Writen by
sadataley
1:58 PM
-
0
Comments
Na Mussa Juma, MwananchiArusha. Rais Jakaya Kikwete amesema serikali inakusudia kuboresha utendaji wa mahakama nchini kwa kuongeza ajira na kuendelea kufanyia mabadiliko sheria ambazo zimepitwa na wakati.
Kwa kuanzia, Rais alisema katika siku chache
zijazo Serikali itaajiri mahakimu 600 wa mahakama mbalimbali ili
kupunguza upungufu wa watumishi hao.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Majaji
Wanawake Duniani (IAWJ) jijini hapa, Rais Kikwete alisema kutokana na
upungufu wa watendaji wa mahakama na mahitaji mengine, wananchi wengi
hasa maskini na wanawake, wanakosa haki zao.
“Serikali ina mikakati kadhaa ya kuhakikisha
inaboresha sekta ya mahakama nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata
haki kwa wakati,” alisema
Aliwataka majaji wanawake kuendelea kusaidia
upatikanaji wa haki kwa wakati ili kuondoa matatizo ya kesi kusikilizwa
kwa muda mrefu.
Awali rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani,
Jaji wa Rufaa Mstaafu Eusebia Munuo alisema kaulimbiu ya mkutano huo ni
kutolewa haki kwa usawa kwa wananchi wote.
Alisema utoaji wa haki kwa usawa ni suala la
utekelezwaji wa haki za binadamu na akatoa wito kwa majaji wanawake
kusaidia wananchi kupata haki zao.
Akizungumza mapungufu ya sheria, alitaka kuunga
mkono jitihada za serikali ya Tanzania kuendelea kufanya mabadiliko ya
sheria hasa ambazo zimepatwa na wakati.
Alisema mkutano huo ambao umewashirikisha majaji
zaidi ya 600 umeandaliwa kwa pamoja na IAWJ na Chama cha Majaji Wanawake
Tanzania (TAWJA).
Mkutano huo wa siku nne unafanyika kwa mara ya kwanza nchini tangu chama hicho kianzishwe mwaka 1991.
Jaji Munuo alisema, mkutano huo unashirikisha
majaji zaidi ya 600 wanawake kutoka nchi mbalimbali duniani wakiongozwa
na rais wa chama hicho.
Alisema mkutano huo utatoa fursa ya kupanua wigo
wa mawasiliano kati ya majaji wanawake ili kujenga mazingira mazuri ya
utendaji kazi pamoja na kujenga ubora na uadilifu katika utoaji wa haki
na ukuzaji wa haki za binadamu.
No comments
Post a Comment