Writen by
sadataley
12:50 PM
-
0
Comments
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
Dar es Salaam. Oktoba 14 ya kila mwaka imetengwa katika Tanzania kuwa siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Katika kukumbuka siku hiyo Mwandishi Wetu, Exuper Kachenje amefanya mahojiano na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mwaka wa Mwalimu Nyerere kwa miaka mingi, ambapo anaeleza mambo mbalimbali kuhusu miaka 14 ya Tanzania bila kuwepo kwa kiongozi huyo.
Swali: Kwa miaka 14 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, amefariki dunia, ukiwa mmoja wa watu waliokuwa karibu naye, ukiwa Katibu Myeka wake, Je, unahisi kukosa nini kutoka kwake?
Jibu: We, akitutoka baba yako inakuwaje? Akiondoka, kama binadamu unakosa mtu mwenye ubinadamu, aliyekuwa kiongozi wako na wewe msaidizi wake, unamkosa.
Kwangu, Nyerere alikuwa baba, mwalimu na Baba wa Taifa. Tungefurahi kama angeendelea kuwa nasi leo hata kama angekuwa kikongwe kiasi gani au hana meno;
Ninakosa staili yake ya utendaji, uwezo wa kufikiri, kutenda, kueleza mambo kwa ufasaha na usahihi wa kiwango kikubwa. Hivyo, tunakosa mawazo ya msingi kama kuheshimu utu wa watu wote na usawa wa watu.
Swali: Binafsi umechota nini kutoka kwake na unakitumiaje?
Jibu: Nimechota uadilifu, ukweli, heshima kwa watu wote, kujali watu na kujitahidi kuwa mtu kwa watu wengine. Mwalimu alikuwa ‘role model’ (mtu wa mfano) wangu. Kitu ambacho sikuweza kuchota kutoka kwake, ni imani yake katika utu na usawa kwa wote, niliona imani hiyo na iliendana na imani yake katika kumcha Mungu na jitihada zake kuhudumia watu kadri ya imani yake ya Kikristo.
Mwalimu alikuwa mtu mwenye kuona mbali, alipenda umoja, amani kubwa na ndogo, mwadilifu, mtu maalumu aliyetumia muda wake wote kutumikia watu wengine.
Tunaweza kusema, sisi tunajitahidi kufuata yake, lakini hatujamfikia bado tuna upungufu.
Swali: Unapozungumzia upungufu, unaitazamaje Tanzania ya leo ukiwianisha na mambo aliyoasisi?
Jibu: Yapo mengi mazuri yaliyoendelezwa na sisi tuliobaki na viongozi wetu, moja ni Utanzania umeendelezwa. Tumedumu kama Watanzania tukiwa wamoja na ukisikiliza Watanzania hao wanapenda taifa lao, wanapenda umoja wao, wanapenda amani yao, wanataka uhuru wao, wanapenda mali zao zikubalike na zitambuliwe kuwa zao.
Wanapenda viongozi wao wajue kwamba ni viongozi wa watu na wajali wananchi, lakini hatujawa na viwango vya kukosa amani na kuyumbisha nchi yetu.Yapo mambo ya kawaida ya maendeleo, ukitembea nchini utakutana nayo, kwa mfano miundombinu. Mapenzi yetu kwa elimu yamekuwa makubwa, ongezeko la huduma lipo hata huduma za umma zimepanuka kwa karibu kila kitu, ila tunaendelea kubishana juu ya ubora.
Bahati mbaya tumekumbwa na tatizo la rushwa, kasoro nyingine ambazo hatukuwa nazo ni dawa za kulevya, tunaanza kwenda huko Umoja wa Mataifa (UN) au popote Watanzania tunajulikana kama watu wa mabange (bangi) tu, hii inatuondolea sifa.
Halafu, nadhani tumeongeza viwango vya ubinafsi hasa katika ngazi za uongozi. Viwango vya ubinafsi ni vikubwa. Ubinafsi hauzuiliki, ndiyo maana ya utu unaainisha mimi ni nani au wewe ni nani, lakini viwango vyake nadhani vimeongezeka. Vimezidi hasa katika ngazi ya uongozi na vinatuletea matatizo.
Uwezo wa viongozi unapungua, wanakosa uadilifu, mwelekeo wao wa kuhudumia taifa unapungua hata katika utumishi wa Serikali. Tatizo hili pia ni kubwa.
Sasa tuige misingi yetu ya maadili na miko, ipo inajulikana tatizo ni kutenda, tujitahidi sasa.
Swali: Kisiasa, Tanzania bila Mwalimu Nyerere unaitazamaje leo, mwelekeo wake ukoje?
Jibu: Ina mwelekeo mzuri, kwa sababu imetumia misingi yake ya umoja na mshikamano kutafsiri hali halisi na kukubaliana kwamba miaka ijayo inahitaji tuwe na Katiba Mpya na sasa hivi Watanzania wanafanya jambo kubwa, wanazungumza hatima yao lakini wakijadili sheria mama itakayowasaidia katika kufaulu au kutofaulu katika hiyo hatima hiyo wanayotaka katika mustakabali wa taifa lao.
Swali: Umezungumzia hatima ya taifa, Mwalimu aliuasisi muungano, akaonya kuhusu kuuchezea, unadhani leo angekuwepo angesemaje?
Jibu: Kabla hajafariki, Mwalimu alizungumzia nyufa mbalimbali za muungano, ametoka akituonya kwamba anaona dalili za kukejeli au kushindwa kuendeleza juhudi za kuimarisha muungano. Nafikiri alikuwa akiwasema zaidi Wazanzibari, aliona kama wao wanataka kuvunja muungano.
Alisema yoyote anayemkataa mwenzake, anatenda dhambi ya msingi. Alitoa mfano kuwa ukianza dhambi hiyo ni sawa na kula nyama ya mtu, huwezi kuacha.
Angekuwepo leo nadhani angesema tunajadili muungano wa Tanzania, lakini unaoonekana siyo mjadala wa kuimarisha muungano. Ni mjadala ambao watu wengi wanasema muungano unaanza kushindwa. Mwalimu angeendelea kutusihi tusishindwe kuulinda muungano.
Siyo kwamba muungano ukishindwa utasambaratisha Bara na Zanzibar pekee, bali utasambaratisha Zanzibar na Pemba, Upemba na Uunguja, huku bara utasambaratisha makundi mbalimbali Wasukuma, Wanyamwezi, Wachagga.Swali: Nini msimamo wako kuhusu muungano?
Jibu: Msimamo wangu napenda uendelee kuwepo, uimarishwe na udumu, faida zake ni kubwa zaidi kuliko hasara, wala siyo hasara ni changamoto ndogo ndogo. Leo, mataifa makubwa kama Marekani na Uingereza yanatafuta kuungana kuwa makundi makubwa zaidi, sisi ni nani wa kushindwa kuulinda muungano, ka umoja kadogo haka?
Swali: Unafikiri leo Mwalimu angeendelea kuwepo ndani ya CCM, angeiambia nini kutokana na malalamiko ya wananchi kwamba wanakiuka misingi na maadili yake?
Jibu: Angeiambia yale yale, aliyowaambia karibu ya siku zake za mwisho, kwamba misingi ya CCM na itikadi yake ipo. Ndiyo katiba ya chama hicho. Lakini, wanachama wa CCM na viongozi wake wametetereka na wanaendelea kutetereka katika kutetea na kuishi kwa mujibu wa misingi hiyo.
Swali: Mwalimu aliwahi kusema CCM siyo baba yake, wala mama yake. Unafikiri bado angeendela kuwapo ndani ya CCM au angewaambia nini Watanzania?
Jibu: Sidhani kama angerudisha kadi kwa CCM, siwezi kumsemea maana hayupo, lakini nadhani angeendelea kuwa mzee anayeishauri CCM, kuhakikisha kwamba haiendelei kupotoka, ikiacha misingi yake na angeendelea kuvishauri vyama vya upinzani ili vifanye kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kabla ya kufariki kwake, Mwalimu alisema hajaona chama cha upinzani kinachoweza kutawala Tanzania, ndiyo maana alibaki CCM. Mimi naishauri CCM izingatie misingi na sera zake.
No comments
Post a Comment