Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, March 4, 2014

Mizigo ya DRC yafikia tani 1 mil

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.PICHA|MAKTABA 
Na Hadija Jumanne, Mwananchi
Dar es Salaam. Uingizaji wa mizigo kwa wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kupitia Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kutoka tani 176,000 mwaka 2004 hadi tani 1.17 milioni mwishoni wa mwaka 2013.
Mizigo hiyo ni ile inayotoka nchi mbalimbali na kupitia katika Bandari ya Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali nchini Kongo.
Hayo yalisemwa juzi jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe wakati akizindua Kamati ya Chama cha Wafanyabiashara wa Kongo (BCI) nchini Tanzania.
Dk Mwakyembe alisema katika kipindi cha mwaka jana pekee, shehena ya mzigo wa Kongo ilikuwa asilimia 23 ya mizigo ya nje ya nchi.
Kadhalika kuna asilimia 9 ya mzigo wote katika Bandari ya Dar es Salaam unaokwenda DRC.
“Kwa shehena hii, Kongo inashika nafasi ya pili baada ya Zambia kwa nchi jirani zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuingiza shehena ya mizigo,” alisema Dk Mwakyembe.
“Naamini iko siku nchi hii itashika nafasi ya kwanza kwa kusafirisha mizigo mingi kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema
Alisema Serikali inataendelea kuondoa vikwazo vinavyolalamikiwa katika bandari hiyo ikiwamo kuyafanyia kazi mapendekezo mbalimbali ya wadau.
Miongoni mwa mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuboresha huduma za bandari ni kupunguza vizuizi vya barabarani ili kujenga uhusiano zaidi na wafanyabiashara wa Kongo.
Kuhusu mizigo yao kuchelewa kuhamishwa kutoka sehemu ya kuhudumia makontena (TICTS,) Dk Mwakyembe alisema tayari suala hili linashughulikiwa katika kikao baina ya viongozi wa kitengo hicho na waziri kinachoendelea.
“Tutahakikisha tunashughulikia kwa haraka changamoto mbalimbali zinazoikabili bandari yetu ya Dar es Salaam,” alisema Mwakyembe na kuongeza: “Tutaongeza vitendea kazi pamoja na rasilimali watu ili kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa mizigo na kuongeza tija ya ufanisi katika bandari.”
Awali, Katibu Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kongo (BCI) Kapuya Robert alisema chama hicho kilisajiliwa nchini mwaka 2005 na kwamba hadi sasa kina wanachama 250.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment