Writen by
sadataley
9:05 AM
-
0
Comments
Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amekana mashtaka yote yanayomkabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou Bensouda anayesimamia kesi hiyo, alisema watuhumiwa wawili waliofikishwa mahakamani hapo jana, Ruto na mtangazaji wa Redio, Joshua arap Sang wanakabiliwa na mashtaka matatu kila mmoja, ambayo ni kuwalazimisha watu kukimbia makazi yao, mauaji na kuchochea ghasia.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa siku chache baada ya Bunge la Kenya kupiga kura kutaka nchi hiyo ijitoe uanachama wa ICC, wakieleza kwamba imekuwa haina tija na inatumiwa kuwakandamiza Waafrika.
Ruto ambaye alionekana kujiamini alifika kwenye jengo la Mahakama akiwa ameambatana na baadhi ya wabunge waliosafiri kutoka Kenya hadi The Hague kwa ajili ya kumuunga mkono.
Mwendesha Mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda alianza kwa kusoma mashtaka matatu yanayomkabili kiongozi huyo wa Kenya na akaiomba Mahakama hiyo kumtia hatiani kutokana na vurugu zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Akiwasilisha hoja ya mashtaka, Bensouda alisema kuwa Ruto ni mwanasiasa aliyejawa na kiu ya madaraka na wakati fulani aliitii kiu yake kwa gharama ya maisha ya wengine. Alieleza kuwa Ruto alianzisha machafuko alipoona shabaha yake kutwaa madaraka kwa njia ya kura kushindwa.
“Ruto alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu sana ambaye alikuwa tayari kuratibu uhalifu dhidi ya binadamu ili kukidhi matakwa yake ya kutwaa madaraka.
Ni vigumu sana kutathmini maumivu na mateso waliyoyapata wanaume, wanawake na watoto ambao baadhi yao walichomwa moto huku macho yao yakishuhudia kile kilichotendeka. Wengi waliteswa hadi kufa huku wengine wakitimuliwa kutoka kwenye nyumba zao na kwenda kuishi uhamishoni,” alisema Bensouda katika sehemu ya hoja zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji.
Akieleza zaidi mahakamani hapo, Bensouda alisema kuwa Ruto na wenzake waliapa kutwaa madaraka kwa njia yoyote na walipoona jaribio lao kwa kuingia Ikulu kwa njia ya kura limeshindikana walianzisha hila kwa kuchochea machafuko ya kikabila.
Alisema upande wa walalamikaji uko tayari kuthibitisha madai kwamba Ruto alihusika kuandaa mashambulizi dhidi ya wananchi wa kabila la Kikuyu.
“Tupo tayari kudhibitisha madai yetu pasipo na shaka yoyote kwamba mashambulizi ya Wakikuyu yaliratibiwa na kutekelezwa na wahusika hawa,” alisema Bensouda.
Wakati Bensouda akiendelea kuwasilisha ushahidi upande wa pili, Ruto alionekana kuwa mtulivu na wakati fulani alitikisa kichwa na kisha akanyanyua glasi ya maji na kunywa. Kuna wakati pia alitabasamu na kuendelea kufuatilia kwa makini ushahidi wa upande wa walalamika.
No comments
Post a Comment