Writen by
sadataley
1:30 PM
-
0
Comments
Na Phinias Bashaya,Mwananchi
Bukoba. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amemtaka Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk Anatory Amani kuachia ngazi baada ya Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kubaini ubadhilifu katika miradi ya halmashauri hiyo na ukiukwaji wa taratibu za kusaini mikataba.
Akisoma maelezo ya Serikali kutoka kwa waziri mkuu baada ya mkaguzi mkuu kuwasilisha taarifa yake,Naibu Waziri wa Tamisemi Agrey Mwanri alisema jana kuwa, maelekezo ya Serikali kutoka kwa Waziri Mkuu yanawataka madiwani kumuwajibisha ikiwa atakataa kujiuzulu.
Kwa mujibu wa maleezo hayo yaliyosomwa kwa niaba ya waziri mkuu, ameagiza aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Hamis Kaputa ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya kuvuliwa madaraka, akiwamo Mhandisi wa Manispaa,Stephen Mzihirwa na wakuu wengine wa vitengo na idara. Ripoti hiyo ilipelekwa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya taarifa ya CAG kugundua kuwapo kwa makosa mbalimbali ya jinai na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi na uingiaji wa mikataba.
Baada ya taarifa hiyo, Meya Dk Anatory Amani alisema, anakubaliana na maagizo ya Serikali na Naibu Meya, Alexander Ngalinda alikabidhiwa maelekezo hayo na kuahidi vikao vya madiwani vitaanza mara moja baada ya kususiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Akisoma matokeo ya ukaguzi huo maalumu, Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh pamoja na kubainisha upungufu na harufu ya rushwa katika miradi mbalimbali pia amebatilisha uteuzi uliofanywa na Waziri wa Maji kwa kumteua Mulungi Kichwabuta ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu (CCM) kuingia katika Bodi ya Maji bila taratibu za kisheria.
Kwa mujibu wa Utouh, waziri huyo wa maji ambaye hakumtaja jina alikiuka sheria kwa kupendekeza jina ambalo halikupitia katika mapendekezo ya vikao vya mkoa ambapo mkoa ulikuwa umependekeza jina la Ashura Hassan viti maalumu CCM.
Katika ripoti hiyo iliyosomwa mbele ya madiwani na viongozi mbalimbali wa mkoa,CAG alisema Meya wa Manispaa hiyo, Dk Anatory Amani aliingia makubaliano ya ujenzi wa soko bila madiwani kushirikishwa huku ripoti ikibaini ukiukwaji wa taratibu katika uwekezaji wa kituo cha kuosha magari.
Aidha kwa mujibu wa ripoti hiyo kuna uwekezaji wenye utata kati ya Manispaa ya Bukoba na Benki ya Uwekezaji( UTT)katika upimaji wa viwanja 5,000 na kuwa baadhi ya kampuni zilizopewa mikataba hazikuwa na usajili na hazina utambulisho wa mlipa kodi.
Pia CAG amemtaka Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Hamisi Kagasheki kukabidhi gari lililosajiliwa kwa namba za Serikali za mitaa kwa manispaa alilodai alilinunua kusaidia wananchi au alisajili kwa namba binafsi na kulipa kodi.
Ripoti hiyo ilisema madai ya Meya Dk Anatory Amani kuhamisha mradi wa maji kutoka Kata ya Nyanga kwenda kwenye Kata yake ya Kagondo hayakuwa na ukweli kwa kuwa taratibu zilifuatwa ikiwa ni pamoja na mchango wa wananchi.
Baada ya ripoti hiyo askari polisi walilazimika kuimarisha ulinzi kufuatia taarifa kuwa wananchi wanaodaiwa kuunga mkono makundi yaliyokuwa yanavutana kuzingira maeneo ya ofisi za mkuu wa mkoa wa Kagera na wengine kulipuka kwa shangwe.
Tuhuma za ubadhilifu katika utekelezaji wa miradi ya Manispaa ya Bukoba ziliibuliwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Balozi Hamisi Kagasheki katika mkutano wa hadhara kauli iliyoleta mvutano na hata kuibuka mgogoro uliokosa usuluhishi katika vikao vya chama katika ngazi tofauti.
No comments
Post a Comment