Writen by
sadataley
11:16 AM
-
0
Comments
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma. Siku moja baada ya kuteuliwa na CCM
kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema ameanza kupitia sheria na kanuni
zitakazomwezesha kuliongoza huku akiahidi kutenda haki kwa wajumbe wote
iwapo atachaguliwa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Sitta alisema:
“Nawashukuru wote waliokuwa wakiniunga mkono na niseme wazi kuwa
nitatenda haki kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba.”
Alisema kazi kubwa aliyonayo baada ya uteuzi huo
ni kuhakikisha kuwa anazipitia sheria na kanuni zinazoongoza bunge hilo
na sheria nyingine kwa kuwa ndizo nyenzo zake za utendaji kazi.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi ndani ya chama
hicho na mchuano uliokuwapo kati yake na Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge alisema: “Hii ni hatua ya awali na ya kawaida tu ndani ya
CCM. Mara nyingi chama changu kikiona kuna mambo yanayoleta msuguano,
basi huamua kuteua jina moja kwa ajili ya kugombea. Wameteua majina
mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru chama changu kwa kuniteua na
kwa sasa najiandaa na uchaguzi.”
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa upande wake, Mjumbe wa bunge hilo aliyeteuliwa
na CCM kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan
aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ana uwezo mkubwa wa
kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na hana shaka katika uteuzi wake.
Samia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano), alijisifu akisema ana rekodi nzuri ambayo
haitiliwi shaka kwa weledi wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa nafasi
hiyo.
“Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote,” alisema.
Samia aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira na Wanawake
na baadaye, Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kabla ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kinana na mchakato
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta kuwania nafasi hiyo na kusema
ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Hata hivyo, alisema Chenge aliamua kwa hiari yake
kujitoa baada ya kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi wa chama kwa
ushauri. Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Kinana
alisema: “Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la Katiba,
angeweza kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili
walionyesha nia; Sitta na Chenge.
“Wote hawa wana sifa kwa historia za maisha yao. Chenge aliwahi
kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sitta, Waziri wa Sheria na Katiba,
halafu wote ni wanasheria. Hawa wote wakaanza kutafuta maoni kwa wenzao
na kila mmoja akitafuta wenzake wa kumuunga mkono. Kwa sababu wote ni
wanaCCM na kwa kuogopa makundi, tukaona tuwaite na kuwaambia jamani nyie
wote ni wetu, tusingependa mkalumbane.
“Tukawaambia washauriane na kufikia mwafaka.
Chenge akajitoa mwenyewe na jana (juzi), kwenye mkutano, WanaCCM wote
wakaamua kumuunga mkono Sitta.”
Mjadala moto bungeni
Wakati huohuo; mjadala wa kanuni za Bunge la
Katiba umeendelea kuwa moto baada ya baadhi ya wajumbe kutaka kanuni
zitambue haki ya mwanamke katika nafasi hiyo ya juu ya uongozi.
Malumbano hayo yalizuka wakati wajumbe hao
walipokuwa wakijadili kanuni ya saba inayohusu uchaguzi wa mwenyekiti na
makamu wake. Mjumbe wa bunge hilo, Christine Mzava alishauri kuwa
endapo mwenyekiti atakuwa mwanamume, makamu wake awe mwanamke.
Akijibu hoja hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni,
Magdalena Rwebangila alisema kwa kuwa sheria imetamka kuwa mwenyekiti
akitoka Tanzania Bara, makamu atatoka Zanzibar, itakuwa vigumu kuweka
uwiano mwingine wa kijinsia.
Baada ya ufafanuzi huo, Lediana Mng’ong’o
alisimama na kusema: “Kwani mnaona ugumu gani wa kuongeza hicho
kipengele? Mbona Rais katika uteuzi wa wajumbe 201 alizingatia uwiano wa
kijinsia?”
Mjumbe mwingine wa Kamati ya Kanuni, George
Simbachawene alisema haiwezekani kuwa na aina mbili za uwiano. Hali hiyo
ilimfanya mjumbe mwingine, Dk Ave-Maria Semakafu kusimama na kuomba
busara itumike na kutengua kanuni kwa kuweka nafasi sawa.
Hata hivyo, Mjumbe Ezikiah Wenje alisema itakuwa ajabu kumchagua mtu katika nafasi hizo kwa sababu tu ni mwanamke.
“Demokrasia inahitaji ushindani sawa na hao
kinamama wanaamini tuko sawa. Mimi naomba kama kuna mtu ana sifa za kuwa
mwenyekiti au makamu, wagombee washindane,” alisema.
Maelezo hayo yaliwafanya wajumbe wanawake kusimama
na kuanza kuimba: “Tunataka haki zetu, tunataka haki zetu.” Kuona
hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, Anna Abdallah alisimama na kuwataka
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waliopitisha sheria hiyo
kujilaumu kwa sababu walipaswa kuliangalia hilo.
Habari hii imeandikwa na Kizitto Noya, Habel Chidawali, Sharon Sauwa na Fidelis Butahe, Mwananchi.
No comments
Post a Comment