Writen by
sadataley
4:16 PM
-
0
Comments
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (kulia)
akimkabidhi zawadi mkurugenzi msaidizi wa mawasiliano na masuala ya
kijamii wa Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa), Nicolas Maingot baada ya
kufungua rasmi semina ya mafunzo ya mawasiliano kwa vyama vya soka
ambavyo ni wanachama wa CECAFA, kushoto ni Rais wa CECAFA, Leodegar
Tenga. Picha na Michael Matemanga.
Na Vicky Kimaro, Mwananchi
Dar es Salaam. Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa) limeahidi kuzisaidia timu zinazotoka Ukanda wa Afrika Mashariki
na Kati (Cecafa) ili zifanikiwe zaidi katika soka na kuweka ushindani
duniani kote.
Akizungumza katika semina maalumu iliyoandaliwa na
Cecafa Jijini Dar es Salam jana, mkurugenzi msaidizi wa mawasiliano na
masuala ya kijamii wa Fifa, Nicholas Maingot alisema shirikisho hilo
litatoa misaada ya kifedha, kiutawala na pia kuanzisha programu
mbalimbali za kuinua soka katika ukanda huo.
“Siku zote ukanda wa Cecafa umekua mstari wa mbele
kuwajibika na kuhakikisha mpira wa miguu unazidi kupata umaarufu
duniani. Tunashukuru kwa kujitoa huko na sisi tunaahidi kuendelea
kufanya kazi bega kwa bega na shirikisho hili ili kuupa mpira umaarufu
zaidi hususani kwa kutumia mawasiliano,” alisema Maingot.
Fifa kwa kushirikiana na Cecafa wanaendelea na
semina ya siku mbili jijini Dar es Salam yenye lengo la kuwaongezea
ujuzi viongozi wanachama wa Cecafa juu ya umuhimu wa mawasiliano kwenye
soka hususani katika karne hii ya digitali. Wanachama wa Cecafa ni
Burundi, Kenya, Djibout, Eritrea, Ethiopia, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini,
Uganda, Tanzania na Zanzibar.
Awali semina hiyo ilikuwa ifunguliwe na katibu
mkuu wa Fifa, Jerome Valcke, lakini jana wajumbe wa mkutano huo
waliwekewa CD ya katibu huyo akiwaomba radhi kutohudhuria mkutano huo
kwa vile wakati akijiandaa kuja Tanzania, mke wake aliumwa na uchungu na
amebahatika kujifungua mtoto wa kike aliyepewa jina la Valentine.
Semina hiyo inaendelea kwenye Hoteli ya Double
Tree jijini, na lengo la semina hiyo ni kujadili masuala mbalimbali ya
utawala wa soka na changamoto zinazoikabili Cecafa. Pia masuala ya
mawasiliano na upashanaji habari katika nchi za Afrika Mashariki na
Kati.
No comments
Post a Comment