Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Wednesday, May 7, 2014

Ni ‘vita’ baina ya serikali na wananchi na siyo upinzani


 
Na Padri Baptiste Mapunda, Mwananchi
Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini   mwaka 1992, hali ya kisiasa imekuwa ni ya mvurugano. Watawala, CCM wamekuwa wakilinda nafasi yao ili isichukuliwe na wapinzani.
Mfumo wa chama kimoja uliwaaminisha watu kwamba CCM ndicho chama pekee kinachostahili kutawala na watu waliamini. Hivyo  kimantiki  ujio wa vyama vingi ulikuwa ni vita.
“Siasa siyo harusi, wala sherehe, siasa ni vita na siasa inahusu kutawala na madaraka yananoga. Hakuna anayependa kuachia kirahisi,” alisema mwanasiasa mmoja wa Kenya katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2007.
Kiuhalisia, inaonekana wazi kwamba CCM walilazimishwa au kushinikizwa kukubali mfumo wa vyama vingi.
Tangu hapo siasa za Tanzania  hazijatulia hadi tunafikia leo muda wa kujaribu kuandika Katiba mpya. Vita hiyo bado imeingizwa huko kiasi cha kutia shaka  kwa wananchi kama kweli tutapata katiba bora au bora katiba.
Pia muda wote huu vita hii ilikuwa  baina ya serikali ya CCM,   yaani chama tawala na wapinzani wao hasa wale wanaounda chama kikuu cha Upinzani; mwanzoni walikuwa  NCCR-Mageuzi, wakaja CUF na sasa Chadema.
Wapinzani nao wamekuwa na mbinu za jinsi za kuendesha siasa zao pamoja na kwamba chama tawala kinajaribu kuwabana kila kona.
Hata hivyo pamoja na upinzani kubanwa  na vyombo vya dola, Tume ya Uchaguzi  pamoja na Serikali, bado upinzani unaendelea kukua kwa kiwango kikubwa.
Kuna baadhi ya mikoa kama Arusha, Mbeya, Mwanza, Mara, Kagera na hata Iringa na Ruvuma upinzani unasonga mbele hata kama ni kwa kupitia mateso, dhuluma na  pengine hata kupoteza maisha.
Kama tunapenda kuambiana ukweli lazima tuseme wazi kwamba kwa sasa Watanzania hawadanganyiki katika mambo mengi.
Siasa za Tanzania zimekuwa na dosari nyingi hata kama chama tawala hakitaweza kukubali. Muda wote  kumeonekana wazi kuwa hali halisi ni ya vita kati ya serikali ya CCM na  upinzani.
Hata hivyo, jinsi siku zinavyopita na hasa katika zoezi la kuandika Katiba mpya kupitia mijadala ya Bunge la Katiba lililoahirishwa, vita hii inaonekana kuhama.  Imehamia kwa nani?
Kwa mtu mwenye kupenda kutafiti nini kinaendelea katika nchi yetu atagundua kwamba vita ya kisiasa imehama kutoka kwa serikali ya CCM na kuhamia kwa wananchi na siyo tena wapinzani.
Hili limefanyika bila serikali ya CCM kufahamu kana kwamba Mungu ndiye alifanya jambo hili bila mtu kufahamu.
Hata hivyo, kilichotokea ni kwamba inaonekana wazi wananchi wengi wamechoshwa na siasa za chama tawala, siasa za kuahidiahidi kila wakati, lakini vitendo ni kidogo.
Pia ukweli ni kwamba ukisoma alama za nyakati utagundua kwamba, nyakati hizi ni nyakati za mabadiliko duniani. Tanzania siyo kisiwa na hivi nayo imekumbwa na mkondo huu wa mabadiliko  itake isitake huu ndiyo ukweli.
Mabadiliko si wingi wa serikali
Mabadiliko hayo hayategemei serikali moja, mbili, tatu, saba wala kumi. Hii siyo hoja ya msingi. Naona hilo ni jambo la msingi kwa chama tawala kulifahamu na wala siyo kitu  cha kubeza. Watanzania wa leo si wa jana, wala juzi, wala wa mwaka l968.
Ukweli mwingine ambao umesaidia kuhamishia vita hii kwa wananchi badala ya kuendelea kubaki kwa wapinzani ni kwa sababu  wapinzani wanaonekana kutetea  masilahi ya umma (taifa au watu wote bila kujali itikadi za kisiasa, dini, kabila, wala rangi).
Kinyume chake ni kwamba kila wakati CCM wanaonekana kutetea masilahi ya chama chao, ili kuendeleaa kuwepo madarakani kwa kutumia mbinu mbalimbali hata kama ni dhalimu.
Mfano ni mjadala wa Rasimu ya Pili ya Katiba  mpya ambayo imesheheni maoni, mawazo na matashi ya wananchi na ambayo ndiyo msingi wa katiba yetu, lakini CCM wameamua kujaribu kupenyeza mawazo ya chama chao. Je, kwa mantiki hii wananchi watampenda nani?
Siyo hili pekee. Hata taasisi kama vile taasisi za dini,  mathalan maaskofu wa Kanisa Katoliki katika umoja wao, wametoa ujumbe unaowataka wajumbe wa Bunge  hilo kuheshimu mawazo na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Je, viongozi wakuu kama hao kwa nini waje na ujumbe kama huu, wakati wa mvurugano kama huu? Serikali ya CCM imejiuliza vya kutosha maana yake ni nini?
Pia tumeona Taasisi ya Kiislamu nayo imekuja na tamko kama hilo na hivi kuungana  pamoja na maaskofu.
Dini kuu mbili nchini  kama zinakuja na wazo moja maana yake ni nini? Lakini, pia kuna taasisi nyingine kama Chama cha Walimu (CWT), Tanzania, Tucta,  na wengineo, wote wanatetea mabadiliko yaliyoletwa na rasimu ya Tume ya Warioba.
Hivi sasa wale wanaofikiri kwamba kumshambulia, kumdhalilisha na kumtukana Warioba ni mbinu yao ya kuudhoofisha  mawazo ya wananchi, basi wajue wanajisumbua.
Mwalimu Nyerere alitufundisha mambo mengi, lakini moja  la msingi ninalolikumbuka ni “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.”
Wana CCM nchini  ni zaidi ya milioni  nane, na hivi wao si wengi kuzidi wananchi wanaobaki.
Kwa mantiki hii kama wananchi wanataka mabadiliko, basi yatapatikana tu.  Mtazamo mwingine ni huu  kwamba wananchi wameanza kugundua kwamba Watanzania wanaishi katika dunia inayobadilika.
Msimamo wa Ukawa
Kususia vikao kulikofanywa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni  alama nzuri ya kujua nini kinaendelea katika bunge hilo.
Hatua yao ilikuwa ni kupinga kuwa sehemu ya kuwasindikiza wajumbe wa CCM katika kile wanachokiita kusimamia msimamo wao wa kubadilisha rasimu ya katiba yenye muundo wa serikali tatu na kuchomeka ile ya serikali mbili ambayo ni msimamo wa chama tawala.
Ni vyema kwa chama tawala kutambua kuwa kuishinikiza Katiba kwa nguvu  hakuleti maana yeyote ile  kwa sababu wananchi wenye Katiba ndiyo mwishowe watakaokuwa na uamuzi wa kuikubali au kuikataa katika sanduku la  kura ya maoni.
Nakumbuka nchini Kenya kuna rasimu ilikataliwa na wananchi kwa sababu chama tawala, KANU wakati ule kilikuwa kimepenyeza sera zake ili kiweze kuendelea kutawala na kukandamiza wananchi.
Wakati ule  Wakenya walikuwa amechoshwa na vitendo vya KANU vya rushwa, unyanyasaji wa wananchi wa kawaida, kupendeleana, kubebana, vyombo vya dola kuua raia hovyo hasa wakosoaji wa serikali, kuua viongozi wa dini, ubambikizaji wa kesi na kadhalika.
Rasimu hiyo ya Kenya ilikataliwa kwa sababu vita ya serikali ilikuwa imehamia kwa wananchi na siyo kubakia kwa  wapinzani.
CCM na propaganda 
Kitu kingine ambacho kimehamisha vita  hii ya serikali ya CCM na kwenda kwa wananchi ni kutokana na propaganda (porojo) zinavyotumiwa na wahusika.
Wengi  wameanza kuelewa propaganda, yaani kusema uongo unaolingana na ukwei na hivi kuweza kuwashawishi  watu wawe upande wako.
Kila wakati nchi yetu inapokuwa na tukio la kuashiria mabadiliko katika serikali au chama, mfano uchaguzi mkuu, kwa kawaida propaganda hutumika sana.
Mfano,  wakati wa uchaguzi  iliibuka porojo kwamba CUF walikuwa wameleta majambia ya kutumika katika uchaguzi na kule Igunga ilisemekana Chadema walikuwa wamekodi Mungiki kutoka Kenya.
Hii propaganda ilitumika kuwaharibia wapinzani kwamba hawafai kuchukua nchi. Propaganda nyingine ni ile ya kusema kwamba mkichagua wapinzani nchi itaingia katika vita kama Rwanda ama Burundi.
Hivi karibuni,  Waziri William Lukuvi alitumia propaganda alipokaribishwa kutoa hotuba katika sherehe za kumsimika askofu kanisani mjini Dodoma.
Alisema: “Kama tutapitisha serikali tatu, basi huenda  Serikali haitakuwa na fedha ya kuwalipa wanajeshi wetu na hivyo kusababisha  kuipindua Serikali na hivyo kusababisha maasi ambayo yatapelekea makanisa kufungwa.”
Huku ni kuwatisha ili watu wakati wa kura za maoni waipigie kura ya ndiyo Katiba itakayopendekeza serikali mbili hata kama mbaya.  Tumshukuru Mungu ameiweka propaganda hii hadharani ili watu wapate kuijua.
Hiyo ni lazima ifike mahali siku moja wananchi waamke kutoka usingizini na kushagaa kujiuliza: “Jamani tupo wapi’?”
*Baptist Mapunda ni  mtaalamu wa mawasiliano Frmapunda91@gmail.com
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment