Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Sunday, March 16, 2014

HOTUBA YA RAIS KIKWETE KWENYE UZINDUZI WA MVIMAUTA BCIC MBEZI BEACH


Rais Jakaya Kikwete katika picha ya pamoja na Askofu Sylvester Gamanywa, mkewe, pamoja na viongizi wengine mbalimbali baada ya kuzindua sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania, MVIMAUTA. ©WAPO FM
Hivi karibuni, sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania, MVIMAUTA - ilizinduliwana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dakta Jakaya Kikwete, (picha za tukio hilo ziko hapa.)Baada ya kusikiliza upande wa mbeba maono, Askofu Sylvester Gamanywa, Rais Kikwete alieleza yafuatayo; hotuba kamili imenukuliwa.


Mheshimiwa Baba Askofu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa kitaifa wa WAPO Mission International na Mwasisi wa maono ya harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya, Mheshimiwa Askofu Michael Peter Imani, Mwangalizi wa makanisa ya WAPO Mission International Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, waheshimiwa maaskofu, wachungaji, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya, wageni waalikwa wenzangu, waumini, mabibi na mabwana.

Nakushukuru sana Baba Askofu Mkuu Gamanywa na viongozi wenzako wa WAPO Mission International kwa kunialika na kunishirikisha katika tukio hili la kihistoria la kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA).
Nakushukuru kwa risala ambayo umeelezea kwa ufasaha malengo na madhumuni ya MVIMAUTA kwa jinsi mlivyojipanga kuyatekeleza na nini mnachotegemea Serikali ifanye kusaidia utekelezaji wake.

Napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa dhati kwa ubunifu wako na kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya wewe na kanisa lako ya kulea vijana wawe raia wema, vijana wawe wana manufaa kwa familia zao, jamii zao na Taifa kwa ujumla.

Hii ni mara yangu ya pili kushuhudia matunda ya ubunifu wako na kazi njema inayofanywa na WAPO Mission International, mara ya kwanza ni mwaka 2010 uliponishirikisha katika uzinduzi wa mpango wa kizazi kipya Tanzania. Matokeo ya mpango ule ni kuanzishwa kwa mkakati huu ambao ni Mtandao wa Vikundi vya Maadili ya Uchumi Tanzania ambao sera yake ndiyo tunaizindua leo.
Nasema Baba Askofu hongera sana, viongozi wenzako na waumini hongera sana, nakuamini sana, nakuthamini sana, nakupenda sana kwa kazi yako nzuri unayoifanya. Changamoto unazozipata ni sehemu ya changamoto za maisha. Sisi wengine hapa tuna changamoto lukuki. Lakini lililo muhimu ni kwamba je hili unalokusudia kulifanya ni jema? Kama unaamini kwamba ni jema; fanya. Wanaokuona huna maana leo watakupongeza kesho.

Baba Askofu napata faraja kubwa kuona kuwa mpango huu sasa umewekewa mkakati madhubuti, mkakati thabiti wa utekelezaji ili malengo yake yaweze kufikiwa. Sote tumekusikia ukieleza kwa ufasaha maudhui ya sera na mikakati ya utekelezaji wake. Ni ukweli ulio wazi kuwa ni sera nzuri na hakuna mpenda maendeleo wa kweli anayeweza kubeza au kukataa kuwaunga mkono. Jambo mnalokusudia kufanya ni jema sana kwa nchi yetu, ni jambo lenye manufaa kwa vijana ambao ndio taifa la leo na kesho. Mnalenga kusaidia kundi muhimu, kundi linalotegemewa na familia, linalotegemewa na jamii, linalotegemewa na nchi yetu kwa ujumla. Kundi ambalo bahati mbaya linakabiliwa na changamoto nyingi za kimaadili na kimaisha. Lakini changamoto ni fursa ya aina yake kwa mwanadamu. Kiingereza wanasema: “ Challenges are opportunities”. 

Changamoto fursa yake ya kwanza ni kwamba inampanua mawazo mwanadamu. Kwamba pale unapokabiliwa na tatizo, unapohangaika kutafuta majawabu, mawazo yako yanapanuka. Kuna vitu vingi unavyovifikiria na katika kufikiria vitu vile kuna ubunifu unaotokea ndani yake, kuna ufumbuzi unaotokea ndani yake. Kwa hiyo fursa ya kwanza ya mwanadamu anapopata changamoto anapata fursa ya ubongo wake kupanuka. La pili changamoto huwafanya wanadamu kuwa wabunifu katika kutafuta majawabu. 

Baba Askofu, na WAPO Mission International mmefanya kile kinachostahili kufanywa, mmetambua changamoto, mmechuna bongo zenu, mmekuwa wabunifu kutafuta jawabu la changamoto zinazowakabili vijana wetu. Mmetimiza vyema jukumu lenu kama wazazi, kama sehemu ya familia na hasa kama viongozi wa dini, ambao mkiwa viongozi wa dini mnayo majukumu mawili katika kuwachunga wanakondoo na majukumu ya kiroho lakini pia muwaongoze wanakondoo wenu hawa waweze kuishi maisha mema.

Sura moja ni kuwapatia vijana wetu malezi mema ili waweze kukabili na kushinda changamoto za kimaadili. Najua ni kazi ngumu hasa katika dunia ya leo ya utandawazi, dunia inayosukumwa na kuongozwa na teknolojia ya kisasa, teknolojia ya kisasa ya habari na mawasiliano. Television, computer, Internet, mablog, mitandao mbalimbali inachukua nafasi kubwa sana katika kuongoza mawazo ya vijana na wakati mwingine inawapa vijana tafsiri isiyokuwepo. Wakiwaona watu kwenye sinema wanapanda magari mazuri, wanavyoishi kwenye nyumba nzuri, ni kweli wanaona ndiyo maisha,watamani waishi hivyo. Lakini sasa akigeuza kwamba jambo lile ni lazima alipate kesho, wanasahau kujua kwamba hata wale wanaocheza sinema wakitoka pale wanarudi Magomeni, wanarudi Tandale, Manzese, Kinondoni, ndipo wanapoishi. Lakini kwenye sinema unamuona anaendesha gari BMW safi, anatanua kwenye jumba la ghorofa makochi mazuri. Ni ya sinema tu yale. Kwa hiyo hayo ndiyo maisha unachokiona pale kwenye zile sinema, ukifungua kwenye internet unayoyaona mle ndani mengine hata huwezi ukaangalia kwa dakika mbili kama imani imekushiba, lakini kama imani haikukushiba ndiyo unaendelea kufurahia, na ndiyo unaishia kuharibikiwa baada ya hapo unayaona yale ndiyo yenyewe, ukija hapa Bwana asifiwe sana, ameni, ameni, lakini ukitoka hapa unarudi kwenye mitandao. Hiyo ndiyo mitihani lakini katika mazingira haya mtu kubaki na imani yake ni jambo kubwa sana. Aliyeshinda vishawishi vyote hivyo akabaki na msimamo thabiti wa kumwabudu Mwenyezi Mungu, wa kumuenzi Mwenyezi Mungu wa kufuata mafundisho yake na hasa kuzingatia makatazo yake ni jambo la ushindi mkubwa.

Lakini hatunabudi kufanya kazi hiyo, tena tuifanye kwa umahiri mkubwa ili tushinde kwa sababu tukishindwa tutakuwa tumepata hasara kubwa, tutakuwa na vijana wasiokuwa waadilifu, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo na ustawi wao, familia zao, jamii zao na taifa letu. Na sisi lazima tuwe wabunifu, tutumie utandawazi huo huo, teknolojia ya kisasa hiyo hiyo, kupenyeza neno kuwajengea vijana wetu imani ili wawe waadilifu na waweze kuwa na maadili mema. Mwiba unatokea palepale ulipochoma, kama wanatumia mitandao hiyo kupunguza maadili ya vijana wetu, sisi tuitumie mitandao na teknolojia hiyo kinyume chake kufanya kile cha kujenga maadili ya vijana wetu.

Natoa pongezi nyingi kwa WAPO Mission International kwa jitihada mnazozifanya kufanikisha jambo hili, la msingi sana. WAPO Radio inafanya na endeleeni kutafuta vyanzo mbalimbali na hata mkianzisha mitandao iwe ya watu wanaobadilishana mambo mema ili yule aliyechoshwa na mitandao inayozungumza mambo mabaya kila wakati, anakwenda kwenye mitandao na anachart na wenzake lakini wanawasiliana juu ya Neno la Mungu na maadili mema. Ni kitu kinachowezekana tafadhali fanyeni. Dumisheni msimamo wenu, endelezeni jitihada mnazozifanya mtafanikiwa. Penye nia pana njia, kwa Mungu Hakuna lisilowezekana. Baba Askofu Mungu ni mwema, atawabariki, atawashindia kwa kazi njema na nia njema mliyonayo.

Mhe. Baba Askofu, waheshimiwa maaskofu na waumini na wageni waalikwa wenzangu sote tumekusikia ukieleza kwa ufasaha kwenye risala shabaha za sera ya Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania na jinsi mnavyokusudia na mlivyojipanga kuzitekeleza. Lazima nikiri kwamba nimetiwa moyo sana na mambo mazuri mliyokusudia kufanya. Nina imani kuwa kwa kufanya haya mtafanikiwa katika dhamira yenu hii, baadhi ya changamoto kubwa zinazowakabili vijana wengi nchini zitakuwa zimepata muharobaini.

Mambo mengi mazuri umeyaeleza Baba Askofu sina sababu ya kuyarudia. Naomba niyasemee mawili matatu, kwanza nawapongeza sana kwa uamuzi na hatua mliyofikia kuanzisha mchakato wa kusajili Chuo Kikuu cha Uongozi wa Kimaadili na Taasisi ya Kukuza Vipaji. Nawaombea mafanikio katika kukamilisha mapema usajili wa taasisi hizi za aina yake ili vijana wetu waweze kupata manufaa yake. Mmeeleza changamoto mbalimbali na mimi nimesikia, pale ninapoweza kusaidia nitawasaidieni.

Kuhusu maombi yenu ya ardhi kwa shughuli kubwa ile ya kilimo, ninachoshauri tu ni kwamba, pelekeni maombi kwenye mamlaka zinazohusika naamini mtafanikiwa. Nchi yetu ina ardhi ya kutosha ya kuwawezesha kujenga na kuyatekeleza yale mnayoyafanya. Kujenga hizi taasisi na kutekeleza shughuli zenu za kilimo. Lakini ardhi hiyo ina wenyewe wanaoimiliki ama ni wananchi mmoja mmoja au familia zao au serikali za vijiji au halmashauri za wilaya na miji. Kuna baadhi ya maeneo yako kwenye mamlaka ya Serikali Kuu. Serikali yenyewe ilivyo haina ardhi inayomiliki labda kuwe kuna shamba lilitaifishwa hakuna, shughuli zinazoendelea pale ndiyo unakuta kwamba hilo linamilikiwa na Serikali.

Ni kweli Katiba inasema ardhi yote ya nchi hii ni mali ya Rais, lakini hana haki ya kumiliki hata kipande kimoja. Ila imempa fursa ya kuwa mdhamini wa ardhi ya nchi yetu kwa niaba ya wananchi wote. Kwa sababu hiyo inampa Rais fursa ya kutwaa ardhi ya mtu yeyote, wakati wowote, bora tu kutwaa huko kuwe ni kwa ajili ya shughuli za kitaifa, jambo lenye manufaa kwa Taifa. Tunataka kujenga barabara na barabara ile lazima ipite kwenye ardhi ya Bwana Sadick, kuna nyumba, kuna mgahawa, wakati mwingine kuna baa. Sasa ardhi ile lazima ipatikane ili barabara ile ijengwe. Rais amepewa mamlaka hayo ya kuitangaza adhi ile imetwaliwa kwa manufaa ya Taifa ili ifanye ile kazi inayokusudiwa kwa manufaa ya Taifa.

“Katika mazingira mengine kama ardhi mnayoitafuta iko kwenye mazingira ya uwezo wa Serikali niambieni nitawasaidia”, ardhi iliyoko kwenye mikono ya mtu binafsi na familia hapo lazima mzungumze na mhusika muelewane naye na ushauri wangu ni kwamba msitumie mawakala, ila mkizungumza na wahusika wa ardhi moja kwa moja mtanufaika sana lakini mkitumia mawakala mtauziwa ardhi hiyo kwa bei kubwa.

Baba Askofu Mkuu, nimefurahi sana kusikia miongoni mwa shughuli za kipaumbele kwenye vikundi vyetu hivi ni kilimo. Ni ukweli ulio wazi ndugu zangu kuwa kilimo kinatoa fursa kubwa sana ya ajira kwa vijana kuliko sekta nyingine yoyote hapa nchini. Bahati mbaya sana kilimo hakivutii watu wengi na hasa vijana na sababu kubwa ni kwamba kuna matumizi madogo sana ya teknolojia za kisasa zinazofanya kazi za kilimo kuwa rahisi na wakati huo kuwa na tija kubwa. Kilimo chetu kimekuwa ni kazi ya mitulinga, jasho jingi kwa kutegemea jembe la mkono au plau ya kukokotwa na ng’ombe. Jembe la mkono mtu hawezi kulima shamba kubwa, kwa kutumia ng’ombe nayo unaweza ukalima shamba kubwa lakini hiyo siyo kazi nyepesi ni ngumu.

Kijana msomi anapofikiria diploma zake, shahada zake akutwe pale ameshika jembe la mkono au plau anaona havifanani naye. Kwa hiyo ni kazi inayofukuza sana vijana. Lakini kijana yule ukampa trekta, au kijana yule ukamuwezesha kukodi trekta lilime, na siku hizi kuna trekta linalolima, kuna trekta linalofua kuna trekta linalopanda. Kuna dawa zinazoua magugu kwa hiyo hakuna haja ya kupalilia. Si lazima kila mtu awe na la kwake, lakini mkimuwezesha akapata fedha ya mkopo akamlipa mwenye trekta akafanya hizo kazi, unakuwa umemrahisishia na kazi ya kilimo hapo inaweza kuwa ya mvuto zaidi kwa vijana.

Kilimo kina tija ndogo, kwamba ile nguvu mtu anayoiweka,na mavuno anayoyapata hayafanani na jasho alilolitumia pale shambani, kwanza kuna changamoto ya kutegemea mvua za Mwenyezi Mungu katika maeneo mengi nchini ambazo ambao si za kuaminika siku hizi kwa sababu tunamuudhi sana Mungu, basi na wakati mwingine anatuadhibu tu na mvua haleti na hata akileta zinakuwa za mafuriko. Kwa hiyo kilimo cha kutegemea mvua za Mwenyezi Mungu ni kilimo kinachopunguza tija na ndiyo maana jawabu lake ni kilimo cha umwagiliaji, ambapo kwa maelezo ya Baba Askofu ndiyo shabaha ya mpango wenu huu katika kujihusisha kwenye kilimo mmefanya uamuzi sahihi. Lakini tija kwenye kilimo pia inategemea aina ya mbegu unazozipanda shambani kwako. Kuna mbegu zinazozaa sana na mbegu zinazozaa kidogo. Mbegu zetu za asili zinazaa kidogo. Mbegu za kisasa zinazotokana na kazi walizofanya wanasayansi kwenye vituo vya utafiti mavuno ni makubwa. Mwenzako akalima heka moja na wewe ukalima heka, wewe ukapanda mbegu za Kikwere na mwenzio kwa heka moja aliyepanda mbegu za kisasa, atavuna mara kumi zaidi yako. Tija yetu ni ndogo kwa sababu matumizi yetu ya mbolea kisayansi ni madogo sana kwenye kilimo. Kilimo cha kisasa wanasayansi wana utafiti wa mbegu zinazozaa sana, mbegu zinazohimili maradhi, na mazingira yenye matatizo mbalimbali ya hali ya hewa. Tambueni kuwa siyo kila ardhi ina virutubisho vyote vinavyotakiwa na mimea.

Kwa hiyo matumizi ya mbolea ni muhimu sana. Kwa hiyo kubadili kilimo chetu ndiyo malengo na madhumuni ya mpango wetu wa maendeleo ya kilimo tuliyouzindua mwaka 2006. Kuongeza matumizi ya trekta, matumizi ya kilimo cha umwagiliaji, kuongeza upatikanaji na matumizi ya mbegu bora, mbolea na dawa, kuongeza maafisa ugani ili wawafundishe wakulima kilimo cha kisasa ndiyo mambo ya msingi tuliyokuwa tunaendelea nayo hadi sasa na tumepata mafanikio lakini kasi yake hairidhishi. Tukaongeza pesa kwenye programu ya ruzuku ya mbegu, mbolea na dawa ili wakulima waweze kupata, nimekuwa tukiagiza matrekta kupitia Suma Jkt, matrekta makubwa na madogo kwa sababu ukiingia kwenye kilimo cha bustani trekta kubwa halifanyi kazi sana na powertiller linafanya kazi vizuri kwenye vishamba vidogo vya mboga na matunda. Kwa hiyo Baba Askofu, ninachoweza kusema kwamba likazanieni sana hilo. Mmefanya uamuzi sahihi, uamuzi mzuri, hili jambo la kilimo kufanya na vikundi vyenu likazanieni na sisi katika Serikali tutaendelea kushirikiana nanyi kufanikisha malengo hayo.

Ila pia mchague kilimo cha namna gani, mnataka kulima nini, mimi nitawashauri hivi, limeni mbogo na matunda. Sisemi kwamba mpunga na mahindi ni jambo baya, hata kidogo, mapato makubwa yako kwenye mboga na matunda. Heka moja utakayopanda mananasi kazi yake ni kubwa kidogo, lakini ukipanda mananasi elfu 22, ni miezi 18 yale mananasi yatakuwa yameiva.

Kwa hiyo mimi ninachosema tu kwamba nawapongeza sana, ninawaahidi kwamba katika programu mbalimbali tulizokuwa nazo sisi za kuendeleza kilimo kwenye maeneo yale mtakayokuwa mnaendesha programu hizi kuna misaada mnayoweza mkaipata kwenye maeneo yale kama ile tunayotoa kwa wakulima kwenye maeneo yale na siyo kwamba tutakuwa tumeipendelea WAPO kwa sababu Askofu Gamanywa ni rafiki yetu, tunamjua, hata kidogo, hiyo ni kwa sababu zipo programu kule zinazoendelea sasa hivi za ruzuku kwa wakulima na mbegu, mbolea, na madawa, mikopo kwa vikundi na matrekta, mnaweza kutumia fursa hizo. Ni eneo ambalo mmefanya uamuzi kwa wakati muafaka kushirikiana vizuri itasaidia sana. Mkurugenzi wa vijana yupo hapa akishirikiana na vijana wenzake vizuri tutafika. Wako vijana wa vyuo vikuu ambao tayari wamekwishajiunga kwenye kilimo, wengine baada ya kupata manufaa hata wakitangaziwa kwamba sasa umepata kazi hawaende kwa sababu akilinganisha mshahara anaoenda kuupata akilinganisha na mamilioni anayoweza kuyapata katika kilimo cha mboga haendi. Wapo hao mifano yake itumieni, mimi nitawasaidieni kuwatambulisheni na baadhi watumieni wawasimulie jinsi maisha yao yalivyo mazuri huko vijijini na yanaleta matumaini na kilimo kinalipa.

Kwa wale kwa siku za usoni watakaoweza kujishughulisha na shughuli za viwanda, maana hata hata kwenye hiki kilimo mtafika mahali mnataka kuongeza thamani, badala ya mananasi mtataka kuuza juice ya mananasi, au juice ya machungwa na hapo WAPO Cooperative itakuwa na viwanda vyake vya kutengeneza juice inauza kama anavyouza Bakhresa. Ni vitu vinavyowezekana, mwanzoni mnaweza kuanza kitu kidogo lakini jinsi mnavyoendelea mnaweza mkakijenga kikawa kitu kikubwa sana.

Wale mtakaokuwa mmefikia hatua hiyo nitafikisha ujumbe kwa watu wa SIDO, na Baba Askofu nenda ukaonane nao watawashauri namna ya kufanya shughuli hizo za kuongeza thamani mazao hayo kwa hiyo suala kubwa litakuwa ni mtaji na Serikali tutaona namna ya kukusaidieni kwani jungu kuu halikosi ukoko. Mkijipanga vizuri na ikathibitika kwamba mna mradi mzuri tutawasaidieni tu hata kama siyo sisi tutawasaidieni kusema kwamba wasaidieni vijana na sisi Serikali mchango wetu ni huu.

Kwa sasa Serikali inashughulikia na kuanzisha benki ya wakulima, tupo kwenye hatua nzuri, itakapoanza itatoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja kwa wakulima na hasa italenga sana vikundi na mimi ninaamini na ninyi mtakuwa miongoni mwa wanafaikaji wakubwa wa benki hiyo.

Baba Askofu Mkuu natoa wito kwa mashirika na taasisi zetu mbalimbali nao waangalie jinsi ya kusaidia juhudi kama hizi kwa sababu vijana wetu wanapata ajira na wakipata shughuli za kuendeleza maisha yao. National housing na Veta wanafanya vizuri kwa kuwasaidia vijana.

Napenda kurudia kuwapongeza kuanzia Baba Askofu, na viongozi wenzako kwa jambo hili jema mliloamua kufanya leo, lakini nyinyi ni sifa yenu ya miaka mingi kwa sababu Baba Askofu Gamanywa tunamjua ni mbunifu na ana maono mapana, maono ya mbali kwa hiyo hatushangai.
Ninachotaka kuahidi kuwa ni kwamba Serikali itajitahidi kufanya yale inayotakiwa kufanya ili sera hii mnayoizindua leo ifikie malengo yake.

Mwisho kabisa nawashukuru tena kwa kunialika,nawapongeza wale wote walioshiriki kuandaa na kufanikisha shughuli hii ya leo. Wamefanya kazi nzuri, kazi iliyotukuka. Nawapongeza waumini na hasa vijana kwa kufika kwa wingi, nyinyi ndiyo walengwa, bila ya nyinyi kuwepo hakuna MVIMAUTA. Ushiriki wenu ndiyo kufanikisha shughuli hii. Naomba sote tuendelee kumuunga mkono Baba Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, tuendelee kumtia moyo azidi kufanya mambo mengi mengine mazuri katika kuwatumikia ninyi waumini wa kanisa lake lakini pia katika kuwatumikia Watanzania wote.

Baba Askofu tunatambua na kuthamini sana kazi njema unazozifanya, tunawaomba muendelee kuliombea Taifa letu liendelee kuwa na amani, liendelee kuwa na utulivu, watu wake waendelee kupendana licha ya tofauti mbalimbali tulizonazo ili katika hatima ya yote tuweze kupata mafanikio.

Baada ya kusema maneno hayo, Baba Askofu sasa niko tayari kuifanya kazi ya kuizindua sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment