Writen by
sadataley
2:15 PM
-
0
Comments
Na Mussa Juma na Julius Mathias, Mwananchi
Dodoma/Dar. Suala la ama kutumia kura ya siri au ya wazi kuamua ibara za Rasimu ya Katiba jana liliuteka upya mjadala wa Kanuni za Bunge la Katiba, huku ikielezwa kuwa limewekwa kama mtego kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika kuwania urais.
Sitta ni mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kuwa katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao kupitia CCM, huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mahasimu wake kisiasa ndani ya chama hicho.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Godbless Lema alimtaka Sitta kuwa makini na maelekezo aliyodai mwenyekiti huyo anapewa katika uendeshaji wa Bunge na kudai pia kuwa, kuna kundi la watu wanaotaka urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 wanaotaka kumkwamisha.
Akichangia hoja ya mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni yaliyotaka kupitishwa mifumo miwili ya kura kwa wazi na siri, Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha alisema kwa mazingira ambayo yanaendelea, Sitta anapaswa kuwa makini na watu wanaompatia maelekezo wakitaka aonekane hafai baadaye.
“Ni vyema ukawa makini na mapendekezo unayoletewa kwa sababu hao wote pamoja na wanachama wa chama chako wanajua kama utaliongoza vizuri Bunge hili, basi unaweza ukapata tiketi ya kugombea urais 2015 ndani ya chama chako, lakini ukishindwa watakudhihaki kuwa umeshindwa, hivyo hutaweza kuliongoza taifa,” alisema Lema huku Sitta aliyeonekana awali akitabasamu, alibadilika na kumtazama mbunge huyo kwa umakini.
Lema alisema miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM na kamati nyingine za Bunge hilo, kuna watu ambao wanataka kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika mjadala huo, ilionekana wazi kuwa wajumbe bado wamegawanyika pande mbili – CCM wakionekana kuunga mkono kura ya wazi na upande wa upinzani wakipigia chapuo kura ya siri.
Miongoni mwa waliopigia debe kura ya siri ni John Mnyika aliyesema suala la upigaji kura ni la kikatiba ili kuhakikisha kila mjumbe anapiga kura yake bila kushurutishwa, kushinikizwa wala kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au chombo chochote.
Wajumbe hao walikuwa wanajadili mapendekezo yaliyowasilishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho, baada ya juzi kuzua mvutano uliosababisha Bunge hilo kuvunjika ili kusubiri maridhiano ya pande zinazopingana.
Mapendekezo ya Kanuni
Kificho alisema, mapendekezo hayo yamefikiwa kutokana na masharti ya kanuni ya 59 (1) na 87 (1) kwamba kanuni ya 38 (1) iweke utaratibu wa kupiga kura ama ya wazi au ya siri, ambao utatekelezwa na mwenyekiti kwa kushauriana na katibu.
Alisema wakati wa kupiga kura ya siri kila mjumbe atapiga kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’ kwa kutumia karatasi ya kupigia kura itakayokuwa imeandaliwa na katibu kwa ajili ya hilo.
Mjumbe Michael Laizer alisema wamechoshwa na malumbano juu ya kura za wazi au siri, hivyo iwapo kuna wajumbe ambao hawataki mapendekezo ya kamati waondoke.
Naye Ezekiel Olouch alisema utaratibu unaopendekezwa na kamati haujawahi kufanyika mahala popote duniani.
Alisema kura ya siri imekuwa ikitumika kuamua mambo ya msingi na kuepusha mpasuko katika jamii hasa katika masuala ambayo yanaweza kuligawa taifa.
Mohamed Raza alisema msimamo wake ni kupiga kura ya wazi kwani wengi wanajua msimamo wake ambao ametoka nao Zanzibar.
Joshua Nassari alisema anashangazwa kuona Taifa linarejeshwa katika karne ya 18 katika upigaji wa kura kwa kung’ang’ania kura ya wazi wakati wao wamechaguliwa kwa kura za siri.
“Mwenyekiti wewe tumekuchagua kwa siri wajumbe wote wamepatikana kwa siri, iweje leo kulazimisha kura ya wazi ili wajumbe wa CCM watakaopiga kura za siri wachukuliwe hatua,” alisema Nassari.
No comments
Post a Comment