Writen by
sadataley
9:59 AM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amewavua madaraka maofisa wanne wa polisi kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo, huku akiwafukuza kazi askari saba wa vyeo vya chini pamoja na kuwapa onyo wawili kutokana na kushiriki moja kwa moja katika matukio ya wizi, kusababisha mauaji na uzembe kazini.
Nchimbi alipoulizwa sababu za kutowafukuza kazi maofisa wa juu, badala yake amekuwa akiwavua madaraka alisema, “Hawa niliowataja sio kama wanahusika, tunawavua madaraka kwa sababu ya kushindwa kusimamia majukumu yao kikamilifu. Madaraka waliyopewa yamewashinda hivyo tumewanyang’anya.”
Maofisa waliovuliwa madaraka ni Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Arusha, Mrakibu wa Polisi Ramadhan Giro, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mvomelo, Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha Polisi Dumila, Juma Pamba na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kasulu, Daniel Bendarugaho.
Hii ni mara ya pili kwa Dk Nchimbi kuwachukulia hatua maofisa wa polisi, kwani Machi mwaka huu waziri huyo aliwafukuza kazi maofisa watano wa polisi na kumsimamisha kazi kwa mwezi mmoja Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi hilo, Renatus Chalamila kutokana na kuhusishwa na rushwa katika kuajiri.
Pia aliwafukuza makuruta 95 waliokuwa Chuo cha Polisi (CCP), Moshi kutokana na kugundulika kutumia rushwa kupata ajira.
Maofisa watatu kati ya hao watano walifukuzwa kutokana na kugundulika kuwa walikamata dawa za kulevya aina ya cocaine lakini zilipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ziligundulika ni chumvi na sukari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk Nchimbi alisema amechukua hatua hiyo baada ya kupata ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza matukio yaliyotokea kati ya Desemba 26 mwaka jana na Mei 18 mwaka huu.
Alisema matukio hayo ni lile la gari la FFU kutumika kubeba bangi mkoani Kilimanjaro, polisi kutumia fuvu la kichwa cha binadamu kumbambikizia mfanyabiashara kesi kwa lengo la kupata fedha mkoani Morogoro pamoja na mauaji ya mfanyabiashara wilayani Kasulu yaliyofanywa na askari wawili.
Sababu za kuvuliwa madaraka
Alisema Giro amevuliwa madaraka kutokana na kushindwa kusimamia kikamilifu askari na maofisa walio chini yake na kusababisha Mei 18 mwaka huu, kutumika kwa gari la polisi lenye namba za usajili PT 2025 kubeba bangi kilogramu 540 zenye thamani ya Sh81 milioni.
“Yeye ndiye msimamizi wa magari yote ya FFU na ndiye mkuu wa kikosi hicho katika mkoa huo, kwa utaratibu wa magari ya FFU hayaendi popote bila yeye kujua, ikitokea hakujua na mpaka gari limevuka nje ya mkoa maana yake hakutimiza wajibu wake ipasavyo, kamati ilishauri avuliwe madaraka,” alisena na kuongeza;
“Nilipoipata taarifa ya kamati juzi niliagiza polisi wamvue madaraka na hilo lilifanyika siku hiyohiyo.”
Alisema kuwa Inspekta Ramadhani ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mvomelo alikuwa na taarifa juu ya mpango wa kufanyika utapeli katika maeneo ya Dakawa na Dumila ambapo matapeli walipanga kwa kushirikiana na polisi wasio waaminifu kumbambikizia kesi ya fuvu la kichwa cha binadamu mfanyabiashara, Samson Mwita Kihindi wa Dumila kwa lengo la kupata fedha.
Alisema Inspekta Mpamba alionyesha udhaifu katika utendaji wa kazi kwa kutosimamia kikamilifu askari waliopo chini yake, kitendo kilichosababisha askari hao kujipangia kazi nje ya utaratibu, ikiwa ni pamoja na kuhusika katika tukio hilo la kubambikizia kesi.
Alisema ASP Bendarugaho amevuliwa madaraka kutokana na kushindwa kusimamia upelelezi wa jalada la kesi ya mauaji ya Gasper Mussa Sigwavumba (36) ambaye alipigwa na askari wawili (Koplo Peter na PC Sunday) Disemba 25, mwaka jana, kuwekwa katika mahabusu ya kituo kidogo cha polisi cha Heru Ushingo wilayani Kasulu, bila msaada wa matibabu na kufariki dunia siku moja baadaye.
Waliofukuzwa kazi
“Koplo Edward wa FFU mkoani Arusha na PC George wa kituo cha polisi Ngarananyuki wilaya ya Arumeru mkoani humo, wamefukuzwa kazi Mei 20 mwaka huu baada ya kukiri kosa la kusafirisha bangi kwa kutumia gari la polisi walilolifanya Mei 18,” alisema na kuongeza;
“Nimewafukuza kazi Sajenti Mohamed na Koplo Nuran wa kituo cha polisi Dumila na Sajenti Sadick Madodo wa kituo cha polisi Dakawa, kutokana na kushirikiana na raia wawili matapeli ambao walisambaza fuvu la kichwa cha binadamu kwa Kihindi. Askari hao wamefukuzwa kazi na wameshtakiwa kwa uhalifu waliotenda.”
Alisema Koplo Peter na PC Sunday wamefukuzwa kazi baada ya kumpiga Sigwavumba na kisha kumweka katika kituo cha polisi bila msada wowote mpaka alipokutwa na mauti.
Aliyepanda cheo,waliopewa onyo
Alisema ASP Francis Duma ambaye alikuwa kiongozi wa tukio la kukamata gari la polisi lililokuwa limebeba bangi mkoani Kilimanjaro amepandishwa cheo na kuwa Mrakibu wa polisi kuanzia juzi.
“Askari 14 waliokuwa na Duma siku ya tukio nimeagiza wapongezwe na Mkuu wa Jeshi la polisi nchini, IGP Said Mwema kwani wako chini ya mamlaka yake” alifafanua.
Aliwataja waliopewa onyo kuwa ni Ispekta Salum Juma Kingu wa kikosi cha FFU mkoani Kilimanjaro ambaye alibaki katika gari umbali wa mita 80, kutoka nyumba ya Koplo Edward ambaye alipelekwa kutoka wilayani Moshi, kukabidhi vifaa vya jeshi hilo na kusababisha mtuhumiwa huyo kutoroka.Mwingine ni Ispekta Mikidadi Galilima ambaye alishindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kushidnwa kumshauri Giro katika usimamizi wa rasilimali za kikosi.
Kamati iliyoundwa kuchunguza matukio hayo iliongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Malalamiko cha polisi, Agustino Shayo, Kamishna Msaidizi wa polisi, ACP Germanus Muhume na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Manland Tesha.
No comments
Post a Comment