni kubwa mno kulinganisha na
idadi ya watu 400 nchi nzima iliyotajwa na Serikali juzi. Taarifa
tulizonazo ni kwamba Hospitali ya Mwananyamala pekee imepata wagonjwa
wapatao 300 kati ya Aprili na mwezi huu.
Ofisi ya WHO iliyopo jijini Dar es Salaam jana
ilitoa tahadhari kwamba dengue sasa ni janga na kuonya kuwa,
zisipopatikana takwimu sahihi za ugonjwa huo nchi nzima, hali itakuwa
mbaya sana baadaye. WHO ilisema ugonjwa huo ni suala mtambuka, kwa maana
ya kuzigusa wizara nyingine nyingi, hivyo isiachiwe Wizara ya Afya
pekee, bali pia wizara zinazohusika na miundombinu, maji, ujenzi na
kadhalika lazima zihusishwe.
WHO inasema pia kwamba lazima utafiti ufanyike ili
kujua tabia za mbu hao na virusi vipi vimesambazwa kulinganisha na
maeneo mengine yenye ugonjwa huo. Dengue iliingia nchini mwaka 2010 na
kuua baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Serikali
haikutaka kuufahamu ugonjwa huo na hivi sasa ndipo taasisi zake kama
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Muhimbili (MUHAS) na Taasisi ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) zinahaha kufanya tafiti ili
kuufahamu na kuishauri Serikali.
Tunaitaka Serikali ielekeze nguvu zake katika
kuutokomeza ugonjwa huo. Zinahitajika fedha nyingi, vifaa na vitendea
kazi vya kuchukulia vipimo na kutoa kinga kwa wauguzi na madaktari ili
wasizidi kuambukizwa na kupoteza maisha. Vipimo visitozwe fedha ili
kunusuru maisha ya wagonjwa wasio na uwezo kifedha. Ianzishwe operesheni
maalumu kunyunyizia dawa katika mazalio ya mbu na kazi hiyo iwe
endelevu badala ya zimamoto. Matarajio yetu ni kwamba Serikali
haitafanya mzaha tena katika kupambana na homa ya dengue.
No comments
Post a Comment