Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, October 18, 2013

Vyama vinaogopa nini hesabu kukaguliwa?

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi PICHA|MAKTABA 
Tumesikitishwa na hatua ya viongozi wa vyama vya siasa kumshambulia kwa maneno makali Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutokana na kauli yake kwamba angewasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa ili ruzuku ya vyama hivyo isitishwe hadi hapo vitakapowasilisha taarifa za ukaguzi wa matumizi ya vyama hivyo kama sheria inavyotaka.
Zitto alisema juzi kuwa, tangu mwaka 2009 Serikali ilitoa kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa vyama tisa vya siasa, lakini vyama hivyo havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu zake. Tunasema kauli hiyo ya Zitto ni nzito na haipaswi kupuuzwa. Serikali inapaswa kuifanyia kazi haraka pamoja na kwamba viongozi wengi wa vyama hivyo wanazungumzia suala hilo kwa mitazamo ya kisiasa na kiitikadi.
Kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2009, vyama vya siasa vinawajibika kuwasilisha hesabu zake kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambaye ofisi yake inaweza kuzifanyia ukaguzi yenyewe au kuteua mkaguzi anayeaminika. Itakumbukwa kwamba CAG, Ludovick Utouh aliwahi kuhadharisha kwamba utaratibu unaotumiwa na vyama hivyo wa kuteua kampuni binafsi kufanya kazi hiyo siyo sahihi na ni kinyume cha sheria.
Sisi hatutaki kuingia katika malumbano hayo ya Zitto na vyama vya siasa, kwani hatuoni kama yana tija kwa walipakodi ambao kodi zao ndizo zinazoendesha shughuli za vyama hivyo kwa njia ya ruzuku. Kwa msingi huo, yatakuwa makosa makubwa iwapo waliopewa dhima ya kutunza na kuratibu matumizi ya fedha hizo wataachwa kuzitafuna kama mchwa.
Lazima matumizi ya fedha hizo yadhibitiwe na kukaguliwa ili kama kuna ubadhirifu wahusika wawajibishwe, ikiwa ni pamoja na kusitisha ruzuku kwa vyama husika.
Mpaka sasa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo, pengine katika kujaribu kujinasua wanaonekana kutoa matamshi yenye matege, kwa maana ya kutojitetea kwa hoja na badala yake kutoa kauli tete zisizoacha shaka kwamba hakika ruzuku kwa vyama vyao zinatumiwa visivyo.
Kwa mfano, siyo sahihi kusema siyo jukumu la vyama kulipa gharama za ukaguzi wa hesabu za vyama hivyo, wakati fedha hizo zinatokana na ruzuku zinazotolewa kwa vyama hivyo. Pia, ni kichekesho pale chama kongwe kinapodai kwamba hesabu zake zimekuwa zikikaguliwa na kampuni moja pekee tangu mwaka 1977.
Mamlaka gani yenye heshima duniani itazikubali hesabu za chama hicho? Inawezekana kabisa kwamba Kamati ya PAC ambayo Zitto anaongoza haina taarifa kamili kuhusu taarifa zote za ukaguzi wa hesabu katika baadhi ya vyama.
Hiyo siyo kasoro au udhaifu wa PAC, bali ni upungufu katika mfumo mzima wa Serikali ambao unaendeleza usiri na urasimu na kushindwa kusambaza taarifa kamili na kwa wakati katika mamlaka zote husika.
Pia, bado kuna mkanganyiko katika sheria tuliyoitaja, kwa maana ya utaratibu wa kuwasilisha hesabu za vyama kutoeleweka vizuri kama ziwasilishwe kwa Msajili au CAG.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameahidi hatasitisha ruzuku za vyama husika pasipo kuvipa fursa ya kujieleza. Ni matumaini yetu kwamba hatasita kuchukua hatua kali kwa viongozi wa chama chochote pale atakaporidhika kwamba wanafuja fedha mithili ya mabaharia walevi.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment