Writen by
sadataley
5:05 PM
-
0
Comments
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Dodoma. Serikali imeliambia Bunge kuwa, iko katika mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Maafa ili kuliondoa suala la uokoaji kutoka Jeshi la Zimamoto kwenda Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema juzi kuwa katika mabadiliko
hayo ya sheria, JWTZ litakabidhiwa dhamana pia ya kufanya uokoaji majini
na nchi kavu. Lukuvi alitoa kauli hiyo wakati akifafanua swali la
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango
gani wa kuipatia JWTZ, vifaa na teknolojia ya kisasa ya uokoaji.
Mbunge huyo aliomba ufafanuzi huo wakati Bunge
lilipoketi kama kamati, kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Ulinzi na JKT kwa mwaka wa fedha wa 2014/15.
Mbatia alirejea matukio mbalimbali ya maafa,
yakiwamo mafuriko na kuanguka kwa jengo la ghorofa Dar es Salaam ambako
JWTZ lilishiriki katika uokoaji kwa kutumia vifaa duni.
“Jeshi letu kwa hali tuliyonayo sasa, waziri
anasemaje kuwa na vifaa na teknolojia ya kisasa ili maafa yanapotokea
wasitumie mtulinga,” alihoji.
Swali hilo lilijibiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi aliyesema tayari wana mpango wa
kukiimarisha Kitengo cha Uhandisi cha Jeshi ili kiwe na vifaa vya kisasa
vya uokoaji.
Katika nyongeza ya majibu ya swali hilo, ndipo
Lukuvi aliposimama na kusema ingawa ipo Sheria ya Maafa, imekuwa
haisaidii, hivyo Serikali inaifanyia marekebisho ili JWTZ ikabidhiwe
dhamana ya uokoaji.
“Kwa sasa unaweza kuona suala hili la uokoaji
linafanywa na Zimamoto ambao kisheria ndiyo wanaosimamia zimamoto na
uokoaji, lakini mara nyingi tumekuwa tukitumia Jeshi... “Kwa hiyo
tunataka tuwape uwezo wa kisheria wa kushughulikia mambo kama hayo
baharini na uokoaji kama huu ambao utawezesha jeshi lenyewe kuwa na
bajeti ya kufanya mambo hayo kuliko ilivyo sasa wanajiminya kwenye
bajeti zao kwa mambo ambayo kwa kweli hayako ndani ya sheria.
Kauli hiyo ya Serikali kukabidhi shughuli za
uokoaji kwa JWTZ, imekuja wakati kukiwa na mapendekezo ya wadau
mbalimbali kutaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liwe sehemu ya Jeshi la
Polisi.
Hoja hiyo inatokana na ukweli kwamba, mara zote
kwenye matukio ya moto, polisi ndiyo wanakuwa wa kwanza kufika, hivyo
Zimamoto ikiingizwa huko, uokoaji utafanyika sambamba na kazi za ulinzi.
No comments
Post a Comment