Writen by
sadataley
9:55 AM
-
0
Comments
Na Beatrice Moses na Raymond Kaminyonge
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema itawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akiwatuhumu kwa kulidanganya Bunge.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe baada ya kumhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert Mrango kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2011/2012.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka huo kiasi cha Sh348,075,000,000 fedha za ndani zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililotajwa kuwa ni la mradi maalumu (Special Road Construction Project) hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni.
“Ni vizuri leo uiambie kamati fedha hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi zilipunguzwa kiasi cha Sh95 bilioni na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi, zilibakia Sh252.975bilioni katika kifungu hicho lakini kuna bilioni 100 zimetumika visivyo,” alisema Zitto, ambaye pia ni Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Alisema katika majumuisho ya Bajeti ya wizara hiyo, Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Lukuvi walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha.
Alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa ajili ya kuanzia kazi za ujenzi wa barabara,” Zitto alisema akikariri maneno ya Dk Magufuli wakati anawasilisha bajeti.
“Fedha hizi zitachangia miradi ya wafadhili,” haya yalikuwa maneno ya Dk Mwakyembe wakati akifanya majumuisho.
“Hizi ni fedha kwa ajili ya counterpart fund,” alimkariri Lukuvi wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo.
Zitto alisema CAG alihoji mwaka huu kuhusu matumizi ya fedha hizo na alitoa taarifa akidai kuwa fedha hizo zilikuwa miradi hewa na kasma kivuli.
Zitto alisema kuwa Dk Magufuli na Katibu Mkuu wake walipohojiwa walidai kutumia fedha hizo kulipa madeni.
“Kwa nini mlidanganya Bunge? Mliomba fedha za kuanza miradi maalumu. Hamkuomba fedha za madeni. Kwa nini mliunda kasma kivuli na kuifuta baada ya pesa kulipwa?” Zitto alimhoji Balozi Mrango.
Katika majibu yake, Balozi Mrango alisema kwa nia njema, fedha hizo zilitumika kuwalipa makandarasi waliokuwa wamechachamaa, huku baadhi yao wakisisitiza kusitisha kuendelea na miradi. Hivyo wakalazimika kuomba fedha kwa njia hiyo ili miradi kuendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Zitto hakuridhishwa na majibu hayo akisema hapakuwa na haja ya kutumia fedha hizo kuwalipa makandarasi wakati kulikuwa na kasma yao ya awali. Alisema kama kulikuwa na haja hiyo, wizara isingeita mradi rasmi.
“Jambo hili siyo sahihi hata kidogo kulidanganya Bunge na hadi sasa wewe na waziri wako hamuonyeshi kukubali kosa hili, hata Waziri Lukuvi naye alisisitiza bungeni kwamba fedha hizo zinaombwa ili kutekeleza mradi maalumu lakini sasa imebainika sivyo, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge tutawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ili wahojiwe nao wajieleze kwa kulidanganya,” alisema Zitto.
Pia kamati hiyo imeitaka wizara hiyo kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu matumizi ya Sh100 bilioni zilizotumika kinyume na maombi yaliyowasilishwa kwenye Bajeti ya mwaka huo wa fedha.
CAG ameshauri madeni yote ambayo Wizara ya Ujenzi inadaiwa yaorodheshwe ili yawe wazi kuepuka migongano katika matumizi ya fedha.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Lukuvi alisema haelewi chochote na kusisitiza kuwa akipata taarifa rasmi za Kamati ya PAC, atatoa ufafanuzi.
Halmashauri zinavyotafuna mabilioni
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAACc), imeeleza namna mamilioni ya fedha za Serikali zinavyoibwa kutoka Hazina kupitia halmashauri za wilaya huku Ilala ikitajwa kuongoza kwa ufisadi huo.
Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohammed aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Hazina imekuwa ikipeleka fedha kwenye halmashauri zikiwa zimezidi na kwamba kiasi kinachozidi hakirudishwi badala yake huliwa.
Alisema kamati hiyo imefanya uchunguzi kwenye halmashauri 43 na kubaini kwamba mtindo huo ndiyo unaotumika kuiba fedha za Serikali.
“Mwaka 2011/12 kiasi cha Sh1.5 bilioni zilipelekwa zikiwa zimezidi kwenye halmashauri hizo lakini hazikurudishwa Hazina kama inavyoonyesha kwenye ripoti ya CAG.
Alisema kati ya kiasi hicho, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilipewa ziada ya Sh213 milioni ikifuatiwa na Geita iliyopewa Sh129 milioni.
“Fedha hizo za mishahara zilipelekwa kwenye halmashauri hizo na Hazina kimakosa zikiwa zimezidi lakini watendaji wa hawakuzirudisha kama wanavyotakiwa kisheria badala yake zikayeyuka,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa uchunguzi huo pia ulibaini kwamba katika halmashauri hizo 43 kiasi cha Sh693 milioni hulipwa mishahara hewa ambayo wafanyakazi wake walishakufa na wengine kustaafu.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ililipa mishahara hewa yenye thamani ya Sh79.4 milioni ikifuatiwa na Ukerewe iliyolipa Sh57.5 milioni.
Kwa upande wa fedha za miradi ya maendeleo, mwaka 2011/12, Hazina ilipeleka katika Halmashauri ya Mbarali, Mbeya Sh724 milioni kwa ajili ya Mradi wa Maendeleo ya Elimu Sekondari wakati mradi huo ulikuwa ukihitaji Sh70 milioni tu.
“Kiasi cha Sh654 milioni zilipelekwa kimakosa na Hazina lakini badala ya kurudishwa zilitumiwa katika mazingira ya kutatanisha,” alisema.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ilipelekewa ziada ya Sh500 milioni na Mvomero ilipewa Sh85 milioni. “Kuna mtandao mkubwa wa Hazina na halmashauri ambao ukiachwa utaendelea kupoteza fedha nyingi za walipakodi,” alisema.
Chanzo http://www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment