Writen by
sadataley
12:50 PM
-
0
Comments
Na Kelvin Matandiko, MwananchiSimiyu. Siyo kundi la Sungusungu, Polisi Jamii au askari wa makundi ya kiharakati au kisiasa unaoweza kufahamu. Hakuna ofisi wala vikao wanavyokaa kusikiliza mashtaka kabla ya uamuzi, mbaya zaidi hakuna anayejitambulisha kama mfuasi wa baraza hilo, lakini linatoa hukumu na kutekeleza mauaji ya kutisha.
Taarifa zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana pekee, wastani wa watu watatu walikuwa wakiuawa kila wiki na kikundi hicho cha watu kinachofahamika kama Baraza la Kimila katika Mkoa wa Simiyu, wakiwamo wanawake na watoto.
Wanachama wa kikundi hicho maarufu Dagashida, hufahamiana muda wa kupokezana ‘Mbiu’inaposikika kama ishara ya kuhudhuria tukio la utoaji wa hukumu.
Unaweza kulinganisha na Kundi la Al-Shabaab, kwani baraza hilo hufanya maasi na kusambaa msituni kwa muda wa siku zisizopungua tano wakihofia kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi.
Baraza hilo ni mfano wa kamati ya ulinzi au mahakama inayojiendesha kwa kufuata miiko na kanuni zake katikati ya Serikali inayoendeshwa kwa utawala wa sharia, likidaiwa kutoka Kabila la Wasukuma na jamii ya Kinyantuzu waliopo Mkoa wa Simiyu.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu aliyeomba kutotaja jina lake gazetini kwa sababu za siyo msemaji wa polisi alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ya kikatili akishauri atafutwe mhusika ili atoe ufafanuzi kuhusu matukio hayo.
Hali ilivyo kwa sasa
Mwandishi wa gazeti hili alifanikiwa kufika Vijiji vya Igangabilili, Nyamiswi, Badugu, Shigala, Budalabujiga na Mikoma vilivyopo Wilaya za Itilima, Bariadi, Busega na maeneo mengine mkoani humo.
Hofu iliyopo siyo kwa wanakijiji tu, bali hata mgeni yeyote, wakiwamo watumishi wa Serikali kama walimu, watakaoonekana kuwa tofauti na jamii hiyo.
Taarifa zinaonyesha kuwa hata kwa mwandishi wa habari atakayebainika kuingilia utaratibu wao, atakutana na adhabu kali.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamiswi Kata ya Gambushi, Leah Muhami anasema kuwa hali ni mbaya na kwamba mbali ya kuchoshwa na ukatili huo, wanakijiji wamekuwa wakihofia kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuogopa kuonekana wasaliti kwa baraza hilo wakihofu kugharimu maisha yao.
“Yaani wakikusikia unatoa taarifa zao polisi, lazima maisha yako yatakuwa hatarini. Watakushughulikia na wanapofanya mauaji hutakiwi kuonekana ukiwa na simu ya mkononi, ”anasema Leah.
No comments
Post a Comment