Writen by
sadataley
4:54 PM
-
0
Comments
Moshi. Uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu la Katiba jana uliteka hisia za wakazi wengi wa mjini hapa, baada ya kuacha shughuli zao na kuamua kufuatilia kupitia televisheni.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa katika baa, migahawa na hoteli mbalimbali wananchi walionekana katika makundi wakifuatilia kwa karibu hotuba hiyo ya uwasilishwaji.
Hotuba hiyo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba ambaye awali ilipangiwa ratiba ya kuwasilishwa Jumatatu wiki hii kabla ya kushindikana.
Mbali na wananchi kufuatilia hotuba hiyo kupitia televisheni katika sehemu za starehe, baadhi ya viongozi walifuatilia hotuba hiyo wakiwa maofisini.
“Tangu saa 3:00 asubuhi niko kwenye TV (runinga). Sikutaka kuhadithiwa alichosema Mwenyekiti (Jaji Warioba) hasa kuhusu suala la Muungano,” alisema mfanyabiashara wa mitumba ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwenye gazeti.
Mfanyabiashara wa vifaa vya elektroniki, Hussein Mfinanga alisema somo alilolitoa Jaji Warioba ni kubwa na anaamini wajumbe wataweka mbele masilahi ya umma.
“Amefafanua vizuri sana kwa nini ni Serikali tatu na siyo mbili na namna Katiba ya Zanzibar inavyoleta mgogoro wa kisiasa,” alisema Mfinanga.
Mkazi wa Soweto, Manispaa ya Moshi, George Mberesero alisema wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kuweka mbele masilahi ya umma na waepuke kuingia katika mkumbo wa ushabiki wa kichama au makundi.
“Jaji Warioba ameweka wazi tafiti mbalimbali kuhusu suala la muungano, sasa tunachotaka ni hoja, siyo wajumbe kung’ang’ania misimamo isiyo na tija kwa wananchi,” alisema Mberesero.
Mmiliki wa Klabu ya Peter Club ya Majengo, Peter Kinabo alisema kwa ufafanuzi wa Jaji Warioba, muundo wa Serikali tatu hauepukiki kama Watanzania wanataka Muungano udumu.
Mfanyabiashara huyo aliitaka CCM yenye wajumbe wengi ndani ya Bunge hilo, kutambua kuwa siku zote katiba inayopatikana kwa ubabe wa wengi haiwezi kupita kwenye kura ya maoni.
No comments
Post a Comment